Mpiga mbiu 8

Mpiga mbiu 8

Wanaotii ukuu nao wamchao Mungu hupata mema.

1Aliye kama mwerevu wa kweli ni nani? Tena yuko nani ajuaye maana ya mambo? Werevu wa kweli wa mtu huuangaza uso wake, ushupavu wa uso wake ugeuzwe.

2Mimi husema: Kiangalie kinywa cha mfalme, kwa kuwa uliapa na kumtaja Mungu!

3Usitoke upesi usoni pake, wala usishikamane na shauri baya! Kwani yeye hufanya yote yampendezayo.

4Kwa kuwa neno la mfalme lina nguvu, yuko nani awezaye kumwambia: Unafanya nini?

5Aishikaye amri yake hataona baya lo lote; nao moyo wa mwerevu wa kweli hujua, siku za wakati wa kukatia shauri zitakapotimia.

6Kwani kila jambo liko na siku zake za kukatiwa shauri. Kwani huu ndio ubaya unaowalemea watu sana:[#Mbiu. 3:1.]

7kwa kuwa hayuko ayajuaye yatakayokuwako, yuko nani atakayewaeleza, jinsi yatakavyokuwa?[#Mbiu. 10:14.]

8Hakuna mtu autawalaye upepo, aweze kuukomesha upepo, wala hakuna aitawalaye siku ya kufa, wala hakuna apewaye ruhusa siku ya mapigano; vivyo hivyo kumwacha Mungu hakuwaponyi wao waliomwacha.

9Hayo yote niliyatazama, nikayaweka moyoni mwangu, nikaziangalia kazi zote zinazofanywa chini ya jua, mtu anapomtawala mtu mwenziwe, apate kumfanyizia mabaya.

10Nikaona, wasiomcha Mungu wakizikwa, wafike pao; nao waliofanya yaliyopasa hawakuwa na budi kuondoka mahali patakatifu, wakasahauliwa mle mjini. Hayo nayo ni ya bure.

11Kwa kuwa patilizo la tendo baya halitimizwi upesi, kwa hiyo mioyo ya wana wa Adamu huzidi kufanya mabaya;[#Iy. 35:15.]

12tena ni kwa hiyo, mwenye kukosa na kufanya mabaya akipata kukaa siku nyingi. Lakini hayo nayo mimi ninayajua, ya kuwa wamchao Mungu wataona mema, kwa kuwa huucha uso wake.[#Sh. 73:17-26.]

13Lakini asiyemcha Mungu hataona mema, wala hatakaa siku nyingi, ila huwa kama kivuli tu, kwa kuwa hauchi uso wake.

14Yako yaliyo ya bure yanayofanyika huku nchini, ni haya: wako waongofu wanaopatwa na mambo yapasayo matendo yao wasiomcha Mungu; tena wako wasiomcha Mungu wanaopatwa na mambo yapasayo matendo yao waongofu. Nasema: Hayo nayo ni ya bure.[#Mbiu. 7:15.]

15Kwa hiyo nikaisifu furaha, kwa kuwa chini ya jua mtu hawezi kuona yaliyo mema kuliko kula na kunywa na kufurahi; haya na yafuatane naye kwa hivyo, anavyosumbuka siku zake za kuwapo chini ya jua, Mungu alizompa.[#Mbiu. 2:24.]

16Mara kwa mara nikauelekeza moyo wangu, uujue werevu wa kweli kwa kuzitazama kazi za utumishi zinazofanywa huku nchini, kwani wako wasioona usingizi machoni pao mchana wala usiku.

17Ndipo, nilipozitazama kazi zote za Mungu, nikaona, ya kuwa mtu hawezi kuzitambua maana hizo kazi zinazofanywa chini ya jua; ijapo mtu ajisumbue sana kwa kuitafuta hiyo maana, haioni. Hata mwerevu wa kweli akijiwazia kwamba ameijua, hawezi kuitambua.[#Mbiu. 3:11.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania