The chat will start when you send the first message.
1Kisha Samweli akawaambia Waisiraeli wote: Tazameni! Nimeviitikia vinywa vyenu katika mambo yote, mliyoniambia, nikawapa hata mfalme wa kuwatawala.[#1 Sam. 8:7,22; 11:15.]
2Sasa tazameni! Huyu mfalme huwatangulia, mimi nami nimekwisha kuwa mzee mwenye mvi, nao wanangu mnao kwenu, nami nimefanya mwenendo machoni penu tangu utoto wangu mpaka siku hii ya leo.
3Basi, nitazameni, mniumbue mbele ya Bwana na mbele ya mtu wake, aliyempaka mafuta, kama nimechukua ng'ombe wa mtu, au kama nimechukua punda wa mtu, au kama nimekorofisha mtu, au kama nimeponda mtu, au kama nimechukua mkononi mwa mtu fedha za kupenyezewa za kuyapofusha macho yangu! Kama ndivyo, nitawarudishia ninyi.[#4 Mose 16:15.]
4Wakamwambia: Hukutukorofisha, wala hukutuponda, wala hukuchukua cho chote mkononi mwa mtu.
5Ndipo, alipowaambia: Siku hii ya leo Bwana ni shahidi wangu kwenu, naye aliyempaka mafuta ni shahidi wangu, ya kuwa hamkuona cho chote mkononi mwangu. Wakasema: Kweli, ndiye shahidi.
6Kisha Samweli akawaambia watu: Ni yeye Bwana aliyemwumba Mose naye Haroni, aliyewatoa baba zenu katika nchi ya Misri.
7Lakini sasa jipangeni, nisemezane nanyi usoni pake yeye Bwana kwa ajili ya wongofu wote, Bwana aliowatendea ninyi na baba zenu!
8Yakobo alipoingia Misri, baba zenu walipomlilia Bwana, Bwana akamtuma Mose na Haroni, akawatoa baba zenu huko Misri, akawakalisha mahali hapa.[#2 Mose 3:7.]
9Walipomsahau Bwana Mungu wao, akawauza mkononi mwa Sisera, mkuu wa vikosi vya Hasori, namo mikononi mwa Wafilisti, namo mkononi mwa mfalme wa Moabu, walipowapelekea vita.[#Amu. 3:12; 4:2; 10:7; 13:1.]
10Lakini walipomlilia Bwana na kusema: Tumekosa tukimwacha Bwana na kuyatumikia Mabaali na Maastaroti, sasa tuponye mikononi mwa adui zetu, tukutumikie,
11ndipo, Bwana alipomtuma Yerubaali na Bedani na Yefuta na Samweli, akawaponya mikononi mwa adui zenu waliowazunguka, mkapata kukaa na kutulia.[#Amu. 6:14; 7:3; 11:29.]
12Tena mlipoona, ya kuwa Nahasi, mfalme wa wana Amoni, anawajia, ndipo, mliponiambia: Hivi sivyo, sharti mfalme atutawale. Naye Mungu wenu alikuwa mfalme wenu.[#1 Sam. 8:19.]
13Sasa mfalme yuko, mliyemchagua kwa kumtaka; tazameni! Bwana amewapa naye mfalme wa kuwatawala.
14Kwa hiyo mcheni Bwana na kumtumikia na kuisikia sauti yake, msikikatae kinywa chake Bwana, ila mmfuate Bwana Mungu wenu, ninyi na mfalme anayewatawala!
15Lakini msipoisikia sauti ya Bwana na kukikataa kinywa chake Bwana, mkono wa Bwana utawapingia, kama ulivyowapingia baba zenu.
16Sasa simameni hapa, mlione jambo hili kubwa, Bwana atakalolifanya machoni penu!
17Je? Mavuno ya ngano hayakutimia? Leo hivi nitamwomba Bwana, alete ngurumo na mvua, mpate kutambua na kuona, ya kuwa hapo mlipojitakia mfalme mlifanya yaliyo mabaya sana machoni pake Bwana.
18Basi, Samweli alipomwomba Bwana, Bwana akaleta ngurumo na mvua siku hiyohiyo; ndipo, watu wote walipoingiwa na woga wa kumwogopa sana Bwana, hata Samweli.
19Kisha watu wote wakamwambia Samweli: Waombee watumishi wako kwake Bwana Mungu wako, tusife! Kwani makosa yetu yote tumeyaongeza na kibaya hiki cha kujitakia mfalme.
20Samweli akawaambia watu: Msiogope! Kweli ninyi mmeyafanya hayo mabaya yote, lakini msijiendee tena mkiacha kumfuata Bwana, ila mtumikieni Bwana kwa mioyo yenu yote!
21Msiondoke kwake na kufuata mambo ya ovyoovyo tu yasiyofaa, nayo hayaponyi kwa kuwa ya ovyoovyo tu.[#5 Mose 32:37-38.]
22Kwani walio ukoo wake Bwana hatawatupa kwa ajili ya Jina lake kuu; kwani ndiye Bwana mwenyewe aliyewataka kuwa ukoo wake.[#2 Mose 19:6.]
23Mimi nami hili na liniendee mbali, nisimkosee Bwana nikiacha kuwaombea! Ila nitawafundisha kuishika njia njema inyokayo.[#1 Sam. 7:8.]
24Ninyi mcheni tu Bwana na kumtumikia kweli kwa mioyo yenu yote, kwani mmeyaona makuu, Bwana aliyowafanyizia.[#2 Fal. 17:39.]
25Lakini mtakapofanya mabaya, mtaangamizwa ninyi na mfalme wenu.