Waebureo 5

Waebureo 5

Utambikaji wa Kristo.

1Kwani kila mtambikaji mkuu anayechaguliwa katika watu huwekwa kwa ajili ya watu, awafanyizie kazi kwake Mungu akimtolea matoleo na vipaji vya tambiko kwa ajili ya makosa yao.

2Huyu anaweza kuwavumilia kidogo wasiojua maana, wakipotezwa, kwa sababu hata yeye ni mwenye unyonge.[#Ebr. 4:15.]

3Kwa ajili yake huo hana budi kujipatia mwenyewe kole ya makosa yake yeye vivyo hivyo, kama anavyowapatia watu.[#3 Mose 9:7; 16.]

4Wala hakuna ajipaye mwenyewe cheo hiki, ila huitwa na Mungu, kama naye Haroni alivyoitwa.[#2 Mose 28:1.]

5Vivyo naye Kristo hakujipa utukufu mwenyewe kuwa mtambikaji mkuu, ila ni yeye aliyemwambia:

Wewe ndiwe Mwanangu, siku hii ya leo mimi nimekuzaa.

6Ndivyo anavyosema hata pengine:

Wewe u mtambikaji wa kale na kale,

kama Melkisedeki alivyokuwa.

7Naye siku zile allikuwapo mwenye mwili wa kimtu, akamwomba na kumbembeleza yule aliyeweza kumwokoa katika kufa. Alipokaza kumlalamikia na kutoa machozi akasikiwa naye, kwa sababu alimcha Mungu.[#Mat. 26:39-46; Luk. 22:41-44.]

8Naye angawa Mwana, lakini katika kuteswa ndimo, alimojifunzia kutii.[#Fil. 2:8.]

9Tena hapo, mambo yake yalipotimilika, akawapatia wote wamtiio wokovu wa kale na kale.[#Yoh. 17:1,5.]

10Kwa hiyo alipewa na Mungu jina la mtambikaji mkuu, kama Melkisedeki alivyokuwa.[#Ebr. 7.]

Maziwa na chakula.

11Hapo tunayo maneno mengi ya kusema, lakini ni magumu ya kuyaeleza vema, nanyi mmekuwa wavivu wa kusikia.

12Kwani tukizipima siku, mlizofundishwa, msingekuwa na budi kuwa wafunzi; lakini mwapaswa, mtu aanze tena kuwafundisha, maneno ya Mungu yalivyoanza; maana yawafaliayo ni maziwa, vyakula vigumu sivyo.[#1 Kor. 3:1-3.]

13Kwani kila anayenyonyeshwa maziwa ni mtu asiyejua bado yaongokayo, kwani ni mtoto mchanga.[#Ef. 4:14.]

14Lakini walio watu wazima hilishwa vyakula vigumu; kwani hao wameizoeza mioyo yao kujua maana, kwa hiyo hupambanua yaliyo mazuri nayo yaliyo maovu.[#Rom. 16:19; Fil. 1:10.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania