Ezekieli 11

Ezekieli 11

Mapatilizo ya wakuu wa Yuda.

1Roho ikanichukua, ikanipeleka kwenye lango la Nyumba ya Bwana la mashariki lielekealo maawioni kwa jua. Hapo pa kulilingilia lile lango nikapaona waume 25; katikati yao nikamwona Yazania, mwana wa Azuri, na Pelatia, mwana wa Benaya, walio wakuu wa ukoo huu.[#Ez. 3:12.]

2Akaniambia: Mwana wa mtu, hawa waume ndio wanaowaza yaliyomaovu na kuwapigia watu mashauri mabaya humu mjini.

3Ndio wanaosema: Kujenga nyumba siko karibu; mji huu ndio nyungu, nasi ndio nyama.

4Kwa hiyo wafumbulie yatakayokuwa! Wafumbulie, mwana wa mtu!

5Ndipo, Roho ya Bwana iliponiangukia, ikaniambia: Sema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Ndivyo, mlivyosema, mlio wa mlango wa Isiraeli, nayo mawazo yainukayo rohoni mwenu mimi nimeyajua.

6Wenzenu, mliowaua humu mjini, ni wengi, mkajaza barabara za mji mizoga yao.

7Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wenzenu, mliowaua na kuwalaza humu mjini, hao ndio nyama, nao mji huu ndio nyungu, lakini ninyi watawatoa humu mjini.

8Panga mnaziogopa, lakini nitawaletea panga; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.

9Kisha nitawatoa humu mjini, niwatie mikononi mwa wageni; ndipo, nitakapowakatia mashauri.

10Mtauawa kwa panga, kwenye mipaka ya Isiraeli ndiko, nitakakowapatiliza; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.[#2 Fal. 25:20-21.]

11Mji huu hautakuwa nyungu yenu, mkiwa nyama humu mjini, ila kwenye mipaka ya Isiraeli ndiko, nitakakowapatiliza.

12Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana; hamkuyafuata maongozi yangu, wala hamkuyafanya mashauri yangu, ila mmefanya, kama wamizimu wawazungukao wanavyopiga mashauri.

13Ikawa, nilipowafumbulia haya, ndipo, Pelatia, mwana wa Benaya, alipokufa; nikaanguka kifudifudi na kulia kwa sauti kuu nikisema: E Bwana Mungu, wewe utalimaliza sao lake Isiraeli![#Ez. 9:8.]

Matulizo ya roho zao waliotekwa.

14Neno la Bwana likanijia la kwamba:

15Mwana wa mtu, ndugu zako, hawa ndugu zako, ambao mlitekwa pamoja nao, hata mlango wote wa Isiraeli, hawa wote ndio, wenyeji wa Yerusalemu waliowaambia: Nendeni mbali mkitoka kwake Bwana! Sisi tumepewa nchi hii, iwe yetu!

16Kwa hiyo sema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema kwamba: Kweli nimewapeleka mbali kwenye wamizimu na kuwatawanya katika hizo nchi siku hizi zilizo chache, nikawa mwenyewe patakatifu pao katika nchi hizo, walikopelewa.[#Ez. 6:8-10; Yer. 24:5-6.]

17Kwa hiyo sema: Hivi ndivyo Bwana Mungu anavyosema: Nitawakusanya ninyi na kuwatoa katika hayo makabila, kweli nitawaunganisha ninyi na kuwatoa katika nchi hizo, nilikowatawanya, niwape ninyi nchi ya Isiraeli.[#Yer. 29:14.]

18Napo watakapoiingia watayaondoa huko matapisho yake yote na machukizo yake yote.

19Nami nitawapa kuwa moyo mmoja, tena nitatia roho moja mioyoni mwao; namo miilini mwao nitaitoa mioyo iliyo migumu kama mawe nikiwatia mioyo inayolegea kama nyama.[#Ez. 36:26; Yer. 24:7.]

20Ndivyo, watakavyoyafuata maongozi yangu na kuyashika mashauri yangu, wayafanye. Watakuwa ukoo wangu, nami nitakuwa Mungu wao.[#Yer. 31:33.]

21Lakini wenye mioyo iyaelekeayo matapisho yao na machukizo yao, mioyo yao ikayafuata, basi, nitawapatilizia njia zao vichwani pao.

22Ndipo, Makerubi walipoyakunjua mabawa yao, nayo magurudumu yakawa kando yao, nao utukufu wa Mungu wa Isiraeli ukawa juu yao.[#Ez. 1:4-28.]

23Kisha utukufu wa Bwana ukapanda ukiondoka mle mjini katikati, ukasimama juu ya mlima ulioko karibu ya mji upande wa maawioni kwa jua.

24Roho ikanichukua, ikanipeleka katika nchi ya Wakasidi kwenye mateka kwa nguvu ya hayo maono ya Roho ya Mungu. Kisha hayo maono, niliyoyaona, yakaniondokea.[#Ez. 3:12.]

25Nikawaambia waliotekwa mambo yote ya Bwana, aliyonionyesha.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania