The chat will start when you send the first message.
1Dawidi akatoka huko, akaja kuponea pangoni kwa Adulamu. Kaka zake na mlango wote wa baba yake walipovisikia, wakashuka kwake.[#Sh. 57:1.]
2Tena wakakusanyika kwake watu wote pia waliosongeka nao wote waliokuwa wenye madeni nao wote waliokuwa na uchungu rohoni mwao, akawa mkuu wao, hivyo akapata watu kama 400 waliokuwa naye.[#Amu. 11:3.]
3Kisha Dawidi akatoka huko, akaja Misipe wa Moabu, akamwambia mfalme wa Moabu: Acha, baba yangu na mama yangu waje kukaa kwenu, hata nitakapojua, Mungu atakayonifanyizia.
4Kisha akawapeleka kwa mfalme wa Moabu, wakakaa naye siku zote, Dawidi alipokuwa hapo ngomeni.
5Kisha mfumbuaji Gadi akamwambia Dawidi: Usikae hapa ngomeni! Ondoka, uende kukaa katika nchi ya Yuda. Ndipo, Dawidi alipokwenda mwituni kwa Hereti.[#1 Sam. 23:14; Sh. 63:1.]
6Sauli aliposikia, ya kuwa Dawidi amejulikana, alipo pamoja na watu waliofuatana naye, yeye Sauli alikuwa anakaa Gibea chini ya miombo kilimani, akiushika mkuki wake mkononi, nao watumishi wake wote wakawa wakisimama na kumzunguka.
7Ndipo, Sauli alipowaambia watumishi wake waliosimama na kumzunguka: Sikilizeni, ninyi Wabenyamini! Mwana wa Isai atawezaje kuwapa ninyi nyote mashamba na mizabibu? Tena atawezaje kuwaweka ninyi nyote kuwa wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia?
8Kwani ninyi nyote mmenivunjia maagano, kwani hakuna aliyeyafunua masikioni pangu, ya kuwa mwanangu alifanya agano na mwana wa Isai wala hakuna kwenu aliyenionea uchungu akiyafunua masikioni pangu, ya kuwa mwanangu alimchochea mtumishi wangu, aniotee, kama yanavyoelekea leo.[#1 Sam. 18:3.]
9Ndipo, Doegi wa Edomu aliyesimama pamoja na watumishi wa Sauli alipojibu akisema: Nimemwona mwana wa Isai, alipoingia Nobe kwa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu.[#1 Sam. 22:22; Sh. 52:2.]
10Huyu akamwuliza Bwana kwa ajili yake, akampa pamba za njiani, nao upanga wa yule Mfilisti Goliati akampa.[#1 Sam. 21:6-9.]
11Mfalme akatuma kumwita mtambikaji Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, na mlango wote wa baba yake waliokuwa watambikaji huko Nobe, nao wakaja wote kwa mfalme.
12Sauli akasema: Sikiliza, mwana wa Ahitubu! Akajibu:
Nipo hapa, bwana wangu,
13Sauli akamwuliza: Mbona mmenivunjia maagano, wewe na mwana wa Isai? Nawe umempa chakula na upanga, ukamwuliza Mungu kwa ajili yake, apate kuniinukia na kuniotea kama yanavyoelekea leo.
14Ahimeleki akamjibu mfalme akisema: Miongoni mwa watumishi wako wote yuko nani aliye mwelekevu kama Dawidi? Naye ni mkwe wa mfalme, tena huingia katika njama zako, huheshimiwa nyumbani mwako.[#1 Sam. 18:22,27.]
15Je? Siku hiyo ilikuwa ya kwanza ya kumwuliza Mungu kwa ajili yake? Hilo lisinipate! Mfalme asimsingizie mtumishi wake na mlango wote wa baba yangu jambo kama hilo! Kwani mtumishi wako hayajui haya yote, wala makubwa, wala madogo.
16Lakini mfalme akasema: Utakufa kweli, wewe Ahimeleki na mlango wote wa baba yako.
17Kisha mfalme akawaagiza wapiga mbio waliosimama hapo na kumzunguka: Wageukieni hawa watambikaji wa Bwana, mwaue! Kwani mikono yao nayo humsaidia Dawidi, tena walijua, ya kuwa anakimbia, lakini hawakuyafunua masikioni pangu. Lakini watumishi wa mfalme wakakataa kuinyosha mikono yao kuwakumba watambikaji wa Bwana.
18Ndipo, mfalme alipomwambia Doegi. Waangukie wewe, uwakumbe hawa watambikaji! Basi, Doegi wa Edomu akawaangukia, akawakumba hawa watambikaji, akawaua siku hiyo watu 85 waliovaa visibau vya mtambikaji vya ukonge.
19Kisha akaupiga ule mji wa Nobe kwa ukali wa upanga, waume kwa wake, vijana kwa wachanga, ng'ombe na punda na kondoo, wote pia akawaua kwa ukali wa upanga.[#1 Sam. 21:1.]
20Akapona mtoto mmoja tu, mwana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, jina lake Abiatari, naye akamkimbilia Dawidi.
21Abiatari akamsimulia Dawidi, ya kuwa Sauli amewaua watambikaji wa Bwana.
22Dawidi akamwambia Abiatari: Siku hiyo, nilipojua, ya kuwa Doegi wa Edomu yuko, nikajua, ya kuwa atamsimulia Sauli hayo yote. Kwa hiyo ni mimi niliyewapatia wote walio wa mlango wa baba yako mambo hayo.[#1 Sam. 22:9.]
23Kwa hiyo kaa kwangu, usiogope! Kwani atakayeitaka roho yako sharti kwanza aipate roho yangu, kwangu mimi utakuwa umeangaliwa vema.