Ezekieli 48

Ezekieli 48

Jinsi watakavyojigawanyia nchi yao.

1Haya ndiyo majina ya mashina: upande wa kaskazini kandokando ya njia ya Hetiloni kufika Hamati hata Hasari-Enani penye mpaka wa Damasko upande wa kaskazini kandokando ya Hamati ndiko kutakakokuwa fungu moja, la Dani toka upande wa maawioni kwa jua hata baharini.[#Ez. 47:15,17.]

2Kwenye mpaka wa Dani toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Aseri.

3Kwenye mpaka wa Aseri toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Nafutali.

4Kwenye mpaka wa Nafutali toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Manase.

5Kwenye mpaka wa Manase toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Efuraimu.

6Kwenye mpaka wa Efuraimu toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Rubeni.

7Kwenye mpaka wa Rubeni toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Yuda.

8Kwenye mpaka wa Yuda toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini kuwe fungu la kueuliwa, mtakalolitoa; upana wake uwe mianzi 25000, tena urefu uwe kama fungu moja jingine toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini; tena huko katikati kuwe na Patakatifu![#Ez. 45:1-8.]

9Hata fungu la kueuliwa sharti mmtolee Bwana, urefu wake uwe mianzi 25000, tena upana wake uwe mianzi 10000.

10Hilo fungu takatifu litakuwa lao watambikaji, wapate mahali penye kaskazini, urefu wake uwe mianzi 25000, nako upande wa baharini upana uwe mianzi 10000, nako upande wa maawioni kwa jua upana uwe mianzi 10000, tena kusini urefu uwe mianzi 25000, nako huko katikati kuwe na Patakatifu pa Bwana.

11Fungu hilo liwe lao watambikaji waliotakaswa, walio wana wa Sadoki, walioyaangalia, niliyowaambia, wayaangalie; ndio wasiopotea hapo, wana wa Isiraeli walipopotea, kama Walawi walivyopotea.[#Ez. 44:15.]

12Kwa hiyo hapo patakuwa fungu lao, ni kipande cha lile fungu la kueuliwa lililo nchi takatifu yenyewe kwenye mpaka wa Walawi.

13Tena Walawi wapate kandokando ya mpaka wa watambikaji mahali penye urefu wa mianzi 25000, nao upana uwe mianzi 10000; urefu wote uwe mianzi 25000, nao upana wote uwe mianzi 10000.

14Lakini nchi hiyo wasiiuze kipande tu, wala wasiibadili kipande kwa nchi nyingine, kusudi nchi hii iliyo ya kwanza kwa uzuri wasiitie mikononi mwa mwingine, kwani ni nchi takatifu ya Bwana.

15Yale 5000 yatakayosalia kwa upana wa mianzi wa 25000 yawe mali ya huo mji wote, watu wapate pa kukaa na pa kulisha, huo mji wenyewe ukiwa katikati.

16Vipimo vyake viwe hivyo: upande wa kaskazini mianzi 4500, upande wa kusini mianzi 4500, upande wa maawioni kwa jua mianzi 4500, upande wa baharini mianzi 4500.[#Ufu. 21:16.]

17Mahali pa mji pa kulisha pawe upande wa kaskazini mianzi 250, upande wa kusini mianzi 250, upande wa maawioni kwa jua mianzi 250, nako upande wa baharini mianzi 250.

18Kisha patasalia kwa urefu kandokando ya lile fungu takatifu la kueuliwa mahali penye mianzi 10000 kuelekea maawioni kwa jua, na mianzi 10000 kuelekea baharini, ndipo kandokando ya lile fungu takatifu la kueuliwa; mahali hapo mazao yake yaliwe nao watumikiao mle mjini.

19Hao watumikiao mle mjini watakuwa wa mashina yote ya Isiraeli, nao ndio watakaopalima hapo.

20Fungu lote la kueuliwa, mtakalolitoa, liwe mianzi 25000 kwa pande zote nne, ndipo patakapokuwa fungu takatifu la kueuliwa pamoja na hilo fungu litakalokuwa lake huo mji.

21Patakaposalia patakuwa pake mkuu upande wa huku na upande wa huko penye lile fungu takatifu la kueuliwa na penye lile fungu litakalokuwa lake huo mji kuifuata ile mianzi 25000 ya hilo fungu la kueuliwa mpakani kwenda upande wa maawioni kwa jua na upande wa baharini vilevile kuifuata ile mianzi 25000 kwenye mpaka uelekeao baharini sawasawa na mafungu mengine; hapo patakuwa pake mkuu. Hilo fungu takatifu la kueuliwa pamoja na Nyumba Takatifu itakuwa hapo katikati.[#Ez. 45:7.]

22Fungu lao Walawi nalo fungu lake mji, yote mawili yatakuwa katikati katika fungu lake mkuu; hilo fungu lake litakuwa katikati kwenye mpaka wa Yuda na kwenye mpaka wa Benyamini.

23Nayo mashina yaliyosalia mafungu yao ni haya: toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Benyamini.

24Kwenye mpaka wa Benyamini toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Simeoni.

25Kwenye mpaka wa Simeoni toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Isakari.

26Kwenye mpaka wa Isakari toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Zebuluni.

27Kwenye mpaka wa Zebuluni toka upande wa maawioni kwa jua hata upande wa baharini ni fungu moja, la Gadi.

28Kisha mpaka wa Gadi upande wa kusini uelekeao kwenye jua kali utoke Tamari, ufike Kadesi penye Maji ya Magomvi, kisha ufuate mto kufika kwenye Bahari Kubwa.[#Ez. 47:19.]

29Hizo ndizo nchi, mtakazoyagawanyia mashina ya Isiraeli kwa kupiga kura kuwapatia mafungu yatakayokuwa yao. Hayo ndiyo mafungu yao makuu; ndivyo asemavyo Bwana Mungu.

Majina ya malango ya Yerusalemu

30Pa kutokea mle mjini patakuwa hivyo: upande wa kaskazini utakuwa wa mianzi 4500.

31Nayo malango ya mji yataitwa kwa majina ya mashina ya Isiraeli. Malango matatu yataelekea kaskazini: lango moja la Rubeni, lango moja la Yuda, lango moja la Lawi.[#Ufu. 21:12-13.]

32Nao upande wa maawioni kwa jua utakuwa wa mianzi 4500, nao utakuwa na malango matatu: lango moja la Yosefu, lango moja la Benyamini, lango moja la Dani.

33Nao upande wa kusini utakuwa wa mianzi 4500, nao utakuwa na malango matatu: lango moja la Simeoni, lango moja la Isakari, lango moja la Zebuluni.

34Nao upande wa baharini utakuwa wa mianzi 4500, nao utakuwa na malango matatu: lango moja la Gadi, lango moja la Aseri, lango moja la Nafutali.

35Kuuzunguka mji wote itakuwa njia yenye urefu wa mianzi 18000. Jina lake huo mji litakuwa toka siku ile: Bwana yumo.[#Ez. 43:7; Ufu. 21:3.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania