Wakolose 4

Wakolose 4

1Ninyi mabwana, wapeni watumwa wenu yawapasayo, mwalinganishe! Jueni, nanyi mko na Bwana mbinguni![#3 Mose 25:43,53.]

Paulo anawahimiza, wamwombee.

2Fulizeni kumwomba Mungu! Kesheni kuomba na kushukuru![#1 Tes. 5:17.]

3Na sisi vilevile tuombeeni, Mungu atufungulie mlango wa kuingizamo Neno lake, tupate kulisema fumbo la Kristo, ni lilelile, nililofungiwa,[#Kol. 1:26; Rom. 15:30; Ef. 6:19; 2 Tes. 3:1; 1 Kor. 16:9.]

4nipate kulifumbua, kama inavonipasa kulisema!

5Walioko nje waendeeni kwa werevu wa kweli! Siku mlizopewa, mzitumie vema![#Ef. 5:15-16; 1 Tes. 4:12.]

6Maneno yenu yawe po pote ya kupendeza yakiwa matamu kama yenye chumvi, mpate kujua yanayofaa ya kumjibu mtu awaye yote![#Ef. 4:29; Mar. 9:50.]

7Mambo yangu yote yalivyo, atawatambulisha Tikiko aliye ndugu mpendwa na mtumishi mwelekevu na mtumwa mwenzangu, kwa kuwa wake Bwana.

8Nami nimemtuma kwenu kwa ajili ya neno lili hili, mpate kuyatambua mambo yetu, naye ataituliza mioyo yenu.[#Ef. 6:22.]

9Anaye Onesimo, ni ndugu mwelekevu, nimpendaye, ni mtu wa kwenu. Watawatambulisha, yote ya huku yalivyo.[#File. 10.]

Salamu.

10Aristarko, mfungwa mwenzangu, na Marko, mpwae Barnaba, wanawasalimu ninyi; kwa ajili yake yeye mmepata maagizo; atakapokuja kwenu, mpokeeni![#Tume. 12:12,25; 19:29; 27:2.]

11Naye Yesu anayeitwa Yusto anawasalimu. Kwao Wakristo wa Kiyuda ni hao watatu tu walio wenzangu wa kazi ya kuujenga ufalme wa Mungu, ndio walionituliza moyo.

12Epafura aliye wa kwenu anawasalimu; ni mtumwa wa Kristo Yesu, naye huwagombea kila siku na kuwaombea, mpate kusimama wenye kuyatimiza na kuyatambua yote, Mungu ayatakayo.[#Kol. 1:7.]

13Kwani namshuhudia kwamba: Hujisumbua sana kwa ajili yenu na kwa ajili yao walioko Laodikia na Hierapoli.

14Luka aliye mganga mpendwa na Dema wanawasalimu.[#2 Tim. 4:10-11; File. 24.]

15Wasalimieni ndugu walioko Laodikia, naye Nimfa nao wateule waliomo nyumbani mwake!

16Barua hii, ikiisha kusomwa kwenu, angalieni, isomwe hata kwao wateule wa Laodikia, nanyi mwisome ile ya Laodikia!

17Tena mwambieni Arkipo: Uangalie utumishi wako, ulioupokea wa kumtumikia Bwana, uutimize vema![#File. 2.]

18Salamu hii naiandika kwa mkono wangu mimi Paulo. Ikumbukeni hii minyororo yangu! Upole uwakalie! Amin.[#1 Kor. 16:21; 2 Tes. 3:17.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania