Ezekieli 13

Ezekieli 13

Wafumbuaji wa uwongo wanaumbuliwa.

1Neno la Bwana likanijia la kwamba:

2Mwana wa mtu wafumbuaji wa Isiraeli wanaowafumbulia yatakayokuwa wafumbulie wewe yatakayowajia. Waambie hao wafumbuaji wanaosema kwa hayo yaliyomo mioyoni mwao: Lisikieni neno la Bwana!

3Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wafumbuaji hawa wajinga watapatwa na mambo! Maana huzifuata roho zao, husema mambo, wasiyoyaona![#Yer. 23:21,31.]

4Kama mbweha walivyo kwenye mabomoko, ndivyo, wafumbuaji wako, Isiraeli, walivyo.

5Hamkukwea hapo palipoatuka nyufa, wala hamkuuzungushia mlango wa Isiraeli boma, wapate kusimama kwenye mapigano, siku ya Bwana itakapokutia.[#Ez. 22:30.]

6Wameona maono yasiyokuwako, nayo maaguo yao ni ya uwongo, wakisema: Ndivyo, asemavyo Bwana, lakini Bwana hakuwatuma, nao wakangojea, alitimize neno lao.[#Ez. 22:28; Yer. 23:32.]

7Je? Hamkuona maono yasiyokuwako? Hamkusema maaguo ya uwongo, mliposema: Ndivyo, asemavyo Bwana, nami nalikuwa sikuyasema?

8Kwa hiyo Bwana Mungu anasema: Kwa kuwa mmesema yasiyokuwako, mkaona mambo ya uwongo, kwa hiyo mtaniona, nikiwajia ninyi; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.

9Itakuwa, mkono wangu uwajie hao wafumbuaji walioona yasiyokuwako na kuagua uwongo; hawatakula bia nao walio ukoo wangu, wala hawataandikwa katika kitabu cha mlango wa Isiraeli, wala hawataiingia nchi ya Isiraeli; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu.[#Ez. 14:9.]

10Wanawapoteza mara kwa mara walio ukoo wangu wakisema: kumetengemana, lakini utengemano hauko; tena watu wakijenga boma wenyewe, hao utawaona, wakilipaka chokaa.[#Yer. 6:14.]

11Kwa sababu hii waambie hao mafundi wa kupaka chokaa: Litaanguka! Itakunya mvua ifurikayo maji, nami nitanyesha mvua ya mawe, yaliangukie, hata upepo wa kimbunga utalibomoa;

12ndipo, mtakapoona, hilo boma likianguka, nanyi mtaulizwa: Chokaa, mliyolipaka, iko wapi?

13Kweli hivyo ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwani machafuko yangu yenye moto nitaleta upepo wa kimbunga wa kulibomoa, hata mvua ifurikayo maji itakunya kwa makali yangu, nayo mvua ya mawe ya kuangamiza itaanguka kwa yale machafuko yangu yenye moto.

14Ndipo, nitakapolibomoa boma, mlilolipaka chokaa, nitaliangusha chini, msingi wake utokee; napo, litakapoanguka, mtaangamia huko katikati. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.

15Hayo machafuko yangu yenye moto nitayamaliza huko katika hilo boma nako kwao waliolipaka chokaa, kisha nitawaambia: Hilo boma haliko tena, wala hao waliolipaka chokaa hawako tena.

16Nao ndio waliokuwa wafumbuaji wa Isiraeli walioufumbulia Yerusalemu yatakayokuwa na kuupatia maono yenye utengemano, utengemano usipokuwa kabisa; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#Ez. 13:10.]

17Wewe mwana wa mtu, uso wako uuelekezee wanawake wa ukoo wako wanaoagua kwa hayo yaliyomo mioyoni mwao, uwafumbulie yatakayowajia!

18Sema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Watapatwa na mambo hao wanawake wanaoshona vitambaa vya uganga katika maungo yote ya mikono, wanaotengeneza hata miharuma ilinganayo na vichwa vya kila umbo, kusudi wapate kunasa roho za watu! Je? Mwataka kuzinasa roho zao walio ukoo wangu, mziokoe roho zenu wenyewe?

19Mkanitia uchafu mbele yao walio wa ukoo wangu mkiweza kupata makufi mawili tu ya mawele au vipande vichache vya mkate; ndivyo, mnavyoziua roho za watu wasioipaswa na kufa, nazo roho za wengine wasiopaswa na kupona mnaziponya, mkiwaogopea walio ukoo wangu, wanaopenda kusikia maneno ya uwongo.[#Fano. 17:15; Yes. 5:23.]

20Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mtaniona, nikivijia vitambaa vyenu vya uganga, mnavyovitumia vya kunasia roho za watu, kama ni ndege, nitavirarua mikononi mwenu, nizinasue zile roho za watu kwenda zao, ni zile roho, mlizozinasa, kama ni ndege.

21Nayo miharuma yenu nitairarua, niwaokoe mikononi mwenu walio ukoo wangu, wasiwe mateka tena mikononi mwenu. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.

22Kwa madanganyo yenu mmeiumiza mioyo yao waongofu, nisiowaumiza mimi, mkaishupaza mikono yao wasionicha, wasiweze kurudi katika njia zao mbaya, wapate uzima.[#Yer. 23:14.]

23Kwa sababu hii hamtaona tena maono yasiyokuwako, wala hamtaagua tena maaguo, kwani walio ukoo wangu nitawaponya mikononi mwenu; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania