1 Watesalonike 2

1 Watesalonike 2

Jinsi Paulo alivyowapigia mbiu.

1Ndugu, mwajua wenyewe, tulivyoingia kwenu, ya kuwa hatukuingia bure.[#1 Tes. 1:5,9.]

2Huko Filipi, tulipoanzia, tuliumizwa na kukorofishwa vibaya, kama mnavyojua; lakini Mungu wetu akatupa mioyo ya kuwatangazia Utume mwema wa Mumgu pasipo woga wo wote na kuushindania sana.[#Tume. 16:12,20-24; 17:1-5.]

3Kwani yale, tuliyowaonya, siyo ya kuwapoteza wala ya kuwapeleka penye uchafu wala ya kuwadanganya.[#2 Kor. 4:2; 11:7.]

4Ila kama tulivyojulika kwake Mungu kuwa wakweli wapaswao na kupewa Utume mwema, hivyo ndivyo, twasemavyo, siko kwamba tupendeze watu, ila tumpendeze Mungu ajulishaye, mioyo yetu ilivyo.[#Gal. 1:10; 1 Tim. 1:11.]

5Kwani hatukutumia maneno matamutamu ya kujipendezesha kwenu, kama mnavyojua, wala hatukujitendekeza kama wenye kuficha choyo; hapa Mungu ndiye anayetushuhudia.[#Tume. 20:33.]

6Wala hatukutaka kutukuzwa na watu, wala nanyi wala na watu wengine.[#Yoh. 5:41,44.]

7Tuliweza kuwa wenye macheo, maana tu mitume wake Kristo, lakini kati yenu tulikuwa wenye upole, kama mlezi akiwalea watoto wake.

8Vivyo hivyo na sisi tuliwatunukia ninyi, tukataka sana kuwagawia Utume mwema wa Mungu, hata mioyo yetu nayo, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu.

9Ndugu, mwayakumbuka masumbuko na maumivu yetu: tuliutangaza Utume mwema wa Mungu kwenu na kufanya kazi usiku na mchana, tukikataa kumlemea mtu wo wote wa kwenu.[#Tume. 20:33-34; 1 Kor. 4:12.]

10Ninyi pamoja na Mungu m mashahidi, jinsi tulivyowaendea ninyi mmtegemeao, maana tulikuwa wenye kumcha Mungu na wenye wongofu, mtu asione la kutuonya.

11Hilo nalo mwalijua: kama baba anavyowabembeleza watoto wake, vivyo hivyo tumewabembeleza ninyi kila mmoja wenu peke yake;

12tukawatuliza mioyo pamoja na kuwakaza, mfanye mwenendo uwapasao walio wake Mungu aliyewaitia ninyi kuuingia ufalme na utukufu wake.[#Ef. 4:1; Fil. 1:27.]

Mateso yatokayo kwa ndugu.

13Kwa sababu hii na sisi hatukomi kumshukuru Mungu kwamba: Mlipolisikia kwetu Neno lake Mungu mmelipokea si kama neno la watu, ila kama Neno lake Mungu, lilivyo kweli. Naye ndiye anayetenda nguvu mwenu mmtegemeao.[#1 Tes. 1:2; Gal. 1:11.]

14Kwani ninyi ndugu, mmepata kufanana na wateule wa Mungu walio wake Kristo Yesu katika nchi ya Yudea, kwani nanyi mmeteswa yaleyale na wenzenu wa kabila, kama nao wale walivyoteswa na Wayuda.[#Tume. 8:1; 17:5-6.]

15Ndio wao hao waliomwua naye Bwana Yesu, hata wafumbuaji, tena ndio waliotufukuza na sisi; hawampendezi Mungu kwa kupingana na watu wote.[#Mat. 23:37; Tume. 2:23; 7:52.]

16Kisha hujaribu kutukataza sisi, tusiwaambie wamizimu Neno la wokovu wao; hivyo huyatimiza makosa yao po pote. Lakini makali yamewafikia, waishie.[#Mat. 23:32-33.]

Hamu ya kuonana.

17Sisi ndugu tumetengwa nanyi kitambo cha sasa, tusionane nanyi uso kwa uso, lakini mioyo haikutengwa; kwa hiyo tulijipingia sana kuonana nanyi uso kwa uso, kwani tuliwatunukia sana.[#Rom. 1:11,13.]

18Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, mimi Paulo nilitaka mara moja, hata mara mbili, lakini Satani alituzuia.

19Kwani kingojeo chetu au furaha yetu au kilemba, tujivuniacho mbele ya Bwana wetu Yesu Kristo, atakapokuja, ndio nini, msipokuwa ninyi?[#Fil. 2:16; 4:1.]

20Kwani ninyi m utukufu wetu na furaha yetu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania