Ezekieli 23

Ezekieli 23

Waisiraeli na Wayuda hufanya ugoni na wamizimu.

1Neno la Bwana likanijia la kwamba:

2Mwana wa mtu, kulikuwako wanawake wawili waliozaliwa na mama yao mmoja.

3Wakafanya ugoni katika nchi ya Misri; wangaliko wasichana bado, walifanya ugoni. Huko wakapenda kushikwashikwa vifua vyao na kubanwabanwa maziwa ya uwanawali wao.

4Majina yao mkubwa aliitwa Ohola (Hema lake) naye nduguye Oholiba (Hema langu limo mwake); wakawa wangu, wakazaa wana wa kiume na wa kike. Nayo hayo majina yao lile la Ohola lilikuwa la Samaria, nalo la Oholiba lilikuwa la Yerusalemu.

5Ohola akafanya ugoni alipokuwa ni wangu, akawatamani wapenzi wake Waasuri waliomkaribia.

6Walikuwa wamevaa nguo za kifalme za rangi nyeusi; nao walikuwa watawala nchi na wakuu, wote walikuwa vijana wa kutamaniwa kwa kupendeza, wakaja wakichukuliwa na farasi, hao farasi ndio waliopandwa nao.

7Hao ndio, aliojitolea kwa ugoni wake, kwani wote walikuwa vijana wateule wa wana wa Asuri, kwao wote, aliowatamani, akajipatia uchafu na kuyatumikia magogo yao ya kutambikia.

8Nao ugoni wake, alioufanya Misri, hakuuacha; kwani wao walilala kwake, alipokuwa msichana bado, nao ndio walioyabanabana maziwa ya uwanawali wake wakimmwagia ugoni wao.

9Kwa hiyo nimemtia mikononi mwao wapenzi wake, ndimo mikononi mwa wana wa Asuri, aliowatamani,

10Nao waliyafunua yake yenye soni, wakawachukua wanawe wa kiume nao wa kike, naye mwenyewe wakamwua kwa upanga. Kisha jina lake likatumiwa kwa wanawake kuwa tisho, alipokuwa amekwisha kuhukumiwa.[#Ez. 23:29.]

11Ijapo nduguye Oholiba alikuwa ameyaona, akauzidisha ubaya wa tamaa zake kuliko yule, nao ugoni wake ukazidi kuliko ugoni wake yule.[#Ez. 16:51.]

12Akawatamani wana wa Asuri, watawala nchi na wakuu wakamkaribia wakiwa wamevaa nguo za urembo kabisa, nao wakaja wakichukuliwa na farasi, hao farasi ndio waliopandwa nao, wao wote walikuwa vijana wa kutamaniwa kwa kupendeza.

13Nikamwona, alivyochafuliwa. Hao wawili njia yao ilikuwa moja tu.

14Naye huyu akaendelea kwa ugoni wake, alipoona waume waliochorwa ukutani, ni sanamu za Wakasidi zilizochorwa mle na kutiwa rangi nyekundu.

15Walikuwa wamejifunga ukanda viunoni pao, vichwani pao walikuwa wamejifunga vilemba vya nguo za rangi vipana sana, sura zao wote walionekana kuwa wapanda magari ya vita, walifanana nao wana wa Babeli; ndiko, hao wakasidi walikozaliwa.

16Akawatamani alipowaona kwa macho yake, akatuma wajumbe kwenda kwao katika nchi ya wakasidi.

17Ndipo, wana wa Babeli walipokuja kwake kulala naye kwa kumpenda, wakamtia uchafu kwa ugoni wao; alipokwisha kujipatia uchafu kwao, roho yake ikajitenga nao.

18Alipoufunua ugoni wake na kuyafunua yake yenye soni, ndipo, roho yangu ilipojitenga naye, kama ilivyojitenga na dada yake.

19Akauzidisha ugoni wake akizikumbuka siku za ujana wake, alipofanya ugoni katika nchi ya Misri.

20Akawatamani sana wazinzi wa huko walio wenye miili kama ya punda, nazo tamaa zao za kutokeza mbegu zilikuwa kama za madume ya farasi.

21Hivyo uliutazamia uzinzi wa ujana wako, wale walioko Misri walipoyabanabana maziwa yako na kuvishikashika vifua vya uwanawali wako.

Hukumu itakayowapata kwa kumwacha Mungu.

22Kwa hiyo, Oholiba, hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaniona, nikiwaamsha wapenzi wako, wakujie, ambao roho yako ilijitenga nao. Nitawaleta, wakujie toka pande zote:

23wama wa Babeli na Wakasidi wote, Pekodi na Soa na Koa na wana wote wa Asuri pamoja nao; ndio vijana wa kutamaniwa kwa kupendeza, wote ni watawala nchi na wakuu, wapanda magari ya vita na mabwana wakubwa, wote ni wenye kupanda farasi.

24Hao watakujia wakileta vyombo vya vita na magari na magurudumu na mikutano ya makabila ya watu wenye ngao kubwa na ngao ndogo na makofia ya vita, kisha watajipanga kwako na kukuzunguka. Nami nitalipeleka shauri lako mbele yao, nao watakukatia shauri, kama wanavyokata mashauri kwao.[#Luk. 19:43.]

25Kisha nitakutolea wivu wangu, wao wakufanyizie mambo, wayatakayo kwa makali yao yenye moto; watakukata pua na masikio, kisha utauawa kwa upanga. Kisha watawachukua wanao wa kiume na wa kike, nawe wewe mwisho utateketezwa kwa moto.

26Watakuvua nguo zako wayachukue mapambo yako matukufu.

27Hivyo nitaukomesha uzinzi wako, uishe kwako pamoja na ugoni wako ulioanzia katika nchi ya Misri, hutaweza tena kuyainua macho yako, uwatazame, wala hutaikumbuka tena nchi ya Misri.

28Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaniona, nikikutia mikononi mwao, unaowachukia, namo mikononi mwao ambao roho yako ilijitenga nao.

29Nao watakufanyizia mambo, wayatakayo kwa uchukivu wao, wakiyachukua mapato yako yote kisha watakuacha mwenye uchi pasipo nguo ya kujifunika; ndipo, utakapokuwa umefunuka ugoni wako utiao soni nao uzinzi wako ulio pamoja na ugoni wako.

30Watakufanyizia hayo, kwa kuwa uliwakimbilia wamizimu, ufanye ugoni nao, tena kwa kuwa ulijipatia uchafu kwa magogo yao ya kutambikia.

31umeishika njia ya dada yako, kwa hiyo ninakupa kinyweo chake mkononi mwako.[#Ez. 23:33.]

32Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kinyweo cha dada yako utakinywa kilicho kirefu na kipana, uchekwe na kufyozwa! Kwani ni mengi yaliyoenea mle ndani.

33Ndipo, utakapolewa kabisa na kuona majonzi mengi, kwani hicho kinyweo cha dada yako Samaria ni kinyweo chenye mastusho na ukiwa.[#Yes. 51:17; Yer. 25:15,18.]

34Utakinywa, mpaka ukimalize kwa kufyonza, kisha sharti uvilambe navyo vigae vyake na kuyakwaruza maziwa yako, kwani mimi nimeyasema; ndivyo asemavyo Bwana Mungu.

35Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa umenisahau, ukanitupa mgongoni kwako, basi, wewe nawe jitwike uzinzi wako na ugoni wako!

36Bwana akaniambia: Mwana wa mtu, hutamhukumu Ohola naye Oholiba? Waumbulie machukizo yao!

37Kwani wamevunja unyumba, nazo damu zimo mikononi mwao. Unyumba wameuvunja wakiyatamani magogo yao ya kutambikia nao wana wao, walionizalia mimi, wamewapitisha motoni, wayawie vipaji vya tambiko vya kula.[#Yer. 7:31.]

38Tena wamenifanyizia nayo hayo: Siku ileile wamepatia Patakatifu pangu uchafu, wakazitangua siku zangu za mapumziko.

39Walipowachinja wana wao kuwa ng'ombe za tambiko za yale magogo yao, siku ileile wakapaingia Patakatifu pangu, wapatie uchafu. Tazama, hivyo ndivyo, walivyofanya Nyumbani mwangu.

40Tena wametuma hata kwa waume walioko mbali, waje wakitoka kwao; nao hapo, mjumbe alipotumwa kuwaita, ndipo, walipokuja papo hapo. Kwa ajili yao ukaenda koga, ukajitia wanja machoni, ukajipamba na kuvaa mapambo ya urembo.

41Kisha ukajikalisha katika kitanda kizuri mno, mbele yako pakawa na meza iliyotandikwa, juu yake ukayaweka mavukizo yangu na mafuta yangu.

42Wakatulia hapo pako na kupiga makelele kama ya watu wengi, wakatuma kuita watu wakaao kwenye watu wengi, wakaletwa wanywaji waliotoka nyikani, wakawapa vikuku vya kuvaa mikononi pao na vilemba vyenye utukufu kuvaa vichwani pao.

43Nikasema: Hivyo, alivyochakaa kwa kuvunja unyumba, hata sasa ataufanya ugoni wake. Naye akaufanya.

44Watu wakaja nyumbani mwake, kama wanavyoingia mwake mwanamke mgoni; hivyo ndivyo walivyoingia mwake Ohola namo mwake Oholiba, kwa kuwa wanawake wenye uzinzi.

45Lakini waume waongofu watawakatia shauri liwe shauri lipasalo wazinzi, tena liwe shauri lipasalo waliomwaga damu kwani ndio wake wazinzi, nazo damu zimo mikononi mwao,[#3 Mose 20:10.]

46Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wakusanyie mkutano mkubwa uwatoe, watupwe huko na huko, kisha wanyang'anywe mali zao!

47Kisha watu wa huo mkutano wawapige mawe, halafu wawakatekatekwa panga zao! Nao wana wao wa kiume na wa kike wawaue! Tena nyumba zao waziteketeze kwa moto.

48Hivyo ndivyo, nitakavyoukomesha uzinzi, uishe katika nchi hii, wanawake wote waonyeke, wasifanye uzinzi kama wao.

49Hivyo ndivyo, watakavyowatika uzinzi wenu, nayo makosa ya kuyatambikia yale magogo yenu mtatwikwa; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania