2 Watesalonike 2

2 Watesalonike 2

Yatakayotangulia kurudi kwake Yesu.

1Ndugu, kwa ajili ya kurudi kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kwa ajili ya kwamba: Sisi tutakusanyika kwake, tunawaomba sana ninyi,[#1 Tes. 4:13-17.]

2msitetemeshwe upesi mkipotelewa na njia, wala msihangaike mkisikia mambo ya kirohoroho au ya masimulio au ya barua, ya kuwa neno limetoka kwetu la kwamba: Siku ya Bwana imekwisha fika!

3Mtu asiwadanganye na kuwaongoza katika njia, iwayo yote! Kwani sharti kwanza matanguo yaje, naye yule mtu wa upotovu sharti ajulishwe kuwa mwana wa mwangamizo,[#1 Tim. 4:1; 1 Yoh. 2:18; 4:3.]

4ni mbishi, ni mwenye kujikweza kuwa mkuu kuliko yote yaitwayo Mungu au tambiko, mpaka akija kukaa katika Jumba la Mungu na kutangaza: Mungu ni mimi![#Dan. 11:36; Mat. 24:15.]

5Hamkumbuki, ya kuwa niliwaambia hayo nilipokuwa kwenu?

6Nacho kinachomzuia sasa mwakijua; lakini siku yake itakapotimia, atatokea waziwazi.

7Kwani ule upotovu uliokuwa umefichwa umekwisha anza kutenda nguvu, kisaacho ni hiki: yule mwenye kuuzuia mpaka sasa sharti aondolewe, atoke hapo kati.[#Tume. 20:29.]

8Kisha ndipo, yule mpotovu atakapofunuliwa. Naye Bwana Yesu atamwua akimpuzia tu kwa kinywa chake, atenguke kwa mwangaza wa kuja kwake.[#Yes. 11:4; Ufu. 19:15,20.]

9Lakini yule mpotovu uwezo wa kuja kwake ni ule wa Satani, ukamfanyisha ya nguvu yo yote na vielekezo na vioja vya uwongo,[#Mat. 24:24; Ufu. 13:11-13.]

10nao wenye kuangamia huwaponza kwa udanganyi wo wote, kwa sababu waliyakataa yaliyo ya kweli, wasiyapende, wapate kuokolewa.[#2 Kor. 2:15; 4:3.]

11Kwa sababu hiyo Mungu anawaletea mapotevu yenye nguvu, wayategemee yaliyo ya uwongo,[#Rom. 1:28; 2 Tim. 4:4.]

12wapate kuhukumiwa wote wasioyategemea yaliyo ya kweli, ila walipendezwa nayo yaliyo ya upotovu.

13Ndugu, sisi imetupasa kumshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu mliopendwa na Bwana, maana Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo, mpate wokovu mkitakaswa roho, mkayategemea yaliyo ya kweli.[#2 Tes. 1:3; Ef. 1:4.]

14Haya ndiyo, aliyowaitia, tulipowatangazia Utume mwema, mpate kuuchuma utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo.

15Basi, ndugu, sasa simameni na kuyashika mafundisho, mliyofundishwa nasi, ikiwa mliambiwa au mliandikiwa![#2 Tes. 3:6.]

16Lakini yeye, Bwana wetu Yesu Kristo, na Mungu Baba yetu aliyetupenda sisi, akatugawia kwa upole wake matulizo yaliyo ya kale na kale na kingojeo chema, awatulize mioyo yenu na kuitia nguvu, myafuate matendo na mambo yote yaliyo mema!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania