Ezekieli 17

Ezekieli 17

Ufumbuo wa mabaya yatakayompata mfalme.

1Neno la Bwana likanijia la kwamba:

2Mwana wa mtu, utegee mlango wa Isiraeli kitendawili na kuuambia fumbo!

3Sema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kulikuwako tai mkubwa mwenye mabawa makubwa na manyoya marefu mabawani ya kumwendesha, nayo mengi mno yalikuwa yenye rangi; huyo akaja Libanoni, akajichukulia kilele cha mwangati.

4Chipuko lake la juu penyewe akalivunja, akalipeleka katika nchi yenye biashara, akalitia mjini, wachuuzi wakaamo.[#Ez. 16:29.]

5Kisha akachukua nayo mbegu ya hiyo nchi, akaipanda shambani panapopandwa mbegu, kwenye maji mengi, iwe kijiti, akaitunza kama mbula.

6Ikaota, ikawa mzabibu uliotambaa wenye kisiki kifupi, kwani matawi yake yalimgeukia mwenyewe, nayo mizizi yake ilikuwa chini yake yeye; ukawa mzabibu wa kweli, ukapata matawi yaliyochipuza majani mazuri.[#Ez. 19:10.]

7Kukawa na tai mkubwa mwingine mwenye mabawa makubwa yenye manyoya mengi; mara ule mzabibu ukampindukia yeye, mizizi yake imtwetee kwa kumtamani, nayo matawi yake ukamwelekezea yeye, aunyweshe kuliko hayo matuta, ulikopandwa.

8Nao ulikuwa umepandwa katika shamba zuri lenye maji mengi, uchipuke matawi yatakayoleta matunda, uwe mzabibu wenye utukufu.

9Basi, sema: hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Je? Utafanikiwa? Yule hataing'oa mizizi yake na kuyakata matunda yake, ukauke? Kweli majani yote ya machipuko yake yatakauka; hautatakiwa mkono wenye nguvu wala watu wengi wa kuung'oa kwenye mizizi yake.

10Kweli ulikuwa umepandwa, lakini utafanikiwa? Hautakauka kabisa, upepo utokao upande wa maawioni kwa jua utakapouvumia? Utakauka kweli hapo hapo matutani, ulikochipukia.

11Neno la Bwana likanijia la kwamba:

12Uambie mlango huu mkatavu: Je? Hamwijui maana yake hayo? Sema: Mwemwona mfalme wa Babeli, akija Yerusalemu, akimchukua mfalme wake na wakuu wake na kuwapeleka kwake Babeli.[#2 Fal. 24:10,15.]

13Kisha alichukua mmoja wa kizazi cha kifalme, akafanya naye agano na kumwapisha. Lakini wenye nguvu wa nchi hii akawachukua,[#2 Fal. 24:17.]

14ufalme ukae chini tu, usijikweze, usimamike tu kwa kulishika agano lake.

15Kisha huyo akakataa kumtii, akatuma wajumbe kwenda Misri, wampe farasi na watu wengi. Aliyeyafanya hayo atawezaje kufanikiwa na kujiokoa? Kwa kulivunja agano ataponaje?

16Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, kweli atakufa mle Babeli, mle mjini, mfalme akaamo aliyempa ufalme, kwa kuwa alikibeza kiapo chake na kulivunja agano lake.

17Naye Farao hataleta vikosi vikubwa vyenye watu wengi amfalie kitu vitani, watakapomzungushia ukingo wa mchanga na kujenga minara, kusudi waangamize watu wengi na kuwaua.

18Kwa kuwa alikibeua kiapo na kulivunja agano, aliloliinulia mkono, kwa hiyo ataona: kwa kuyafanya hayo yote hataokoka.

19Kwa sababu hii ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, kiapo changu alichokibeua, na agano langu, alilolivunja, nitamtwika kichwani.

20Nami nitamtegea wavu wangu, anaswe katika tanzi langu kisha nitampeleka Babeli; ndiko, nitakakomkatia shauri kwa kuyavunja maagano yangu.[#Ez. 12:13.]

21Nao watoro wake wote katika vikosi vyake vyote wataangushwa kwa panga, nao watakaosalia watatawanywa pande zote za upepo. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi Bwana nimesema.

22Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mimi nitachukua tawi la kilele cha mwangati mrefu, nilipande; pake juu penyewe katika mlima mrefu ulioinuka sana.[#Yes. 11:1; 53:2.]

23Katika huo mlima mrefu wa Isiraeli nitalipanda, lichupuke matawi yatakayozaa mbegu, nalo litakuwa mwangati wenye utukufu; chini yake watakaa ndege wa kila namna wenye manyoya mbalimbali, chini kivulini mwa matawi yake watajenga matundu yao.[#Ez. 20:40; Dan. 4:12; Mat. 13:32.]

24Ndipo, miti yote ya shambani itakapojua, ya kuwa mimi Bwana hunyenyekeza mti mrefu, tena hukuza mti mfupi, ya kuwa mimi hukausha mti mbichi, tena huchipuza mti mkavu. Mimi Bwana niliyeyasema nitayafanya.[#Ez. 21:26.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania