2 Petero 3

2 Petero 3

Kristo atarudi.

1Wapendwa, barua hii ni ya pili, ninayowaandikia ninyi. Nami katika zote mbili nayakeshesha mawazo yenu yaliyo ya kweli kwa kuwakumbusha:[#2 Petr. 1:13.]

2yakumbukeni maneno yaliyosemwa kale na wafumbuaji watakatifu! Tena mlikumbuke nalo agizo la Bwana na mwokozi, mliloambiwa na mitume wenu!

3*Kwanza litambueni neno hili: siku za mwisho patatokea wafyozaji wenye mafyozi mabaya wanaoendelea na kuzifuata tamaa zao wenyewe[#1 Tim. 4:1.]

4wakisema: Kiagio cha kurudi kwake kiko wapi? Kwani tangu hapo, baba zetu walipolala, vyote viko vivyo hivyo, kama vilivyokuwa mwanzoni vilipoumbwa.[#Yes. 5:19; Ez. 12:22; Mat. 24:48.]

5Nao walio hivyo hawataki kuliona neno hili: mbingu zilikuwako toka kale, nayo nchi ilikuwa imetoka majini kwa neno la Mungu ilishikizika mlemle majini.[#1 Mose 1:2,6,9; Sh. 24:2; Mat. 24:48.]

6Kisha ule ulimwengu wa kale uliangamia, ulipofurikiwa na maji.[#2 Petr. 2:5; 1 Mose 7:21.]

7Nazo mbingu za sasa pamoja na nchi zikalimbikwa kwa neno lilelile, zikawekwa, ziteketezwe na moto siku ile, watu wasiomcha Mungu watakapohukumiwa, waangamie.[#2 Petr. 3:10.]

Siku moja kama miaka elfu.

8Lakini wapendwa, neno hili moja msilisahau:

Kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu,

nayo miaka elfu ni kama siku moja!

9Bwana hakawii kukitimiza kiagio, kama wengine wanavyowaza kwamba: Hukawia. Ila huwavumilia ninyi, kwani hataki, wengine waangamie, ila anataka, wote wageuke na kujuta.[#Hab. 2:3; 1 Tim. 2:4.]

Mwisho wa ulimwengu huu.

10Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi; ndipo, mbingu zitakapotoweka kwa shindo kuu, nayo yaliyoko tangu mwanzo yatayeyuka kwa kuchomwa na moto, hata nchi za kazi zilizomo zitateketezwa.[#2 Petr. 3:7; Mat. 24:29,35; 1 Tes. 5:2-3; Ufu. 20:11.]

11Hizi zote zikienda kuyeyuka hivyo, je? Haiwapasi kuutakasa mwenendo wenu kwa kumcha Mungu?

12Kisha mwingoje siku ya Bwana, itakapokutia, mpate kumkimbilia, mbingu zitakapoyeyuka kwa kuunguzwa na moto, yaliyoko tangu mwanzo yatakapoteketea kwa kuchomwa na moto!

13Lakini twatazamia mbingu mpya na nchi mpya zitakazokaa wongofu, kama tulivyoagiwa naye.[#Yes. 65:17; 66:22; Ufu. 21:1,27.]

Uvumilivu wa Bwana ni wokovu wetu.

14Kwa hiyo, wapendwa, mkiyatazamia hayo jikazeni, mpate kuonekana kuwa wenye utengemano pasipo kilema wala pasipo doadoa!*[#1 Kor. 1:7-8.]

15Tena uvumilivu wa Bwana wetu mwuwazie kuwa wokovu, kama naye ndugu yetu mpendwa Paulo alivyowaandikia ninyi kwa ujuzi wake, aliopewa.[#2 Petr. 3:9; Rom. 2:4; 2 Tes. 2:2.]

16Ndivyo, anavyoandika katika barua zote akiyasema mambo hayo; lakini mle baruani mwake yamo maneno mengine yaliyo magumu ya kuyajua maana. Nao wasiofundishwa vema nao wasiomtegemea Mungu vema huyapindua, kama wanavyoyapindua hata Maandiko mengine; ndivyo, wanavyojiangamiza wenyewe.

17Basi, ninyi wapendwa mlioanza kuyatambua hayo, jiangalieni, nanyi msipotezwe na upotevu wao wasioonyeka, mkaanguka na kuiacha ngome yenu wenyewe![#Mar. 13:5,9,33.]

18Ila endeleeni kukuwa mkigawiwa mema, tena mkimtambua Bwana na mwokozi wetu Yesu Kristo! Yeye atukuzwe sasa mpaka siku isiyo na mwisho! Amin.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania