Waebureo 3

Waebureo 3

Kristo ni mkubwa kuliko Mose.

1Kwa hiyo, ndugu zangu watakatifu, mlioitwa kama sisi na mwito utokao mbinguni, yaelekezeni macho kwake Yesu, tunayemwungama kuwa mtume na mtambikaji mkuu![#Ebr. 4:14.]

2Naye aliyempa kazi hiyo alimtumikia kwa welekevu, kama Mose alivyotumika katika nyumba yake yote.[#4 Mose 12:7.]

3Lakini huyu amepaswa kutukuzwa kuliko Mose; ni vivyo hivyo kama vya nyumba; mwenye kuijenga hupata cheo kuliko ile nyumba yenyewe,

4kwani kila nyumba hujengwa na mtu. Lakini anayevitengeneza vyote ndiye Mungu.

5Naye Mose alitumika kwa welekevu katika nyumba yake yote kama mtumishi; hivyo aliyashuhudia yale yatakayosemwa.

6Lakini Kristo alitumika kama mwana aliye mwenye nyumba yake. Nayo nyumba yake ni sisi, tunapoikaza mioyo yetu, ichangamke, tena tunapofuliza kujivunia kingojeo chetu mpaka mwisho.[#Ef. 2:19; 1 Petr. 2:5.]

Msiishupaze mioyo yenu vibaya!

7Kwa hiyo fanyeni, kama Roho Mtakatifu anavyosema:

Leo, mtakapoisikia sauti yake,

8msiishupaze mioyo yenu,

kama hapo, mioyo ilipokuwa yenye uchungu,

siku ile ya kujaribiwa kule nyikani.

9Ndipo, baba zenu waliponijaribu na kunipima,

tena walikuwa wameyaona matendo yangu miaka arobaini.

10Nikachafuliwa moyo nao wa kizazi hicho, nikasema:

Siku zote hupotea njia mioyoni mwao;

lakini hawakuzitambua njia zangu.

11Kwa hiyo nilijiapia kwa makali yangu kwamba:

Hawataingia kamwe kwenye kituo changu!

12Tazameni, ndugu, pasiwe mmoja wenu mwenye moyo mbaya usiomtegemea Mungu, ukijitenga kwake yeye aliye Mwenye uzima!

13Ila mwonyane wenyewe siku kwa siku, pangali pakiitwa leo, kusudi kwenu kusipatikane mwenye moyo mgumu uliodanganywa na ukosaji![#1 Tes. 5:11.]

14Kwani tumekwisha kuwa wenziwe Kristo, tunapokishika kingojeo chetu cha kwanza, kisitupotelee mpaka mwisho.[#Ebr. 6:11.]

15Paliposemwa:

Leo, mtakapoisikia sauti yake, msiishupaze mioyo yenu

kama hapo, mioyo ilipokuwa yenye uchungu!

16Hapo walioyasikia na kupata mioyo yenye uchungu walikuwa akina nani? Sio hao wote waliotoka Misri wakiongozwa na Mose?

17Tena ni akina nani waliochafua moyo wake miaka 40? Sio hao waliokosa, wao waliokufa nyikani, miili yao ikiachwa hapohapo?[#1 Kor. 10:10.]

18Tena ni akina nani, aliowaapia kwamba:

Hawataingia kamwe kwenye kituo chake,

wasipokuwa wale waliokataa kutii?

19Nasi twaona, ya kuwa hawakuweza kuingia, kwa sababu hawakumtegemea.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania