Ezekieli 47

Ezekieli 47

Kijito cha mbaraka kilichotoka Patakatifu.

1Akanirudisha penye kuiingilia Nyumba hii, mara nikaona maji yaliyotoka chini ya kizingiti cha Nyumba hii kwenda upande wa maawioni kwa jua, kwani upande wa mbele wa Nyumba hii ulielekea maawioni kwa jua; nayo hayo maji yakachuruzika chini ya upande wa kuumeni wa Nyumba hii, kusini penye meza ya kutambikia.[#Yoe. 3:18; Zak. 14:8; Ufu. 22:1.]

2Akanitoa kwa njia ya lango la kaskazini, akanizungusha huko nje kwenda kwenye lango la nje lielekealo maawioni kwa jua, mara nikaona maji yaliyotiririka upande wake wa kuumeni.

3Yule mtu akatoka kwenda maawioni kwa jua akishika kamba ya kupimia mkononi, akapima mikono elfu, akanipitisha humo majini, yakafika penye viwiko vya miguu.[#Ez. 40:3.]

4Akapima elfu tena, akanipitisha humo majini, yakafika magotini; akapima elfu tena, akanipitisha humo majini, yakafika viunoni.

5Akapima elfu tena, yakawa mto, nami sikuweza kuupita, kwani maji yalikuwa yameingilia ndani sana, yakawa maji ya kuogelea, basi, yalikuwa mto usiopitika.

6Akaniuliza: umeona, mwana wa mtu? Kisha akanirudisha, nikienda kwa miguu kandokando ya mto.

7Niliporudi mara nikaona ukingoni penye mto huo miti mingi sana huku na huko.

8Akaniambia: Maji hayo yanatoka hapa kwenda katika nchi zilizoko upande wa maawioni kwa jua, yanashuka kwenda nyikani, yafike baharini. Tena hapo yatakapoingia baharini, yale maji ya huko yataonekana, ya kuwa yamegeuka kuwa mazuri.[#1 Mose 14:3.]

9Ndipo, itakapokuwa, vinyama vyote vitambaavyo hapo po pote, maji ya mto huo yatakapofika, vitapata uzima, nao samaki watakuwa hapo wengi sana, kwani maji haya yatafika hapo; ndipo, watakapopona na kupata kuwapo po pote, mto huu utakapofika.

10Ndipo, wavuvi watakaposimama pwani pake toka En-Gedi (Chemchemi ya Wana mbuzi) mpaka En-Egilemu (Chemchemi ya Ndama), maana patakuwa mahali pa kuanikia nyavu; samaki wa hapo watakuwa wa namna zao, tena wengi sana kama samaki wa Bahari Kubwa.

11Lakini mabwawa na maziwa yaliyoko kando yake maji yao hayatageuzwa kuwa mazuri, yatatumiwa ya chumvi.

12Kando ya mto huu pande zake za huku na za huko patakuwa na miti yo yote ifaayo kuliwa, majani yao hayatanyauka, wala matunda yao hayatakwisha. Kila mwezi yatazaa malimbuko tena, kwani maji yao yanatoka Patakatifu; kwa hiyo matunda yao yatatumiwa kuwa chakula, nayo majani yake yataponya watu.[#Ufu. 22:2.]

Mipaka ya nchi.

13Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Huu ndio mpaka wa nchi hiyo, mtakayojigawanyia kuwa mafungu yao yale mashina kumi na mawili ya Isiraeli, Yosefu tu apate mafungu mawili.[#1 Mose 48:5; Yos. 17:17.]

14Mtajigawanyia mafungu yaliyo sawasawa kwa kila mtu na ndugu yake, yawe yenu, kwa kuwa niliapa na kuuinua mkono wangu ya kwamba: Nitawapa baba zenu; kwa hiyo nchi hii itawaangukia kuwa mafungu yenu.

15Nao huu ndio mpaka wa nchi hiyo: upande wa kaskazini toka kwenye Bahari Kubwa unakwenda Hetiloni kufika Sedadi,[#4 Mose 34:2-12.]

16Hamati, Berota, Siburemu ulioko katikati ya mpaka wa Damasko na mpaka wa Hamati na Haseri wa kati ulioko kwenye mpaka wa Haurani.

17Ndivyo, mpaka utakavyotoka baharini kwenda mpaka Hasari-Enoni, mpaka wa Damasko uwe upande wa kaskazini, nao mpaka wa Hamati ukae kaskazini. Huu ndio mpaka wa kaskazini.

18Nao mpaka wa maawioni kwa jua uufuate mto wa Yordani toka Damasko na Haurani, tena toka Gileadi na nchi ya Isiraeli; huu mpaka mwupime toka hapo hata bahari ya maawioni kwa jua, uwe mpaka wa maawioni kwa jua.

19Nao upande wa kusini uelekeao kwenye jua kali uanzie Tamari kwenda Kadesi kwenye Maji ya Magomvi, kisha ufuate ule mto unaoingia katika Bahari Kubwa; huu ndio mpaka wa kusini uelekeao kwenye jua kali.[#4 Mose 20:13; 34:5.]

20Nao upande wa baharini mpaka ni Bahari Kubwa toka hapo kufika ng'ambo ya Hamati; huu ndio mpaka wa upande wa baharini.

21Nchi mtajigawanyia kwa mashina ya Isiraeli.

22Hapo, mtakapoipigia kura za kujipatia mafungu yatakayokuwa yenu, sharti mwapatie nao wageni wakaao kwenu katikati waliozaa wana katikati yenu. Nao watakuwa kwenu kama wazalia waliomo miongoni mwa wana wa Isiraeli; kwa hiyo sharti wapigiwe kura pamoja nanyi za kujipatia mafungu yatakayokuwa yao katikati ya mashina ya Waisiraeli.[#2 Mose 22:21.]

23Kwa shina lilelile, mgeni atakakokaa, ndiko, mtakakompa fungu, liwe lake. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania