1 Timoteo 2

1 Timoteo 2

Kuwaombea watu wote.

1*Neno, ninalokuhimiza kupita yote, ni hili: Mwombe na kumwangukia Mungu na kumbembeleza na kumshukuru mkiwaombea watu wote,[#Fil. 4:6.]

2nao wafalme nao wote walio wakuu, tupate kukaa tukitulia na kutengemana vema, tumche Mungu na kuendelea vema katika mambo yote.

3Kwani hivi ni vizuri vya kumpendeza Mungu, mwokozi wetu.[#1 Tim. 1:1; 4:10.]

4Huyu anataka, watu wote waokolewe, wapate kutambua yaliyo ya kweli.[#Ez. 18:23; 2 Petr. 3:9.]

5Kwani Mungu ni mmoja, naye mpatanishaji wa Mungu na watu ni mmoja, ni yule mtu Kristo Yesu[#Rom. 3:29-30; Gal. 3:19-20; Ebr. 12:24.]

6aliyejitoa mwenyewe kuwa kole ya kuwakomboa wote; huu ndio ushuhuda utakaotangazwa po pote, siku zake zitakapotimia.*[#Gal. 1:4; 2:20; Tit. 2:14.]

7Nami nimewekewa kuwa mtangazaji na mtume wake, nasema kweli, sisemi uwongo, niwe mfunzi wa wamizimu, niwafundishe kumtegemea Mungu na kuyashika yaliyo ya kweli.[#Gal. 2:7-8; 2 Tim. 1:11.]

Mambo yawapasayo waume na wake.

8Nataka, waume wamwombe Mungu mahali pote wakiinua mikono itakatayo, pasipo kukasirika na kuchokoza.[#Sh. 24:4.]

9Vivyo hivyo nataka, penye kuomba wanawake wavae mavazi yafaayo wakijipamba, kama iwapasavyo wenye soni waonyekao; mapambo yao yasiwe misuko ya nywele wala dhahabu wala ushanga wala nguo zilizo za mali nyingi.[#1 Petr. 3:3-5.]

10Ila mapambo yao yawe matendo mema yawapasayo wanawake wanaoungama kuwa wake Mungu![#1 Tim. 5:10.]

11Mwanamke sharti ajifunze kutulia na kutii sana![#Ef. 5:22.]

12Lakini simpi mwanamke ruhusa kufundisha, wala kumtawala mumewe, ila akae na kutulia.[#1 Mose 3:16; 1 Kor. 14:34.]

13Kwani Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, halafu Ewa.[#1 Mose 1:27; 2:7,22.]

14Naye Adamu siye aliyedanganyika, ila mwanamke ndiye aliyedanganyika, akatangulia kukosa.[#1 Mose 3:6; 2 Kor. 11:3.]

15Lakini ataokoka kwa kuzaa watoto, hao wakiwa wenye kumtegemea Mungu na wenye kupendana na wenye kutakaswa mioyo na wenye kuonyeka.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania