The chat will start when you send the first message.
1Neno la Bwana likanijia la kwamba:[#Ez. 24:6.]
2Wewe mwana wa mtu, hutauhukumu, kweli hutauhukumu mji huo ujaao damu za watu? Uujulishe machukizo yake yote!
3Sema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wewe ndiwe mji uliomwaga mwake damu za watu, siku zake zitimie, ukafanya magogo ya kutambikia, ukajipatia uchafu nayo.
4Kwa hizo damu zako, ulizozimwaga, umekora manza, tena kwa hayo magogo ya kutambikia, uliyoyafanya, umejipatia uchafu, hivyo umezifikisha siku zako karibu, ukaja penye mwisho wa miaka yako. Kwa hiyo nitakutia soni kwa wamizimu, usimangwe katika nchi zote.
5Nchi zilizoko karibu yako nazo zilizoko mbali yako zitakusimanga kwamba: Umelipatia jina lako uchafu, ukafanya matata mengi.
6Tazama, wakuu wa Isiraeli wote walikuwa mwako wakiitumia mikono yako kumwaga damu za watu.
7Mwako watu hawachi wala baba wala mama, nao wageni huwafanyia ukorofi mwako, wafiwao na wazazi nao wajane watu huwatesa mwako.[#2 Mose 22:21-22.]
8Patakatifu pangu wewe hupabeza, nazo siku zangu za mapumziko wewe huzichafua.
9Mwako mna watu wanaowaonea wenzao, wapate kumwaga damu zao, tena mwako wamo wanaokula vilimani vyakula vya tambiko, hata uzinzi watu hufanya mwako.
10Yenye soni ya baba watu huyafunua mwako, mwako huwatumia kwa nguvu nao wanawake wenye uchafu kwa kuwa na siku zao.[#3 Mose 18:7,19.]
11Wako wanowafanyizia wake wa wenzao yachukizayo, tena wako wanojichafua kwa kuwatumia wakwe wao wa kike kufanya uzinzi nao, tena wako wanaowatumia kwa nguvu nao maumbu zao waliozaliwa na baba yao.[#3 Mose 18:9,15,20.]
12Mwako wamo wanotaka kupenyezewa fedha, kusudi wamwage damu, tena huchukua faida na nyongeza za kupunja, mkiwadanganya wenzenu kwa ukorofi, lakini mimi mmenisahau; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#2 Mose 22:25.]
13Lakini utaniona, nikiyapiga makofi yangu kwa ajili ya mali zako, ulizojipatia kwa udanganyifu, na kwa ajili ya damu zako zilizomwagwa mwako mjini katikati.
14Je? Moyo wako utasimama? Je? Mikono yako itakuwa na nguvu zao siku zile, nitakapokufanyizia mambo? Mimi Bwana nimeyasema, nami nitayafanya.
15Nitakutawanya kwa wamizimu na kukutupatupa katika nchi zao; hivyo nitaukomesha uchafu wako kabisa, uishe kwako!
16Nawe utakuwa mwenye upujufu machoni pao wamizimu; ndipo, utakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.
17Neno la Bwana likanijia la kwamba:[#Yes. 1:22; Yer. 6:28.]
18Mwana wa mtu, walio mlango wa Isiraeli wameniwia kama mavi ya chuma, wao wote ni kama shaba nyekundu na shaba nyeupe na chuma na risasi katika tanuru, wamegeuka kuwa mitapo ya fedha.
19Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa ninyi nyote mmegeuka kuwa mitapo ya fedha, mtaniona, nikiwakusanya ninyi mjini mwa Yerusalemu;
20kama fedha na shaba nyekundu na chuma na shaba nyeupe zinavyokusanywa ndani ya tanuru, ziwashiwe moto, zipate kuyeyuka, hivyo ndivyo, nitakavyowakusanya kwa makali yangu na kwa machafuko yangu yenye moto, niwatie mle ndani kuwayeyusha.
21Kweli nitawakusanya, niwawashie moto wa machafuko yangu; ndivyo, nitakavyowayeyusha mle ndani.
22Kama wanavyoyeyusha fedha ndani ya tanuru, ndivyo mtakavyoyeyushwa ndani yake. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nimewamwagia makali yangu yenye moto.
23Neno la Bwana likanijia la kwamba:
24Mwana wa mtu, iambie nchi hii: Wewe ndiwe nchi isiyotakasika, isiyonyweshwa mvua siku ya kukasirikiwa.
25Wafumbuaji wake waliomo mwake wamekula njama, wakawa kama simba angurumaye akinyafua nyama, aliowakamata; nao wakazila roho za watu, wakazitwaa nazo mali zao na vitu vyao vyenye kiasi, wakawaua waume wao wanawake wengi waliokuwamo, wakawageuza kuwa wajane.[#Ez. 34:3,8; Sh. 14:4; Mat. 23:14.]
26Watambikaji wao wakayapotoa Maonyo yangu, wakapachafua Patakatifu pangu hawakuyapambanua matakatifu nayo yatumiwayo tu, wala hawakuyajulisha watu kuyapambanua yaliyo machafu nayo yaliyotakata, tena wameyafumba macho yao penye siku zangu za mapumziko nikapatiwa uchafu katikati yao.[#Ez. 44:23; Sef. 3:4.]
27Wakuu wao waliokuwa mle mjini wakawa kama chui wanaonyafua nyama waliowakamata, hutaka kumwaga damu za watu na kuziangamiza roho zao, kusudi wajipatie mali za madanganyo yao.
28Nao wafumbuaji wake huyapaka mambo yao yote chokaa, wakiona maono ya uwongo na kusema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema, naye Bwana hakusema neno.[#Ez. 13:6.]
29Watu wa nchi hii hukorofisha kabisa na kupokonya sana, hutesa wanyonge na wakiwa, hukorofisha nao wageni kwa njia zisizonyoka.[#Ez. 22:7.]
30Nikatafuta mtu wa kwao afaaye kuujenga ukuta na kusimama mbele yangu palipoatuka ufa, aikingie nchi hii, nisiiangamize, lakini sikumwona.[#Ez. 13:5.]
31Nikawamwagia makali yangu nikawamaliza kwa moto wa machafuko yangu, nikawatwika njia zao vichwani pao; ndivyo asemavyo Bwana Mungu.[#Ez. 21:31.]