Ezekieli 20

Ezekieli 20

Ukatavu wao Waisiraeli wa kale na wa sasa.

1Ikawa katika mwaka wa 7 mwezi wa tano siku ya kumi, ndipo waume wazee wa Kiisiraeli walipokuja kumwuliza Bwana, wakakaa mbele yangu.[#Ez. 14:1.]

2Neno la Bwana likanijia la kwamba:[#Ez. 14:3.]

3Mwana wa mtu, sema na wazee wa Kiisiraeli, uwaambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Inakuwaje, mkija kuniuliza? Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, siulizwi nanyi! ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.

4Haitafaa, ukiwahukumu wewe? Je? Haitafaa ukiwahukumu wewe, mwana wa mtu? Wajulishe machukizo ya baba zao!

5Waambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Siku ile, nilipowachagua Waisiraeli, niliuinua mkono wangu na kuwaapia walio uzao wa mlango wa Yakobo, nikajijulisha kwao katika nchi ya Misri, nikauinua mkono wangu na kuwaapia kwamba: Mimi ni Bwana Mungu wenu.[#2 Mose 6:7-8.]

6Siku ile niliuinua mkono wangu na kuwaapia, ya kuwa nitawatoa katika nchi ya Misri na kuwapeleka katika nchi, niliyowachagulia kuwa nchi ichuruzikayo maziwa na asali, tena kuwa nchi iliyo urembo wa nchi zote.

7Ndipo, nilipowaambia: Yatupeni kila mtu hayo yatapishayo kwa kutazamwa tu! Msijipatie uchafu kwa kuyatambikia magogo yao Wamisri ya kutambikia! Mimi Bwana ni Mungu wenu.[#Yos. 24:14,23.]

8Kisha wakanikataa wasipotaka kunisikia, hawakuyatupa kila mtu matapisho yake aliyoyatazama, wala hawakuyaacha magogo yao Wamisri ya kutambikia, nikasema: Nitawamwagia makali yangu yenye moto, machafuko yangu yamalizike kwao kulekule katika nchi ya Misri.

9Lakini nikafanya mengine kwa ajili ya Jina langu, lisitiwe uchafu machoni pao wamizimu, kwani wanakaa wakizungukwa nao, nami nilijijulisha machoni pao kwamba: Nitawatoa katika nchi ya Misri.[#Ez. 36:21-22; 2 Mose 32:12.]

10Basi, nikawatoa katika nchi ya Misri, nikawapeleka nyikani.

11Nikawapa maongozi yangu, nikawajulisha nayo mashauri yangu, nayo ndiyo yatakayompa mtu uzima, akiyafanya.[#3 Mose 18:5.]

12Nikawapa nazo siku zangu za mapumziko, ziwe kielekezo cha maagano, tuliyoyaagana mimi nao, wajue, ya kuwa mimi ni Bwana awatakasaye.[#2 Mose 31:13,17.]

13Lakini walio mlango wa Isiraeli wakanikataa nako nyikani: maongozi yangu hawakuyafuata, mashauri yangu wakayabeza, nayo ndiyo yatakayompa mtu uzima, akiyafanya. Nazo siku zangu za mapumziko wakazipitia uchafu sana, nikasema: Nitawamwagia makali yangu yenye moto huku nyikani, yawamalize.

14Lakini nikafanya mengine kwa ajili ya Jina langu, lisitiwe uchafu machoni pao wamizimu walioona kwa macho yao, jinsi nilivyowatoa.[#Ez. 20:9.]

15Nami nikauinua mkono wangu na kuwaapia huko nyikani kwamba: Sitawapeleka katika nchi ile, niliyowapa, ichuruzikayo maziwa na asali, iliyo urembo wa anchi zote,[#4 Mose 14:12.]

16kwa kuwa waliyabeza mashauri yangu, hawakuyafuata maongozi yangu, wakazipatia siku zangu za mapumziko uchafu, kwani mioyo yao ikayaendea magogo yao ya kutambikia.

17Lakini macho yangu yakawaonea uchungu, nisiwaangamize; basi, nikaacha kuwamaliza nyikani.

18Nikawaambia wana wao huko nyikani: Maongozi ya baba zenu msiyafuate, wala msiyashike mashauri yao, wala msijichafue kwa kuyatambikia magogo yao!

19Mimi Bwana ni Mungu wenu, yafuateni maongozi yangu! Yashikeni nayo mashauri yangu, myafanaye!

20Zitakaseni siku zangu za mapumziko, ziwe kielekezo cha maagano, tuliyoyafanya mimi nanyi, mjue, ya kuwa mimi ni Mungu wenu![#Ez. 20:12.]

21Lakini hao wana nao wakanikataa: maongozi yangu hawakuyafuata, mashauri yangu hawakuyashika, wayafanye, nayo ndiyo yatakayompa mtu uzima, akiyafanya; siku zangu za mapumziko wakazipatia uchafu, nikasema: Nitawamwagia makali yangu yenye moto, machafuko yangu yamalizike kwao nyikani.

22Kisha nikaurudisha mkono wangu, nikafanya mengine kwa ajili ya Jina langu, lisitiwe uchafu machoni pao wamizimu walioona kwa macho yao, jinsi nilivyowatoa.[#Ez. 20:9.]

23Nami nikauinua mkono wangu na kuwaapia huko nyikani kwamba: Nitawatawanya kwenye wamizimu na kuwatupatupa katika nchi zao,

24kwa kuwa hawakuyafanya mashauri yangu, wakayabeza maongozi yangu, wakazipatia siku zangu za mapumziko uchafu, wakayatazamia kwa macho yao magogo, baba zao waliyoyatambikia.

25Ndipo, mimi nami nilipowatolea maongozi yasiyokuwa mema, hata amashauri yasiyoweza kuwapa uzima.

26Nikawapatia uchafu kwa vipaji vyao vya tambiko, wakawapitisha motoni wote waliofungua tumbo la mama, kusudi niwastushe, wajue, ya kuwa mimi ni Bwana.[#Ez. 20:31; 2 Mambo 33:6.]

27Kwa hiyo sema na mlango wa Isiraeli, wewe mwana wa mtu, uwaambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Hata kwa neno hili baba zenu walinitukana, wakilivunja agano.

28Nilipokuwa nimekwisha kuwapeleka katika nchi, niliyowaapia kwa kuuinua mkono wangu kwamba: Nitawapa basi, po pote walipoona kilima kirefu, napo walipoona mti wenye majani mengi, ndipo, walipochinja ng'ombe zao za tambiko, wakatoa hapohapo vipaji vyao vya tambiko, kusudi wanikasirishe, wakavukiza hapo uvumba wao wenye mnuko wa kupendeza, wakamwagia hapo vinywaji vyao vya tambiko.

29Nikawauliza: Kiko kilima gani, mnachokijia hapo? Kwa hiyo jina lake likaitwa Kilima hata siku ya leo.

Mapatilizo na maagizo.

30Kwa hiyo uambie mlango wa Isiraeli: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Je? Mnajipatia uchafu kwa kuzishika njia za baba zenu? Je? Nanyi mnafanya ugoni kwa kuyafuata matapisho yao?

31Hata kwa kutoa vipaji vyenu vya tambiko, mkiwapitisha wana wenu motoni, mnajipatia uchafu na kuyatumikia magogo yenu yote ya kutambikia mpaka siku ya leo, sasa je? Mimi niulizwe nanyi mlio mlango wa Isiraeli? Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Hivyo nilivyo Mwenye uzima, sitaulizwa nanyi kabisa![#Ez. 20:26; 2 Fal. 16:3; 17:17.]

32Nayo yanayowazwa rohoni mwenu hayatakuwa kabisa, ninyi mkisema: Nasi na tuwe, kama wamizimu nao wa koo za nchi hizi walivyo, tukitumikia miti na mawe.

33Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, mimi nitakuwa mfalme wenu kwa kiganja chenye nguvu na kwa mkono ukunjukao na kwa makali yenye moto yamwagwayo.

34Nami nitawatoa kwenye makabila mengine nikiwakusanya na kuwatoa katika nchi hizi, mlikotupwa kwa kiganja chenye nguvu na kwa mkono ukunjukao na kwa makali yenye moto yamwagwayo.

35Nitawapeleka katika nyika ya makabila mengine; ndiko, nitakakowakatia mashauri uso kwa uso.[#Hos. 2:14.]

36Kama nilivyowakatia baba zenu shauri katika nyika ya Misri, ndivyo, nitakavyofanya shauri nanyi; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#4 Mose 14:22-23.]

37Nitawapitisha chini ya fimbo ya uchungaji, nije kuwashurutisha kulishika agano.

38Nitatenga kwenu wakatavu nao walionikosea, nikiwatoa katika nchi wakaako ugeni, wasiingie nchi ya Waisiraeli; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.

39Tena kwa ajili yenu mlio mlango wa Isiraeli Bwana Mungu anasema hivi: Haya! Nendeni kila mtu kuyatumikia magogo yenu ya kutambikia! Lakini siku za nyuma mtanisikiliza kabisa, msilitie jina la Patakatifu pangu tena uchafu kwa vipaji vyenu vya tambiko na kwa magogo yenu ya kutambikia.

40Kwani ndivyo, asemavyo Bwana: Katika mlima wangu mtakatifu utakaokuwa mlima mrefu wa Isiraeli ndiko, watakakonitumikia wao wa milango yote ya Isiraeli nazo nchi zake zote; tena ndiko, nitakakowapendeza nikitaka kuvipokea vipaji vyenu, mtakavyonitolea, nayo malimbuko yenu ya kunitambikia katika yote, mtakayonitakasia.[#Ez. 17:23.]

41Hapo nitawapendeza na kuutaka mnuko mzuri, nitakapowatoa kwenye makabila mengine na kuwakusanya, mzitoke hizo nchi, mlikotawanywa; ndipo, nitakapotakaswa kwenu machoni pao wamizimu.

42Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nikiwapeleka katika nchi ya Isiraeli, katika ile nchi niliyowaapia na kuuinua mkono wangu kwamba: Nitawapa baba zenu.

43Nanyi huko mtazikumbuka njia zenu na matendo yenu, mliyojipatia uchafu nayo, nanyi mtajichukia wenyewe kwa ajili ya mabaya yenu yote, mliyoyafanya.[#Ez. 36:31-32.]

44Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapowafanyizia hivyo kwa ajili ya Jina langu, lakini sivyo kwa ajili ya njia zenu mbaya, wala kwa ajili ya matendo yenu maovu, ninyi wa mlango wa Isiraeli; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.

45Neno la Bwana likanijia la kwamba:

46Mwana wa mtu, uelekeze uso wako kutazama upande wa kusini, uitangazie nchi yenye jua kali, ukiufumbulia mwitu ulioko kwenye mbuga za kusini yatakayokuwa.

47Uuambie huo mwitu ulioko kusini: Lisikie neno la Bwana! Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaona, nikiwasha moto kwako utakaokula kwako miti mibichi yote na miti mikavu yote; miali ya moto huo uwakao haitazimika, mpaka nyuso zote toka kusini hata kaskazini ziunguzwe nao.

48Ndipo, wote wenye miili watakapoona ya kuwa mimi ni Bwana, ya kuwa mimi nimewasha moto usiozimika.

49Nikasema: E Bwana Mungu, hao hunisema kwamba: Yeye siye atumiaye mafumbo?

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania