1 Samweli 1

1 Samweli 1

Kuomba kwake Hana.

1Kulikuwa na mtu mmoja wa Ramataimu-Sofimu ulioko milimani kwa Efuraimu, jina lake ni Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, mtu wa Efuraimu.[#1 Mambo 6:11-12,19-20.]

2Naye alikuwa na wanawake wawili, mmoja jina lake Hana, wa pili jina lake Penina; huyu Penina alikuwa ana watoto, naye Hana alikuwa hana watoto.[#1 Mose 29:31.]

3Yule mtu alitoka mwaka kwa mwaka mjini kwake akipanda kwenda Silo kumtambikia Bwana Mwenye vikosi na kumtolea ng'ombe ya tambiko. Huko wana wawili wa Eli, Hofuni na Pinehasi, walikuwa watambikaji wa Bwana.[#Yos. 18:1.]

4Kila siku, Elkana alipotoa ng'ombe ya tambiko, akampa mkewe Penina na wanawe wa kiume na wa kike vipande vya nyama.

5Naye Hana akampa kipande kimoja mara mbili, kwani alimpenda Hana, lakini Bwana alikuwa amelifunga tumbo lake.

6Naye mchukivu wake akamsikitisha sana kwa kumchokoza, kwa kuwa Bwana alilifunga tumbo lake.

7Ndivyo, alivyofanya mwaka kwa mwaka: kila alipopanda kuingia Nyumbani mwa Bwana, yule alimsikitisha, hata akalia machozi na kukataa kula.

8Ndipo, Elkana alipomwuliza mkewe Hana: Mbona unalia? Mbona huli nyama? Mbona moyo wako unakuwa mbaya hivyo? Kumbe mimi si mwenzio mwema kuliko wana kumi?

9Walipokwisha kula na kunywa huko Silo, Hana akaondoka; naye mtambikaji Eli alikwa amekaa katika kiti chake penye mhimili wa mlango wa Jumba la Bwana.

10Roho yake Hana ilikuwa yenye uchungu, akamlalamikia Bwana na kulia machozi mengi;

11akaaga kiagio na kusema: Bwana Mwenye vikosi, kama utautazama ukiwa wa kijakazi wako, ukinikumbuka, usimsahau kijakazi wako ukimpa kijakazi wako mwana wa kiume, nitamtoa, awe wako, Bwana, siku zote za maisha yake, nacho kinyoleo hakitafika kichwani pake.[#4 Mose 6:2-21; Amu. 13:5.]

12Ikawa, alipozidi kumlalamikia Bwana, Eli alikuwa anakiangalia kinywa chake.

13Lakini Hana alikuwa anasema humo ndani moyoni mwake, midomo yake ikachezacheza tu, lakini sauti yake haikusikilika; ndipo, Eli alipomwazia kuwa amelewa.

14Eli akamwambia: Utalewa mpaka lini? Acha, mvinyo, uliyoinywa, ikuondokee!

15Hana akajibu na kumwambia: Sivyo, bwana, mimi ni mwanamke mwenye roho nzito, mvinyo au kileo cho chote sikunywa, nitammwagia Bwana roho yangu tu.[#Sh. 62:9.]

16Usimwazie kijakazi wako kuwa mwanamke asiyefaa! Kwani hata sasa nimesema kwa wasiwasi na kwa uchungu wangu mwingi.

17Eli akajibu na kumwambia: Nenda na kutengemana! Mungu wa Isiraeli na akupe maombo yako, uliyomwomba.

18Akasema: Kijakazi wako na ayaone macho yako, yakimtazama kwa upole. Kisha huyo mwanamke akaenda zake, hata kula akala, nao uso wake haukuwa tena kama hapo kwanza.

19Kesho yake wakaamka na mapema, wakaja kumwangukia Bwana, kisha wakarudi kwenda nyumbani kwao huko Rama. Elkana alipomtambua mkewe Hana, Bwana naye akamkumbuka.[#1 Mose 30:22.]

Samweli anazaliwa, halafu anatolewa kuwa wa Bwana.

20Ikawa, siku zilipotimia, Hana akapata mimba, akazaa mtoto mwanamume, akamwita jina lake Samweli (Nimesikiwa na Mungu) kwa kwamba: Nimemwomba kwa Bwana.

21Kisha yule Elkana alipopanda pamoja nao wote walio wa mlango wake kumtolea Bwana ng'ombe ya tambiko ya zile siku, walizomwagia,

22Hana hakupanda nao, kwani alimwambia mumewe: Sharti huyu mwana kwanza aliache ziwa Kisha nitampeleka, amtokee Bwana usoni pake, akae hapo siku zote.

23Mumewe Elkana akamwambia: Yafanye yaliyo mema machoni pako! Kaa, mpaka umzoeze kuacha kunyonya! Naye Bwana na alitimize neno lako. Ndipo, mama ya mtoto alipokaa na kumnyonyesha mwanawe, mpaka akimzoeza kuacha kunyonya.

24Kisha akapanda naye, alipokwisha kumzoeza kuacha kunyonya, akachukua hata ng'ombe watatu na kapu moja la unga na kiriba cha mvinyo, akampeleka Silo Nyumbani mwa Bwana, yule mtoto akingali mdogo.

25Wakachinja ng'ombe, kisha wakampeleka yule mtoto kwa Eli.

26Hana akamwambia: Bwana, hivyo roho yako, bwana wangu, ilivyo nzima bado, mimi ni mwanamke yule aliyesimama humu Nyumbani pamoja na wewe kumlalamikia Bwana.

27Nalimlalamikia kwa ajili ya mtoto huyu, Bwana akanipa maombo yangu, niliyomwomba.

28Mimi nami ninamtoa na kumpa Bwana, awe wake siku zote, atakazokuwapo, kwani ameombwa kwake Bwana. Kisha wakamtambikia Bwana huko.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania