The chat will start when you send the first message.
1Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Lango la ua wa ndani lielekealo maawioni kwa jua sharti liwe limefungwa siku sita za kazi, lakini siku ya mapumziko lifunguliwe, hata siku ya mwandamo wa mwezi lifunguliwe.
2Mkuu akiingia penye ukumbi wa hilo lango toka nje, asimame hapo penye mhimili wa hilo lango, watambikaji waitengeneze ng'ombe yake ya tambiko ya kuteketezwa nzima nazo ng'ombe za tambiko za kushukuru, naye amwangukie Mungu penye kizingiti cha hilo lango, kisha atoke; kisha lango hilo lisifungwe mpaka jioni.[#Ez. 44:3.]
3Nao watu wa nchi hii wamwangukie Bwana hapo pa kuliingilia hilo lango siku za mapumziko na za miandamo ya mwezi.
4Nazo ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, mkuu atakazomtolea Bwana siku za mapumziko, ziwe wana kondoo sita wasio na kilema na dume mmoja asiye na kilema.[#4 Mose 28:9.]
5Tena kilaji cha tambiko kiwe frasila moja ya unga kwa yule dume, lakini kwa wana kondoo kiwe, kama mkono wake utakavyotoa, tena pishi moja na nusu ya mafuta kwa kila frasila moja ya unga.
6Siku ya mwandamo wa mwezi atatoa ndama ya ng'ombe ya kiume asiye na kilema na wana kondoo sita na dume moja, wote sharti wawe pasipo kilema.
7Frasila moja ya unga kwa yule ndama, tena frasila moja ya yule dume la kondoo iwe kilaji cha tambiko, nacho cha wana kondoo kiwe, kama mkono wake utakavyoleta, tena kwa kila frasila ya unga pishi moja na nusu ya mafuta.[#Ez. 45:24.]
8Mkuu akiingia aingie kwa njia ya ukumbi wa hilo lango, hata kutoka atoke kwa njia hiyohiyo.
9Lakini watu wa nchi hii wakimtokea Bwana kumwangukia penye mikutano ya sikukuu, wao walioingia katika lango la kaskazini sharti watoke penye lango la kusini, nao walioingia katika lango la kusini sharti watoke penye lango la kaskazini, mtu asirudi kwa njia ya lango lile, aliloliingia, ila atoke kwa lile la ng'ambo.
10Naye mkuu ataingia pamoja nao, wakiingia, kisha atatoka, nao wakitoka.
11Penye sikukuu napo penye mikutano ya sikukuu kilaji cha tambiko kiwe frasila moja ya unga kwa kila ndama, vilevile frasila moja ya unga kwa kila dume la kondoo, lakini kwa wana kondoo kiwe, kama mkono wake utakavyotoa, tena pishi moja na nusu ya mafuta kwa kila frasila moja ya unga.[#Ez. 46:7.]
12Kama mkuu anataka kumtolea Bwana kwa kupenda mwenyewe ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima au za kushukuru, basi, wamfungulie lile lango lielekealo maawioni kwa jua, azitoe ng'ombe zake za tambiko za kuteketezwa nzima nazo za kushukuru, kama anavyofanya siku za mapumziko, kisha atoke! Akiisha kutoka, na walifunge hilo lango.
13Nawe umtolee Bwana kila siku mwana kondoo wa mwaka mmoja asiye na kilema kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, ufanye hivyo kila kutakapokucha![#4 Mose 28:3.]
14Hata kilaji cha tambiko sharti ukitoe kila kutakapokucha, kiwe pishi moja ya unga na vibaba viwili vya mafuta ya kumiminiwa katika huo unga uliopepetwa vizuri. Hiki kilaji cha tambiko cha Bwana kimeagizwa cha siku zote za kale na kale.
15Sharti mtoe mwana kondoo nacho hicho kilaji cha tambiko pamoja na mafuta yake kila kutakapokucha kale na kale.
16Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kama mkuu anampa mmoja wao wanawe fungu la nchi yake, litakuwa lao hata wanawe, walishike, liwe fungu lao, walilolipata.
17Lakini kama anampa mmoja wao watumishi wake fungu la nchi yake, aliyoipata, litakuwa lake mpaka mwaka mkuu wa ukombozi; ndipo, litakaporudi kwake mkuu; ni wanawe tu watakaokaa na fungu lake, liwe lao.[#3 Mose 25:10.]
18Tena mkuu asichukue fungu lililo la watu akiwakorofisha na kuwafukuza kwao. Lililo lake ni fungu lile tu, alilopewa kulishika, liwe lake, nalo ndilo, atakaloachia wanawe, kusudi walio ukoo wangu wasitawanyike, mtu akiweza kuondolewa katika fungu, alilolishika, liwe lake.[#Ez. 45:8-9.]
19Akanipeleka hapo pa kuingia palipokuwa kando ya lile lango la kuviingilia vile vyumba vitakatifu vya watambikaji vielekeavyo kaskazini; hapo nikaona mahali pembeni panapoelekea baharini.
20Akaniambia: Humu ndimo, watambikaji wanamopikia nyama za ng'ombe za tambiko za upozi nazo za weuo, tena ndimo, wanamochomea vilaji vya tambiko, kusudi wasivipeleke katika ua wa nje na kuwapatia watu utakatifu.
21Kisha akanitoa na kunipeleka katika ua wa nje, akanipitisha penye pembe zake nne za huo ua; ndipo, nilipoona penye kila pembe ya huo ua ua mwingine.
22Penye pembe zote nne za huo ua palikuwa na nyua zilizofungwa kwa ukuta, urefu wao ulikuwa mikono 40, nao upana 30, kipimo chao hizo nyua ni kimoja tu.
23Zote nne zilizungukwa na ukuta wa mawe; chini penye hizo kuta kuzizunguka zote palikuwa pametengenezwa majiko.
24Akaniambia: Hizi ndizo nyumba za wapishi, watumishi wa Nyumba hii walimopikia nyama za ng'ombe za tambiko za watu.