Ezekieli 21

Ezekieli 21

Panga za Wakasidi zitawajia Wayudana Waamoni.

1Neno la Bwana likanijia la kwamba:

2Mwana wa mtu, uelekeze uso wako kuutazama Yerusalemu, upatangazie Patakatifu na kuifumbulia nchi ya Isiraeli yatakayokuwa!

3Iambie nchi ya Isiraeli: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Utaona, nikikujia na kuuchomoa upanga wangu alani mwake, niangamize waongofu na wapotovu, watoweke kwako.

4Kwa kuwa nitaangamiza waongofu na wapotovu, watoweke kwako, kwa hiyo upanga wangu utachomolewa alani mwake, uwapige wote wenye miili toka kusini hata kasikazini.

5Ndipo, wote wenye miili watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, ya kuwa nimeuchomoa upanga wangu alani mwake, usirudi humo tena.

6Lakini wewe mwana wa mtu, piga kite! Kwa viuno vilivyovunjika na kwa uchungu ulio mkali piga kite, wakuone!

7Tena wakikuuliza: Unapiga kite? uwaambie: Kwa hayo, niliyoyasikia, ya kuwa yatakuja, moyo wote umeyeyuka, nayo mikono ikalegea, nayo roho yote ikazimia, nayo magoti yakaja kugeuka kuwa kama maji. Mtaona, yakija kutimia; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.

8Neno la Bwana likanijia la kwamba:

9Mwana wa mtu, yafumbue yatakayokuwa ukisema: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Sema: Uko upanga, ni upanga mwenyewe, umenolewa na kusuguliwa vema.[#Ez. 32:20.]

10Umenolewa, kusudi uchinje machinjo, ukasuguliwa, kusudi ukatuke kama umeme. Au tuufurahie? Fimbo ya kumpigia mwanangu haishindwi na mti wo wote.

11Aliutoa, usuguliwe vema, apate kuushika mkononi; nao ukanolewa ule upanga, ukasuguliwa vema, mwuaji apewe mkononi.

12Piga yowe na kupaza sauti, mwana wa mtu! Kwani huo ndio unaowajia walio ukoo wangu, ndio unaowajia nao wakuu wa Isiraeli; wametupwa kwenye upanga pamoja nao walio ukoo wangu. Kwa hiyo jipige mapaja!

13Kwani walijaribiwa, lakini imewafaliaje? Sasa je? Fimbo nayo ikatae kuwapiga? Haitakuwa; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#Yes. 1:5.]

14Nawe mwana wa mtu, yafumbue yatakayokuwa ukiyapiga makofi! Kwani huo upanga utakuja mara mbili, hata mara tatu, ndio upanga upigao madonda kabisa, kweli ndio upanga mkubwa upigao madonda, ndio utakaowazunguka,

15kusudi mioyo iyeyuke, tena wengi waanguke kwa kukwazwa; malangoni pao po pote nitatoa matisho ya huo upanga. A! Umefanywa, umerimete kama umeme! Umenolewa, upate kuchinja!

16Jitege kupiga kuumeni! Jiweke tayari kupiga kushotoni! Piga po pote, makali yako yatakapoelekea!

17Mimi nami nitayapiga makofi yangu nitakapoyatuliza makali yangu yenye moto; mimi Bwana nimeyasema.

18Neno la Bwana likanijia la kwamba:

19Wewe mwana wa mtu, jitengenezee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli utakazozishika! Zote mbili zitatoka katika nchi moja; hapo njia pembeni pachore mkono, uelekezee mji, ndivyo uuchore![#Ez. 4:1.]

20Tengeneza njia, upanga utayoishika kwenda Rabati ya wana wa Amoni, tena nyingine kwenda Yuda katika Yerusalemu ulio na boma.

21Kwani mfalme wa Babeli atasimama hapo penye njia panda, zile njia mbili zinapoanzia, apate kuagua uaguaji, akisukasuka mishale au akipiga bao au akitazama maini.

22Kuumeni kwake kutaanguka kura ya Yerusalemu kwamba: aweke magogo ya kuvunjia boma, afumbue kinywa kupiga kelele, apaze sauti kupiga yowe, aweke magogo ya kuvunjia penye malango, azungushe ukingo wa mchanga, ajenge minara.

23Nao uaguaji kama huo utakuwa uwongo machoni pao, ijapo wauapie viapo; lakini yeye atawakumbusha manza, walizozikora, kusudi watekwe.

24Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Kwa kuwa mnanikumbusha manza, mlizozikora, mapotovu yenu yakifunuliwa, makosa yenu yakitokea waziwazi kwa matendo yenu yote, kwa kuwa mnakumbukwa hivyo, basi, mtakamatwa kwa mikono.

25Lakini wewe mkuu wa Isiraeli uliyejipatia uchafu kwa kuacha kunicha, siku yako imetimia, kwa kuwa ni wakati wa mwisho wa kukora manza.

26Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kiondoe kilemba cha kifalme! Ivue nayo taji! Haya ya sasa siyo yatakayokuwa tena. Yaliyoko chini ndiyo, watakayoyakweza, nayo yaliyoko juu ndiyo, watakayoyanyenyekeza.[#Ez. 17:24; 2 Mose 28:4; Luk. 18:14.]

27Mabomoko na mabomoko na mabomoko ndiyo, nitakayoyaweka huku; lakini nayo siyo yatakayokuwa vivyo hivyo, mpaka aje, ambaye ni haki yake; yeye ndiye, nitakayempa.[#1 Mose 49:10.]

28Nawe mwana wa mtu, yafumbue yatakayokuwa ukisema: Haya ndiyo Bwana Mungu anayowaambia wana wa Amoni kwa ajili ya matusi yao, sema: Upanga ulio upanga kweli umechomolewa, nao umesuguliwa, upate kuchinja na kuua kabisa, kusudi uwe kama umeme.[#Ez. 25:2-7.]

29Lakini wamekutazamia maono yasiyokuwa, wakakuagulia uwongo, wakuvute, uje kuwapiga shingo zao waliojipatia uchafu na kuacha kunicha, kwamba siku yao imetimia, kwa kuwa ni wakati wa mwisho wa kukora manza.

30Lakini urudishe huo upanga alani mwake! Mahali, ulipoumbwa katika nchi, ulikozaliwa, nitakukatia shauri.

31Nitakumwagia makali yangu, kwa moto wa machafuko yangu nitakufokea, kisha nitakutia mikononi mwa watu wasio wa kimtu, walio mafundi wa maangamizo.

32Utakuwa chakula cha moto, damu yako itamwagwa katika nchi yako katikati, hutakumbukwa tena, kwani mimi Bwana nimeyasema.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania