The chat will start when you send the first message.
1Ikawa katika mwaka wa 11 siku ya kwanza ya mwezi, ndipo, neno la Bwana liliponijia la kwamba:
2Mwana wa mtu, Watiro waliuzomea Yerusalemu kwamba: Aha! umevunjika uliokuwa umeingiwa na makabila ya watu! Sasa watageuka, waje kwangu! Bado kidogo nitafurikiwa, kwa kuwa umebomoka![#Ez. 25:3.]
3Kwa sababu hii Bwana Mungu anasema hivi: Utaniona, nikikujia, wewe Tiro! Nitaleta mataifa mengi, wakupige, kama bahari inavyoleta mawimbi kwa mawimbi.[#Yes. 23.]
4Wataziangusha kuta za boma lake Tiro na kuibomoa minara yake nami nitauparapara mchanga wake, upatoke, mpaka nipageuze mahali pake kuwa mwamba mtupu.
5Hivyo patakuwa tu pa kuanikia nyavu katikati ya bahari, kwani mimi nimeyasema; nayo mataifa watapanyang'anyiana; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.
6Navyo vijiji vyake ulivyovijenga mrimani, watu wao watauawa kwa panga; ndipo watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.
7Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mtaniona, nikimleta Nebukadiresari, mfalme wa Babeli, aliye mfalme wa wafalme, aujie mji wa Tiro na kutoka kaskazini na kuleta farasi na magari ya watu wapandao farasi na vikosi vingi vya makabila ya watu.[#Dan. 2:37.]
8Waliomo katika vijiji vyako vya mrimani atawaua kwa panga; kisha atakujengea minara ya vita, tena atakuzungushia ukingo wa mchanga na kukujengea hapohapo vibanda kuwa ngao zao.[#Ez. 26:6.]
9Kisha atazipiga kuta za boma lako kwa vyombo vyake vya kubomolea, nayo minara yako ataivunja kwa vyuma vyake.
10Kwa kuwa na farasi wengi mavumbi yao yatakufunika, kwa mashindo ya wapanda farasi na za magurudumu na za magari kuta zako zitatetemeka, atakapoingia katika malango yako, kama watu wanavyoingia katika mji uliovunjwa kwa nguvu.
11Kwa kwato za farasi wake atazipondaponda barabara zako zote za mjini, walio ukoo wako atawaua kwa panga, nazo nguvu za vinyago vyako zitaangushwa chini.
12Vilimbiko vyako watavinyang'anya, nazo mali zako za kuchuuzia wataziteka, kuta zako za boma watazibomoa, majumba yako, uliyoyatamani kwa uzuri wao, watayavunja, kisha watayatupa baharini mawe yako na miti yako na mavumbi yako.
13Ndipo, nitakapozikomesha shangwe za nyimbo zako, zisisikiwe tena sauti za mazeze yako.[#Yes. 14:11.]
14Hivyo nitakugeuza kuwa mwamba mtupu, uwe mahali pa kuanikia nyavu, hutajengwa tena, kwani mimi Bwana nimeyasema; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.
15Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema kwa ajili ya Tiro: Je? Kwa uvumi wa anguko lako, kwa mauguzi yao walioumizwa na kuuawa kabisa kwa panga mjini mwako nchi za pwani zisitikisike?
16Wafalme wote wa nchi zilizoko baharini watashuka katika viti vyao vya kifalme wakiziondoa kanzu zao za urembo na kuzivua nazo nguo zao za rangi, kisha watajivika mastuko na kukaa chini, wakistuka mara kwa mara kwa kupigwa na bumbuazi kwa ajili yako.
17Kisha watakutungia ombolezo la kukulilia kwamba: kumbe umeangamia uliokaa baharini, uliokuwa mji wa kusifiwa tu kwa kukaa na nguvu zake baharini, huo wenyewe na watu wake waliokuwamo waliowatisha wote waliokaa pwani kwao!
18Siku hiyo, utakapoangushwa, nchi zilizoko baharini zitakuwa zimestuka, navyo visiwa vilivyomo baharini vitakuwa vimetishika sana kwa kutoweka kwako.
19Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nitakapokutoa kuwa mji uliobomolewa, kuwa kama miji mingine isiyokaa watu, nitakapokupandishia mawimbi ya bahari, maji yao mengi yakufunike,
20ndipo, nitakapokusukuma, ushuke kwao walioshuka shimoni, kwao watu wa kale, ndipo nitakapokukalisha kuzimuni chini ya nchi kwenye mabomoko ya kale kwao washukao shimoni, kusudi watu wasikae mwako tena. Lakini nchi yao walio wazima nitaipitia urembo mwingine.
21Nitakapokutisha, utakuwa umetoweka, usioneke tena kale na kale, ijapo watu wakutafute; ndivyo asemavyo Bwana Mungu.