2 Mose 31

2 Mose 31

Kuweka mafundi wawili.

(1-6: 2 Mose 35:30-35; 7-11: 2 Mose 35:11-19.)

1Bwana akamwambia Mose kwamba:

2Tazama, nimemwita kwa jina lake Besaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa shina la Yuda.

3Nikamjaza roho yangu ya Kimungu na kumgawia werevu wa kweli na utambuzi na ujuzi wa kutengeneza kazi yo yote,[#1 Fal. 7:14.]

4ajue kuvumbua kazi nzuri za ufundi wa kufua dhahabu na fedha na shaba;

5naye ni fundi wa kukatakata vito na kuvizungushia vikingo na fundi wa kuchora miti na fundi wa kufanya kazi yo yote.

6Tena tazama, mimi nimempa Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa shina la Dani, kuwa mwenzake. Namo mioyoni mwao wote walio werevu wa kweli nimetia werevu wa kweli, wayafanye yote, niliyokuagiza:

7Hema la Mkutano na Sanduku la Ushahidi na Kiti cha Upozi kilichoko juu yake na vyombo vyote vya hilo Hema,

8na meza na vyombo vyake, na kinara cha dhahabu tupu na vyombo vyake vyote na meza ya kuvukizia,

9na meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko na vyombo vyake vyote na birika na wekeo lake,

10na nguo nzuri za mapazia na mavazi matakatifu ya mtambikaji Haroni na mavazi ya wanawe, wapate kuwa watambikaji,

11na mafuta ya kupata na mavukizo yanukayo vizuri ya kuvukizia Patakatifu. Yote pia, niliyokuagiza, watayafanyiza vivyo hivyo.

Agizo la siku ya mapumziko.

(12-17: 2 Mose 35:1-3.)

12Bwana akamwambia Mose kwamba:

13Wewe sema na wana wa Isiraeli na kuwaambia: Ziangalieni siku zangu za mapumziko, ziwe kielekezo cha Agano, nililoliagana nanyi, wao wa vizazi vyenu vijavyo wajue, ya kuwa mimi Bwana ndimi mwenye kuwatakasa ninyi.[#2 Mose 20:8.]

14Kwa hiyo iangalieni siku ya mapumziko, ipate kuwa takatifu kwenu. Atakayelivunja hili agizo la kuitakasa hana budi kufa, kwani kila atakayefanya kazi siku hiyo, roho yake sharti ing'olewe kwao walio wa ukoo wake.[#4 Mose 15:32-35.]

15Kazi na zifanywe siku sita, lakini siku ya saba ni siku ya sabato, ndio ya mapumziko kabisa, kwani ni siku takatifu ya Bwana. Kila atakayefanya kazi siku hiyo ya mapumziko hana budi kufa.

16Kwa hiyo wana wa Isiraeli sharti waiangalie siku ya mapumziko, huku kuiangalia siku ya mapumziko wakufanye kuwa agano la kale na kale kwa vizazi vyao.

17Hiki ni kielekezo cha kale na kale cha Agano, nililoliagana na wana wa Isiraeli, kwani Bwana alifanya kazi siku sita alipoziumba mbingu na nchi, lakini siku ya saba alipumzika na kutulia.[#1 Mose 2:2.]

18Bwana alipokwisha kusema na Mose akampa kule mlimani kwa Sinai mbao mbili za Ushahidi, nazo zilikuwa za mawe zenye machoro, Mungu aliyoyachora kwa kidole chake.[#2 Mose 32:15-16; 34:28; 5 Mose 4:13; 5:22; 9:10; 10:4.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania