The chat will start when you send the first message.
1Mimi Simoni Petero niliye mtumwa na mtume wa Yesu Kristo nawaandikia, ninyi myategemeayo pamoja na sisi yale makuu, tuliyopewa kwa wongofu wa Mungu wetu na wa mwokozi Yesu Kristo:
2Upole na utengemano uwafurikie, mkimtambua Mungu na Bwana wetu Yesu!
3*Yenye nguvu ya Kimungu yapayo watu kuwapo na kumcha Mungu tumegawiwa yote hapo, tulipomtambua yeye aliyetuitia utukufu na wema wake mwenyewe.[#1 Petr. 2:9.]
4Kisha tukagawiwa viagio vikubwa mno vya kutupa macheo kwamba: Kwa nguvu zao mtakuwa, kama Mungu alivyo, mkiyakimbia yanayowaozesha ulimwenguni, ndiyo tamaa za miili.
5Kwa hiyo jipingieni kwa nguvu zote, hivyo, mnavyomtegemea Mungu, viwapatie wema, nao wema uwapatie utambuzi;[#Gal. 5:6,22.]
6nao utambuzi uwapatie kujishinda wenyewe, nako kujishinda kuwapatie uvumilivu, nao uvumilivu uwapatie kumcha Mungu,
7nako kumcha Mungu kuwapatie kupendana kindugu, nako kupendana kindugu kuwapatie kuwapenda watu wote![#Gal. 6:10.]
8Kwani mambo hayo yakiwa kwenu, tena yakiendelea na kufurika, hamtapatwa na uvivu, wala hamtakosa mapato yaliyomo katika utambuzi wa Bwana wetu Yesu Kristo.
9Lakini asiye na mambo hayo ni kipofu, haoni, amekwisha kusahau, ya kuwa alitakaswa kwa kuondolewa makosa ya kale.[#1 Petr. 3:21; 1 Yoh. 2:9,11.]
10Kwa hiyo, ndugu, jikazeni sanasana kuushupaza wito na uteule wenu! Kwani mkifanya hivyo, hapana tena, mtakapojikwaa.
11Kwani hivyo mtapewa kuingia kifalme katika ufalme wa Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo ulio wa kale na kale.*
12Kwa hiyo sitaacha kuwakumbusha mambo hayo siku zote, ijapo mmeyajua, mkaisha kupata nguvu mkiifuata ile kweli, mliyoambiwa.
13Kwani naona, inafaa kuwakeshesha ninyi na kuwakumbusha mambo hayo siku zote, nikiwa nimo bado katika hema hili.[#2 Kor. 5:1.]
14Kwani najua: siku iko karibu, nitakapolitoka hili hema langu, kama alivyonieleza Bwana wetu Yesu Kristo.[#Yoh. 21:18-19.]
15Lakini nitawakaza, mweze kuyakumbuka mambo hayo siku zote po pote, hata nitakapokwisha kutoka humu.
16*Kwani tulipowatambulisha ninyi, uwezo wa Bwana wetu Yesu Kristo utakavyokuwa hapo, atakaporudi, hatukufuata masimulio yaliyotungwa na watu, ila tulikuwa tumeuona ukubwa wake kwa macho yetu wenyewe.
17Kwani alipopewa heshima na utukufu na Mungu Baba, sauti ilitoka kwenye utukufu mkuu, ikamjia kwamba: Huyu ndiye mwanangu mpendwa, ambaye nimependezwa naye.[#Mat. 17:5.]
18Nasi tuliisikia sauti hiyo, ilipotoka mbinguni, tulipokuwa pamoja naye juu yake huo mlima mtakatifu.
19Kwa hiyo tunalishika neno la ufumbuo kwa nguvu sana, nanyi mnafanya vizuri sana mkiliangalia, maana ni mwanga wa kumulikia mahali penye giza, mpaka kutakapokucha, mpaka nyota iwakayo mapema iwatokee mioyoni mwenu.[#Sh. 119:105; Ufu. 22:16.]
20Nalo hili litambueni kwanza, ya kuwa hakuna neno la ufumbuo lililomo Maandikoni, linaloweza kufumbuliwa kimtu tu!
21Kwani hakuna ufumbuo wo wote ulioletwa kwa hayo, mtu ayatakayo; ila watu watakatifu wa Kimungu waliyasema yaleyale, waliyopewa na Roho takatifu.*[#2 Tim. 3:16-17.]