The chat will start when you send the first message.
1Wakaja kwangu waume wazee wa Kiisiraeli, wakakaa mbele yangu.[#Ez. 20:1.]
2Ndipo, neno la Bwana liliponijia la kwamba:[#Ez. 20:3.]
3Mwana wa mtu, watu hawa wameyatia magogo yao ya kutambikia mioyoni mwao, wakayaweka mbele ya nyuso zao kuwa kwazo la kuwakosesha; sasa je? Niwaitikie nikitafutwa nao?
4Kwa hiyo sema nao na kuwaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mtu ye yote wa mlango wa Isiraeli atakayeyatia magogo yake ya kutambikia moyoni mwake na kuyaweka mbele ya uso wake kuwa kwazo la kumkosesha, kisha akija kwa mfumbuaji, basi, mimi Bwana nitamjibu yayapasayo magogo yake mengi ya kutambikia,
5kusudi niipate mioyo yao walio mlango wa Isiraeli waliotawanyika wote na kuniacha kwa ajili ya magogo yao ya kutambikia.
6Kwa hiyo waambie walio mlango wa Isiraeli: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Rudini! Jigeuzeni na kuyaacha magogo yenu ya kutambikia! Zigeuzeni nyuso zenu na kuyaacha machukizo yenu yote![#Yes. 31:6.]
7Kwani mtu ye yote wa mlango wa Isiraeli, nao walio wageni wakikaa kwa Waisiraeli, wote pia wametawanyika wakiacha kunifuata; hao wakiyatia magogo yao ya kutambikia mioyoni mwao na kuyaweka mbele ya nyuso zao kuwa kwazo la kuwakosesha, kisha wakija kwa mfumbuaji, aniulize kwa ajili yao, basi, mimi Bwana nitawajibu mwenyewe.
8Mtu aliye hivyo nitamkazia macho yangu, nitamwangamiza vibaya, awe kielekezo na fumbofumbo, nikimtowesha kwao walio ukoo wangu; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.[#Ez. 5:15.]
9Kama yuko mfumbuaji aliyeshindwa naye, akamwambia mtu aliye hivyo neno lo lote, mimi Bwana nimemshinda huyo mfumbuaji, tena nitamkunjulia mkono wangu, nimtoweshe kwao walio ukoo wangu wa Isiraeli.[#1 Fal. 22:20-23.]
10Hivyo watatwikwa manza zao walizozikora: manza zake aliyeuliza zitakuwa sawasawa na manza zake mfumbuaji yule.
11Kusudi walio mlango wangu wa Isiraeli wasipotee tena wakiacha kunifuata na kujipatia uchafu tena kwa mapotovu yao yote, wapate kuwa ukoo wangu, nami nipate kuwa Mungu wao; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#Ez. 11:20.]
12Neno la Bwana likanijia la kwamba:[#Ez. 5:16.]
13Mwana wa mtu, nchi ikinikosea na kuvunja maagano, nitaikunjulia mkono wangu, nilivunje shikizo lao la chakula na kuipelekea njaa, nimalize huko watu na nyama.
14Lakini kama wangekuwako katika ile nchi watu hawa watatu: Noa na Danieli na Iyobu, hawa wangejiponya kwa wongofu wao; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#Yer. 15:1.]
15Kama ningeleta nyama wabaya, watembee katika ile nchi na kuwamaliza watu walioko, iwe peke yake, asipite mtu kwa ajili ya wale nyama,[#Ez. 14:21.]
16basi, kama wangekuwako katika ile nchi hao watu watatu: hivyo, nilivyo Mwenye uzima, ndivyo, Bwana Mungu asemavyo, nao hawataponya wana wa kiume wala wa kike, ila wangepona wao wenyewe tu, hiyo nchi iwe peke yake.
17Au kama ningeiletea ile nchi panga nikisema: Panga na zitembee katika nchi hii, nitoweshe kwake watu na nyama,
18kama wangekuwako katika ile nchi hao watu watatu: hivyo, nilivyo Mwenye uzima, ndivyo, Bwana Mungu asemavyo, hawataponya wana wa kiume waka wa kike, ila wangepona wao wenyewe tu.
19Au kama ningeipelekea ile nchi magonjwa mabaya, akiimwagia makali yangu yenye moto pamoja na kumwaga damu, nitoweshe kwake watu na nyama,
20kama wangekuwako katika ile nchi Noa na Danieli na Iyobu: hivyo, nilivyo Mwenye uzima, ndivyo, asemavyo Bwna Mungu, hawataponya mwana wa kiume wala wa kike, ila wengepona wao wenyewe tu kwa wongofu wao.
21Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Ingawa niupelekee Yerusalemu haya mapatilizo yangu manne yaliyo mabaya: panga na njaa na nyama wabaya na magonjwa mabaya, nitoweshe mwake watu na nyama,[#3 Mose 6:16-25; Yer. 15:3.]
22mtaona, wakisazwa mwake waliopona watakaohamishwa wa kiume na wa kike, hao mtawaona wakitokea kwenu, mzitazama njia zao na matendo yao; ndipo, mtakapoituliza mioyo yenu kwa ajili ya mabaya, niliyouletea Yerusalemu, na kwa ajili yao yote, niliyouletea.
23Wataituliza mioyo yenu, mtakapozitazama njia zao na matendo yao; ndipo, mtakapojua, ya kuwa sikuyafanya bure tu hayo yote, niliyoufanyia; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.