The chat will start when you send the first message.
1Kwani huyo Melkisedeki alikuwa mfalme wa Salemu na mtambikaji wa Mungu alioko mbinguni juu. Hapo Aburahamu aliporudi na kutoka katika vita vya wafalme, alimwendea, akampongeza.[#1 Mose 14:18-20.]
2Naye Aburahamu akamgawia fungu la kumi la mali zote. Maana ya jina lake kwanza ni kwamba: Mfalme wa wongofu; tena ni kwamba: Mfalme wa Salemu, ndio mfalme wa utengemano.
3Baba yake na mama yake nao wakale wake hawajuliki, wala siku zake za kuishi hazijuliki, zilipoanzia, wala zilipokomea, maana amefananishwa na Mwana wa Mungu, ni mtambikaji wa kale na kale.[#Yoh. 7:27.]
4Lakini tazameni, huyo alivyokuwa, baba yetu mkuu Aburahamu akimpa fungu la kumi la mateka!
5Kweli nao wana wa Lawi waliopewa utambikaji waliagizwa na Maonyo kuwatoza fungu la kumi wenzao wa ukoo walio ndugu zao, tena ndio waliotoka pamoja nao kiunoni mwa Aburahamu.[#4 Mose 18:21.]
6Lakini yule asiyekuwa wa ukoo wao alimtoza Aburahamu fungu la kumi, akampongeza yule aliyekuwa mwenye kiagio.
7Lakini hili halibishiki kwamba: Kilicho kidogo hupongezwa nacho kilicho kikubwa.
8Napo hapo watu walio wenye kufa hutoza fungu la kumi; lakini alilitoza mtu anayeshuhudiwa kwamba: Anaishi.
9Tena, ikiwezekana kusema hivyo, katika Aburahamu hata Lawi aliye mwenye kutoza fungu la kumi alitozwa naye fungu la kumi.
10Kwani alikuwa kiunoni mwa babu yake, Melkisedeki alipokutana naye.
11Kama utambikaji wa Kilawi ungaliyatimiza yote, (kwani hapo, ulipokuwapo, watu walipewa Maonyo), ni kwa sababu gani tena ikisemwa: Sharti painuke mtambikaji mwingine, kama Melkisedeki alivyokuwa, isiposemwa: Kama Haroni alivyokuwa?[#Ebr. 7:18-19; Sh. 110:4.]
12Kwani utambikaji unapogeuzwa, hapo sharti Maonyo nayo yageuke.
13Kwani yule aliyesemwa yale maneno alikuwa wa shina jingine, ambalo hakutoka kwake mtu ye yote aliyefanya kazi ya utambikaji.[#Sh. 110:4.]
14Kwani hujulikana: Bwana wetu alitoka katika shina la Yuda, nalo shina hilo Mose hakuliambia hata neno moja la utambikaji.[#1 Mose 49:10; Yes. 11:1.]
15Tena huelekea kabisa: Pakiinuka mtambikaji mwingine anayefanana na Melkisedeki,
16yeye utambikaji wake haukutoka kwenye Maonyo yaagizayo mambo ya kimtu, ila umetoka kwenye nguvu ya uzima usiolegezeka.
17Kwani unashuhudiwa kwamba:
Wewe u mtambikaji wa kale na kale,
kama Melkisedeki alivyokuwa.
18Hivyo lile agizo la kale linatanguka, kwa sababu lilikuwa nyonge, tena halikufaa;
19kwani hakuna lililotimizwa na Maonyo. Lakini mahali pake paliingizwa kingojeo kilicho kikuu kuyapita Maonyo, maana kinatufikisha kwake Mungu.[#Ebr. 9:9.]
20Tena hivi havikufanyika pasipo kiapo: kwani wale wengine waliupata utambikaji pasipo kiapo,
21lakini huyu aliupata, yeye Mungu akiapa na kujitaja alipomwambia:[#Sh. 110:4.]
Bwana aliapa, naye hatajuta:
Wewe u mtambikaji wa kale na kale.
22Hivyo Yesu ni mtimizaji wa agano lililo kuu kulipita lile.[#Ebr. 8:6; 12:24.]
23Nao wale ni wengi waliokuwa watambikaji, kwa sababu kufa kuliwazuia, wasikae.
24Lakini huyu anao utambikaji usiopokezanwa, kwa sababu anakaa kale na kale.
25Kwa hiyo anaweza kuwaokoa kale na kale wanaomjia Mungu na kumfuata yeye; kwani yeye anaishi siku zote, apate kuwaombea.[#Rom. 8:34; 1 Yoh. 2:1.]
26Kwani mtambikaji mkuu, ambaye tunapaswa naye, ni yule mcha Mungu, asiye mwovu, asiye mwenye madoa, aliyetengeka na wakosaji, alioko juu kuliko mbingu.[#Ebr. 4:14.]
27Hapaswi kama wale watambikaji wakuu, kila siku kwanza kujipatia yeye kole ya makosa yake mwenyewe, kisha kuwapatia watu nao kole ya makosa yao. Kwani huyu amevifanya hivyo mara moja hapo alipojitoa mwenyewe kuwa kole.[#3 Mose 16:6,15.]
28Kwani Maonyo huweka watu wenye unyonge kuwa watambikaji wakuu. Lakini neno la kiapo kilichoyafuata Maonyo nyuma linamweka Mwana kuwa mtambikaji mtimilifu wa kale na kale.[#Ebr. 5:1-2.]