The chat will start when you send the first message.
1Mtakapopiga kura za kujigawanyia mafungu ya nchi hii, mtatoa kwanza katika nchi hii kipande cha kumpa Bwana kuwa Patakatifu, urefu wake uwe mianzi 25000, nao upana wake uwe mianzi 10000; hapo sharti pawe Patakatifu katika mipaka yake yote ipazungukayo!
2Ndani yake pakatwe mahali penye mianzi 500 pande zake nne zipazungukazo kuwa pake Patakatifu Penyewe; mahali hapo pazungukwe pande zote na uwanda wa mikono 50.
3Mahali hapo palipopimwa utapapima tena urefu wa mianzi 25000 na upana wa mianzi 10000, napo hapo ndipo pajengwe Patakatifu patakapokuwa Patakatifu Penyewe.
4Nchi hiyo itakuwa takatifu, iwe yao watambikaji wanaofanya kazi za utumishi wa Patakatifu wakimkaribia Bwana na kumtumikia; kwa hiyo mahali hapo patakuwa pao pa nyumba zao, napo patakuwa patakatifu penye hapo Patakatifu.
5Pengine penye urefu wa mianzi 25000 na upana wa mianzi 10000 patakuwa pao Walawi wanaofanya kazi za utumishi wa Nyumba hii; hapo patakuwa mali zao za kupashika kuwa pao pa kukaa penye matuo 20.
6Kisha mtatoa tena mahali penye upana wa mianzi 5000 na urefu wa mianzi 25000 kuwa pake mji, pawe kandokando ya kile kipande kitakatifu cha nchi; hapo patakuwa mali zao wote walio mlango wa Isiraeli.
7Naye mkuu mtampa huku na huko penye kile kipande kitakatifu napo penye pake mji mbele ya kipande kitakatifu na mbele ya hapo palipo pake mji paelekeapo baharini upande wa kwenda baharini napo paelekeapo maawioni kwa jua, urefu wake ulingane na urefu wa fungu moja wa mafungu ya mashina toka mpaka wa baharini hata mpaka wa nchi uelekeao maawioni kwa jua.[#Ez. 44:3; 48:21-22.]
8Hapo patakuwa mali zake za kupashika kuwa pake kwa Waisiraeli, wakuu wangu wasiwakorofishe tena walio ukoo wangu, nayo nchi watawapa walio mlango wa Isiraeli ya kuyagawia mashina yake.
9Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Mabaya yenu, mliyoyafanya ninyi wakuu wa Isiraeli, ni mengi; kwa hiyo acheni ukorofi na unyang'anyi, mpige mashauri yaliyo sawa yaongokayo, msiwafukuze kwao tena walio ukoo wangu! ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#Ez. 46:18.]
10Sharti mtumie mizani zilizo sawa na pishi zilizo sawa na vipimo vilivyo sawa.
11Pishi moja na vibaba vinne sharti viwe kipimo kimoja sawasawa, vibaba vinne vipate kuwa fungu la sita la frasila, vilevile pishi moja iwe fungu la sita la frasila; hivyo frasila itatumika ya kulinganisha vipimo.[#3 Mose 19:36; 5 Mose 25:15.]
12Tena fedha (sekeli) moja iwe thumuni nane, fedha 20 na fedha 25 na tena fedha 15 pamoja zitakuwa mane moja, ndio shilingi 240.
13Hivi ndivyo vipaji vyangu vinavyowapasa kuvitoa: nusu kibaba kwa kila frasila ya ngano, vilevile nusu kibaba kwa kila frasila ya mawele.
14Tena mafuta, mtakayoyatoa, ni haya: kwa kila frasila mbili za mafuta ni nusu kibaba, vibaba vinne vikihesabiwa kuwa fungu la sita la frasila, kwani pishi sita ni frasila.
15Tena mwana kondoo mmoja kwa kila mia mbili za kondoo au za mbuzi walioko kwenye malisho ya Waisiraeli yanayonyweshwa. Haya yote ni ya vilaji vya tambiko na ya ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima na za kushukuru na za kuwapatia watu upozi; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.
16Watu wote pia wa nchi hii wanapaswa na kuvitoa vipaji hivi vya kumpa aliye mkuu kwa Waisiraeli.
17Tena mkuu ndiye anayepaswa na kuzitoa ng'ombe za tambiko na vilaji na vinywaji vya tambiko penye sikukuu napo penye miandamo ya mwezi napo penye siku za mapumziko; kila mara walio mlango wa Isiraeli wanapokusanyikia, yeye ndiye atakayetoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima nazo za kushukuru, awapatie upozi walio mlango wa Isiraeli.
18Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Katika mwezi wa kwanza siku ya kwanza uchukue ndama ya ng'ombe ya kiume asiye na kilema, upaeue Patakatifu!
19Mtambikaji achukue damu yake hiyo ng'ombe ya weuo, aipake mihimili ya Nyumba hii nazo pembe nne za daraja la hapo pa kutambikia, hata mihimili ya lango la ua wa ndani.
20Hivyo utavifanya hata siku ya saba ya huo mwezi kwa ajili ya mtu akosaye kwa kupotea au kwa ujinga tu. Ndivyo, mtakavyoieua Nyumba hii.[#3 Mose 4:2; 5:17.]
21Katika mwezi wa kwanza siku ya kumi na nne sharti mfanye Pasaka, ndiyo sikukuu ya siku saba, inapoliwa mikate isiyotiwa chachu.[#3 Mose 23:5.]
22Siku hiyo mkuu atoe kwa ajili yake na kwa ajili ya watu wote wa nchi hii ndama kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo.
23Kisha hizo siku saba za sikukuu hii amtolee Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, ni ndama saba wa kiume na madume saba ya kondoo wasio na kilema, kila siku hizo siku saba, tena kila siku dume la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo.[#4 Mose 28:19-22.]
24Tena sharti atolee kila ndama frasila moja ya unga kuwa kilaji cha tambiko, hata kila dume la kondoo vilevile, pamoja na pishi moja na nusu ya mafuta kwa kila frasila ya unga.[#Ez. 46:5; 4 Mose 15:4,6,9.]
25Siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, kwa kuwa ni sikukuu ya Vibanda, afanye vivyo hivyo siku zake saba, akitoa ng'ombe za tambiko za weuo na za kuteketezwa nzima na vilaji vya tambiko pamoja na mafuta.[#3 Mose 23:34.]