The chat will start when you send the first message.
1Yako mabaya, niliyoyaona chini ya mbingu, nayo huwalemea watu sana.
2Mungu akimgawia mtu mali na mema ya dunia hii na macheo, asijinyime lo lote, moyo wake ulitunukialo, lakini Mungu asipompa uwezo wa kuyala, ila mgeni akiyala, basi, yanamwia ya bure, tena humwuguza vibaya.[#Mbiu. 2:18.]
3Mtu akizaa watoto mia, miaka ya maisha yake ikawa mingi, siku za miaka yake zikihesabiwa ziwe nyingi kweli, lakini roho yake isipoyashiba hayo mema yake, naye asipate hata kaburi, basi, nasema: Mtoto aliyekufa katika kuzaliwa alipata mema kuliko yeye.
4Kwani huyo mtoto huja kama si kitu, huenda gizani, nalo jina lake limo gizani.
5Jua tu hakuliona, wala halijui; lakini hutulia kuliko yule.
6Kama mtu angepata kuwapo miaka elfu mbili, asione mema, huyu naye haendi mahali pale pamoja, wote wanapokwenda?
7Masumbuko yote ya mtu ni ya kukijaza kinywa chake, lakini hivyo roho yake haishibi.
8Kwani yako mapato gani, mwerevu wa kweli anayoyapata, mjinga asiyoyapata? Au yako mapato gani, mnyonge anayoyapata akijua mwenendo ufaao machoni pa watu wanaoishi?
9Kuyatazama yaliyoko machoni ni kwema kuliko kwenda na kuzifuata tamaa; hayo nayo ni ya bure na kuukimbilia upepo.
10Yaliyoko yamekwisha kuitwa jina tangu kale, nayo yatakayompata mtu yamekwisha kujulikana kale; hakuna mtu anayeweza kubishana na mwenziwe amshindaye nguvu.
11Kwani yako mambo mengi yaletayo mengi yaliyo ya bure; hayo mtu yanamfalia nini?
12Kwani yuko nani ayajuaye yamfaliayo mtu huku nchini siku hizi za kuwapo zinazohesabika, zilizo za bure tu? maana huzila kama kivuli. Yuko nani awezaye kumwelezea mtu yatakayokuwako nyuma yake chini ya jua?[#1 Mambo 29:15; Sh. 90:5.]