Hosea 14

Hosea 14

1Samaria atalipishwa manza, alizozikora kwa kumpingia

Mungu wake: kwa hiyo wataangushwa kwa panga,

watoto wao wachanga watapondwa,

nao wanawake wenye mimba watatumbuliwa.

Mema yatakayokuwa, Waisiraeli watakapomgeukia Mungu.

2Rudi, Isiraeli, kwa Bwana Mungu wako!

Kwani umejikwaa kwa maovu, uliyoyafanya.

3Yashikeni maneno haya kwenda nayo,

mkirudi kwake Bwana, ya kumwambia:

Ziondoe manza zote pia, tulizozikora, ututolee wema!

Ndipo, tutakapotoa shukrani za midomo yetu, ziwe ng'ombe za tambiko.

4Mwasuri hawezi kutuokoa, nasi hatujui kupanda farasi;

hatutaziita tena kazi za mikono yetu kwamba: Ni mungu wetu!

Kwani kwako ndiko, wafiwao na wazazi wanakojipatia huruma.

5Watakaporudi hivyo, nitawaponya, nitawapenda kwa moyo,

kwani ndipo, makali yangu yatakapokuwa yamewaondokea.

6Ndipo, nitakapokuwa kwake Isiraeli kama umande,

apate kuchanua kama maua ya shambani,

ashushe mizizi yake kama miti ya Libanoni.

7Matawi yake yatakuwa marefu, uzuri wake uwe kama wa

mchekele,

nao utanuka vizuri kama mti wa Libanoni.

8Watakaokaa kivulini kwake watarudia kupanda ngano,

watachanua kama mizabibu,

sifa yao itakuwa kama sifa ya mvinyo za Libanoni.

9Ndipo, Efuraimu atakaposema: Vinyago vinanifaliaje

tena?

Nami nitamjibu na kumtazama kwa kupendezwa:

Mimi ni kama mvinje mbichi,

kwangu mimi kutaonekana yaliyo mazao yako.

10Yuko nani aliye mwerevu wa kweli, ayatambue hayo?

Yuko nani aliye mtambuzi, ayajue maana yao hayo?

Kwani njia za Bwana hunyoka, nao waongofu huzishika,

lakini wapotovu

hukwazwa nazo.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania