The chat will start when you send the first message.
1Ikatukia, ya kama kulikuwa na mtu asiyefaa, jina lake Seba, mwana wa Bikri, mtu wa Benyamini. Akapiga baragumu kwamba: Sisi hatuna fungu kwake Dawidi, wala hatuna lililo letu kwake mwana wa Isai. Ninyi Waisiraeli, kila mtu na aende hemani kwake.
2Ndipo, watu wote wa Waisiraeli walipopanda kwenda kwao wakiacha kumfuata Dawidi, ila wakamfuata Seba, mwana wa Bikri. Lakini Wayuda wakaandamana na mfalme wao toka mto wa Yordani hata mji wa Yerusalemu.
3Dawidi alipoingia nyumbani mwake huko Yerusalemu, mfalme akawachukua wale masuria kumi, aliowaweka kuiangalia nyumba, akawatia katika nyumba ya kulindwa, akawatunza humo, lakini hakuingia kwao. Basi, wakawa wafungwa mpaka siku ya kufa kwao, siku zao zikawa kama za wajane.[#2 Sam. 16:21.]
4Mfalme akamwambia Amasa: Waite watu wa Yuda, waje kwangu katika siku hizi tatu, kisha nawe uje kusimama hapa!
5Amasa akaenda kuwaita Wayuda; lakini alipokawia na kuupita muda, aliowekewa,
6Dawidi akamwambia Abisai: Sasa Seba, mwana wa Bikri, atatupatia mabaya kuliko Abisalomu; wewe wachukue watumishi wa bwana wako, umfukuze, asijipatie miji yenye maboma ya kuponea humo, macho yetu yasimwone tena.
7Ndipo, watu wa Yoabu walipotoka, wakamfuata nao Wakreti na Wapuleti na mafundi wote wa vita. Wakatoka Yerusalemu kwenda kumfukuza Seba, mwana wa Bikri.
8Wao walipofika kwenye lile jiwe kubwa lililoko Gibeoni, Amasa akawatokea usoni. Naye Yoabu alikuwa amejifunga nguo zake za vitani, alizozivaa kila mara, juu yao alikuwa amejifunga upanga uliofungwa kiunoni, nao ulikuwa ndani ya ala yake; lakini alipokwenda huko na huko, ukaanguka.
9Yoabu akamwamkia Amasa kwamba: Hujambo, ndugu yangu? Kisha Yoabu akamshika Amasa udevu kwa mkono wake wa kulia, anoneane naye.[#Sh. 28:3.]
10Amasa asipouangalia upanga uliomo mkononi mwa Yoabu, akamchoma nao tumboni, matumbo yake yamwagike chini, hakumchoma mara ya pili, akafa tu. Kisha Yoabu na ndugu yake Abisai wakaenda kumfukuza Seba, mwana wa Bikri.[#1 Fal. 2:5.]
11Naye mmoja wao vijana wa Yoabu akaja kusimama kwake Amasa na kusema: Apendezwaye na Yoabu, naye aliye upande wa Dawidi na amfuate Yoabu!
12Lakini Amasa alikuwa anagaagaa katika damu yake katikati ya barabara; yule mtu alipoona, ya kuwa watu wote wanasimama hapo barabarani, akamwondoa Amasa hapo barabarani na kumtupa porini, kisha akamfunika kwa nguo, kwani aliona, ya kuwa kila aliyefika hapo alipo husimama.
13Alipokwisha kumwondoa hapo barabarani, watu wote wakapapita tu, waende kumfuata Yoabu, wamfukuze Seba, mwana wa Bikri.
14Huyo akapita kwa mashina yote ya Waisiraeli mpaka Abeli na Beti-Maka nao Haberimu wote; ndipo, watu walipokusanyika, wakaja kufuatana naye.
15Lakini wale walipokuja wakamsonga na kumzinga kule Abeli kwa Beti-Maka, wakiujengea mji huo boma la mchanga la kuuzunguka, nalo kikasimama papo hapo, mfereji wa boma la mji ulipokuwa. Nao watu wote waliokuwa na Yoabu wakachimba chini ya ukuta wa boma lao, wauangushe.
16Ndipo, mwanamke mwenye werevu wa kweli alipoita toka mjini kwamba: Sikieni! Sikieni! Mwambieni Yoabu, aje hapa karibu, niseme naye!
17Yoabu alipofika karibu yake, yule mwanamke akamwuliza: Wewe ndiwe Yoabu? Aliposema: Ndimi, akamwambia: Yasikilize maneno ya kijakazi wako! Akasema: Mimi nitayasikia.
18Akasema kwamba: Kale watu husema kwamba: Waulizeni watu wa Abeli! Ndivyo, walivyoyamaliza mashauri.
19Sisi tu Waisiraeli watulivu na welekevu, nawe unataka kuwaua watu wa humu mjini waliozaa makundi kwao Waisiraeli. Ni kwa nini, ukitaka kuwameza walio fungu lake Bwana?
20Yoabu akajibu kwamba: Hili linikalie mbali kabisa kwamba: Ninataka kumeza na kuangamiza!
21Hivi haviko kabisa, ila yuko mtoro wa milima ya Efuraimu, jina lake Seba, mwana wa Bikri; huyu ameuinua mkono wake, amwue mfalme Dawidi. Mtoeni huyu peke yake tu! Ndipo, nitakapoondoka penye mji huu. Naye yule mwanamke akamwambia Yoabu: Utakiona kichwa chake, kikitupwa kwako toka ukutani juu.
22Kisha huyu mwanamke akaja kuonana na watu wote na kuwatolea huo werevu wake wa kweli. Ndipo, walipokikata kichwa chake Seba, mwana wa Bikri, wakakitupia huko kwa Yoabu. Kisha akapiga baragumu, nao watu wakatawanyika wakiondoka kwenye ule mji, wakaenda kila mtu hemani kwake, naye Yoabu akarudi Yerusalemu kwa mfalme.
23Yoabu alikuwa mkuu wa vikosi vyote vya Waisiraeli, naye Benaya, mwana wa Yoyada, alikuwa mkuu wa Wakreti na wa Wapuleti.[#2 Sam. 8:16-18.]
24Naye Adoramu alikuwa mkuu wa kazi za nguvu, naye Yosafati, mwana wa Ahiludi, alikuwa mwandishi wa mambo yaliyopasa kukumbukwa.[#1 Fal. 4:6.]
25Naye Sewa alikuwa mwandishi, nao Sadoki na Abiatari walikuwa watambikaji.
26Naye Ira wa Yairi alikuwa mtambikaji wa Dawidi.