The chat will start when you send the first message.
1Wewe mwana wa mtu, ufumbulie mlima wa Isiraeli yatakayokuwa, na kuiambia milima ya Isiraeli: Sikieni neno la Bwana![#Ez. 6:2.]
2Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa adui wamesema na kuwabeza: Aha! Vilima vya kale na kale vimekuwa vyetu, tuvichukue![#Ez. 25:3.]
3kwa hiyo yafumbue yatakayokuwa ukisema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kweli wamewageuza ninyi vilima kuwa mapori tu na kuwafokea pande zote, mwe vyao wa mataifa waliosalia, wawachukue, habari za kwenu zikasimuliwa na vinywa vyao vyenye ndimi mbaya, watu wakazinong'onezana.
4Kwa sababu hiyo, ninyi milima ya Isiraeli, sikieni neno la Bwana Mungu: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyoiambia milima iliyo mirefu nayo iliyo mifupi, hata makorongo na mabonde, nayo mabomoko na mapori, nayo miji iliyo mahame tu, iliyonyang'anywa na kuzomelewa na masao ya mataifa yaliyokaa na kuizunguka.
5Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kweli itakuwa kwa moto wa wivu wangu, nikisema nao walio masao ya mataifa nao Waedomu wote waliojipa wenyewe nchi yangu, waichukue, iwe yao, wakafurahi kwa mioyo yote na kwa roho zenye mabezo walipowafukuza wa kwenu na kuwanyang'anya mali zao.[#Ez. 35:15.]
6Kwa hiyo ifumbulie nchi ya Isiraeli yatakayokuwa ukiiambia milima mirefu na mifupi, nayo makorongo na mabonde: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mtaniona, nikisema kwa wivu na kwa makali yangu yenye moto, kwa kuwa mmejitwika yaliyowatia soni kwa wamizimu.
7Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Mimi nimeuinua mkono wangu, kwa hiyo itakuwa kweli: wamizimu wanaokaa na kuwazunguka watajitwika wenyewe yanayowatia soni.
8Lakini ninyi, milima ya Isiraeli, mtayachipuza matawi yenu, mzae nayo matunda yenu, kwa ajili yao walio ukoo wangu wa Isiraeli, kwani hao watakuja bado kidogo.
9Kwani mtaniona, nikija kwenu na kuwageukia, mpate kulimwa na kupandwa.
10Hata watu wengi nitawakalisha kwenu wa milango yote pia ya Isiraeli, miji yao ikaliwe tena, nayo mabomoko yajengwe tena.
11Nitakalisha kwenu watu wengi na nyama wengi, wazidi tena kwa kuzaa sana. Hivyo nitawapa kuwa wengi hapo, mtakapokaa kama siku zenu za kale, nitawafanyizia mema mengi kuliko siku za kwanza; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.[#Ez. 36:38.]
12Kwenu nitawatembeza tena walio ukoo wangu wa Isiraeli, wawachukue, mwe tena fungu lao; hamtawaua tena wana wao.
13Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa watu huwaambia ninyi: Wewe ndiwe mla watu, tena ndiwe muua watoto wa kwako,
14kwa hiyo hutakula mtu tena, wala hutawaua tena watoto wa kwako; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.
15Sitaki, usikie kwako tena matusi ya wamizimu, wala hutajitwika tena yakutiayo soni kwa makabila ya watu, wala hutawakwaza tena watu wa kwako; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.
16Neno la Bwana likanijia la kwamba:
17Mwana wa mtu, walio mlango wa Isiraeli walipokaa katika nchi yao, waliitia uchafu kwa njia zao na kwa matendo yao; njia zao zilikuwa machoni pangu kama uchafu wa mwanamke mwenye siku zake.[#3 Mose 8:25,28.]
18Nikawamwagia makali yangu yenye moto kwa ajili ya damu, walipozimwaga katika nchi hiyo, tena walipojipatia uchafu na magogo yao ya kutambikia.
19Nikawatawanya kwenye wamizimu na kuwatupatupa katika hizo nchi zao nilipowahukumu kwa hivyo, njia zao na matendo yao yalivyokuwa.
20Walipofika kwenye wamizimu wakalipatia Jina langu takatifu uchafu po pote, walipofika, watu wakisema kwa ajili yao: Hawa ndio walio ukoo wake Bwana, wametolewa katika nchi yao.[#Yes. 52:5.]
21Nikaona uchungu kwa ajili ya Jina langu takatifu, wale wa mlango wa Isiraeli walilolipatia uchafu kwenye mataifa po pote, walipofika.[#Ez. 20:9.]
22*Kwa hiyo uambie mlango wa Isiraeli: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Si kwa ajili yenu, ninyi na mlango wa Isiraeli, nikiwafanyizia hivyo, ila kwa ajili ya Jina langu takatifu, mlilolipatia uchafu kwenye wamizimu po pote, mlipofika.[#Sh. 115:1; Yer. 14:7.]
23Nitalitakasa tena Jina langu kuu lililopatiwa uchafu kwenye wamizimu, mlilolipatia uchafu kwao; ndipo wamizimu watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapotakasika kwenu machoni pao; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#Ez. 37:28.]
24Nitawachukua kwenye wamizimu nikiwakusanya na kuwatoa katika hizo nchi, niwarudishe katika nchi yenu.
25Nami nitawanyunyizia maji safi, ndipo, mtakapokuwa mmesafishwa; nitawasafisha, yawaondokee makosa yenu yote nayo magogo yenu yote, mliyoyatambikia.[#Zak. 13:1; Ebr. 10:22.]
26Nitawapa mioyo mipya, namo ndani yenu nitatia roho mpya, nitaitoa miilini mwenu ile mioyo iliyo migumu kama mawe, niwape mioyo iliyolegea kama nyama.[#Ez. 11:19.]
27Nayo roho yangu nitaitia ndani yenu, niwageuze kuwa watu wanaoyafuata maongozi yangu, wayashike mashauri yangu, wayafanye.[#Ez. 37:24; 39:29; Yes. 44:3.]
28Nanyi mtakaa katika hiyo nchi, niliyowapa baba zenu, mkiwa ukoo wangu, mimi nami nitakuwa Mungu wenu.*[#Ez. 11:20.]
29Nami nitawaokoa katika machafu yenu yote, kisha nitaziita ngano, nizizidishe kuwa nyingi, sitaleta tena njaa kwenu.
30Nayo matunda ya miti nitayazidisha kuwa mengi nayo mazao ya mashamba, kusudi msitiwe soni tena kwa wamizimu mkipatwa na njaa.[#Yoe. 2:17,19.]
31Mtakapozikumbuka njia zenu mbaya na matendo yenu yasiyokuwa mazuri, ndipo, mtakapojichukia wenyewe machoni penu kwa ajili ya maovu yenu na machukizo yenu, mliyoyafanya.[#Ez. 16:61,63.]
32Ndivyo, asemavyo Bwana: Na ijulike kwenu, ya kuwa siwafanyizii hivyo kwa ajili yenu; sharti mwone soni na kuiva nyuso kwa ajili ya njia zenu, ninyi wa mlango wa Isiraeli.[#Ez. 36:22.]
33Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Siku, nitakapowasafisha na kuwaondolea manza zote, mlizozikora, ndipo, nitakapoipatia miji yenu watu wa kukaa humo, nayo mabomoko yatajengwa tena.
34Nayo nchi iliyokuwa majani tu italimwa hapohapo palipokuwa mapori matupu machoni pao wote waliopapita.
35Ndipo, watakaposema: Nchi hii iliyokuwa mapori tu imegeuka kuwa kama bustani ya Edeni, nayo miji iliyokuwa mabomoko na mahame kwa kuvunjwa kwao sasa iko na maboma, nayo inakaa watu.
36Ndipo, wamizimu watakaosalia kwao wakaao na kuwazunguka watakapojua, ya kuwa mimi Bwana nimeyajenga yaliyovunjwa, nikayapanda yaliyokuwa mapori tu. Mimi Bwana nimeyasema, nami nitayafanya.[#Ez. 17:24.]
37Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nalo hili nitawaitikia wao wa mlango wa Waisiraeli wakiniomba, niwafanyizie: Nitawazidisha kuwa watu wengi kama kondoo.[#Mika 2:12.]
38Kama kondoo wa kutambika walivyo wengi, au kama mle Yerusalemu makundi ya watu yanavyokuwa mengi siku za sikukuu, ndivyo, miji iliyo mabomoko tu itakavyojaa makundi ya watu; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.