Ezekieli 5

Ezekieli 5

Mapatilizo ya mji wa Yerusalemu.

1Nawe mwana wa mtu, jipatie upanga mkali, uutumie kuwa wembe wa kinyozi wa kunyolea kichwa chako na udevu wako! Kisha jipatie mizani, uzigawanye hizo nywele!

2Fungu la tatu uliteketeze kwa moto mjini katikati, siku za kusongwa zitakapomalizika! Fungu la tatu jingine lichukue, ulitapanye na kupigapiga kwa upanga ukizunguka mjini po pote! Nalo fungu la tatu jingine utalitupatupa kwenye upepo, nami nitauchomoa upanga, uzifuata nyuma.

3Nawe hizo nywele zichukue chache tu, uzifungue pembeni katika vazi lako!

4Namo uchukue tena kidogo, uzitupe penye ule moto unaowaka mjini katikati, uziteketeze mle motoni! Ndimo, utakamotoka moto wa kuula mlango wote wa Isiraeli.

5Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Huu ndio Yerusalemu! Nimeuweka kwenye wamizimu katikati, ukazungukwa na nchi zao.

6Lakini kwa kuwa haukunicha, uliyakataa mashauri yangu kuliko hao wamizimu, ukayakataa nayo maongozi yangu kuliko hizo nchi ziuzungukazo, kwani mashauri yangu wakayabeua, hawakuyafuata maongozi yangu.

7Kwa sababu hii Bwana Mungu anasema hivi: Kwa kuwa mnafanya matata kuliko wamizimu wanaowazunguka, msipoyafuata maongozi yangu, wala msipoyafanya mashauri yangu, wala msipoyafanya maamuzi yangu, wamizimu wawazungukao wanayoyafanya,

8kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Utaniona, mimi nami nikikujia, nifanye katikati yako mashauri machoni pa wamizimu.

9Nitakufanyizia mambo, nisiyoyafanya bado, wala sitayafanya mara nyingine yaliyo hivyo kwa ajili ya machukizo yako yote.

10Nayo ni haya: katikati yako baba watakula wana, nao wana watakula baba zao! Haya ndiyo mashauri, nitakayokufanyizia, kisha masao yako nitayatupiatupia pande zote za upepo.[#5 Mose 28:53-55; Omb. 4:10.]

11Kweli ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Hivyo nilivyo Mwenye uzima, kwa kuwa umepachafua Patakatifu pangu kwa matapisho yako yote na kwa machukizo yako yote, kwa hiyo mimi nami nitaliondoa jicho langu, lisikuonee uchungu, nami mwenyewe sitakuhurumia.[#Ez. 8:6-18.]

12Fungu lako la tatu watakufa kwa magonjwa mabaya wakizimia kwa njaa katikati yako, fungu la tatu jingine watauawa kwa panga kwenye pande zako zote; fungu la tatu jingine nitawatupiatupia pande zote za upepo, kisha nitauchomoa upanga, uwafuate.[#Ez. 5:2.]

13Hivyo makali yangu yatakwisha, hivyo nitayapoza machafuko yangu yenye moto kwao nikiwalipisha. Ndipo, watakapotambua, ya kuwa mimi Bwana nimesema kwa wivu wangu, nikawatimilizia machafuko yangu yenye moto.[#Ez. 16:42.]

14Kisha nitakugeuza kuwa mabomoko ya kuzomelewa kwa wamizimu wote wakuzungukao, kila atakayepapita ayaone.

15Hivyo itakuwa, uwe wa kuzomelewa na wa kufyozwa, tena uwe kitisho cha kuwashangaza wamizimu wakuzungukao, nitakapokufanyizia mashauri na kukutolea makali na machafuko yenye moto na mapigo yenye moto. Mimi Bwana nimeyasema.[#Yer. 24:9.]

16Ndipo, nitakapowapigia mishale mibaya ya njaa ya kuangamiza; hiyo ndiyo, nitakayoipiga kweli, iwaangamize ninyi, nitakapoizidisha njaa na kulivunja kabis shikizo lenu la chakula.[#Ez. 4:16; 5 Mose 32:23.]

17Pamoja na hiyo njaa nitawapelekea nyama wabaya, wawaue watoto wako, nayo magonjwa mabaya ya kuozesha damu yatapita kwako, kisha nitaleta nazo panga na kukuua. Mimi Bwana nimeyasema.[#Ez. 14:21.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania