Yakobo 2

Yakobo 2

Mpendane, lakini msipendelee!

1Ndugu zangu, msiwaze kwamba: Kumtegemea Bwana wetu mtukufu Yesu Kristo hupatana na kupendelea watu![#1 Kor. 2:8.]

2Ni hivyo: mle mkutaniamo mkiingia mtu mwenye pete za dhahabu vidoleni, aliyevaa mavazi mazuri, tena mkiingia hata maskini mwenye mavazi machakavu,

3nanyi mkamtazama yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia: Wewe kaa hapa pazuri! kisha mkamwambia yule maskini: Wewe simama huko au kaa hapa chini miguuni pangu!

4je? Hivyo mioyo yenu haikujiumbua kwamba: Mkiwagawanya hivyo mmefuata mawazo mabaya?

5Sikilizeni, ndugu zangu wapendwa! Mungu hakuwachagua walio maskini ulimwenguni, wawe wenye mali kwa kumtegemea, tena wautwae ufalme, aliowaagia wampendao, uwe urithi wao?[#Luk. 12:21; 1 Kor. 1:26.]

6Lakini ninyi mmemnyima maskini heshima. Wenye mali sio wanaowaendea ninyi kwa nguvu? Sio wanaowaburura bomani?

7Nao sio wanaolitukana lile Jina zuri, mwitwalo nalo?[#1 Petr. 4:14.]

8Kweli, mkilitimiza Agano la kifalme, kama lilivyoandikwa kwamba: Umpende mwenzio, kama unavyojipenda mwenyewe! mnafanya vizuri.[#3 Mose 19:18.]

9Lakini mkiwapendelea watu mnakosa, mkajulishwa na hilo agizo waziwazi kuwa wenye kulipita.[#5 Mose 1:17.]

10*Kwani mtu akiyashika Maonyo yote akalikosea moja tu, amekwisha kuyakosea yote.[#Mat. 5:19.]

11Kwani yeye aliyesema: Usizini! ndiye aliyesema: Usiue! Nawe usipozini, lakini unaua, basi, umekwisha kuwa mwenye kuyapita Maonyo.[#2 Mose 20:13-14.]

12Semeni, tena fanyeni hivyo, kama watu wafanyavyo watakaohukumiwa kwa Maonyo yanayotupatia kukombolewa![#Yak. 1:25.]

13Kwani mtu akosaye huruma atapata naye hukumu ikosayo huruma; lakini huruma hushangilia nako kwenye hukumu.[#Mat. 5:7; 18:30,34; 25:45,46.]

Kumtegemea Mungu pasipo matendo ni kwa bure.

14Ndugu zangu, mtu akisema: Niko na kumtegemea Mungu, lakini matendo hanayo, inamfaliaje? Kumtegemea Mungu kunaweza kumwokoa?[#Mat. 7:21.]

15Kwetu kukipatikana ndugu mume au mke walio wenye uchi na wenye kukosa chakula cha siku moja tu,

16mtu wa kwenu akawaambia: Nendeni na kutengemana, mwote moto, mpate kushiba! asiwape yaipasayo miili yao, itawafaliaje?[#1 Yoh. 3:17.]

17Hapo mwaona: Kumtegemea Mungu kusikoendelea na matendo yakupasayo kumekwisha kuangamika kwenyewe.*

18Labda yuko atakayesema: Wewe uko na kumtegemea Mungu, nami niko na matendo; nionyesha, unavyomtegemea Mungu pasipo matendo! kisha nami nitakuonyesha, matendo yangu yanavyotimilika katika kumtegemea Mungu.[#Gal. 5:6.]

19Wewe unaamini, ya kuwa Mungu ni mmoja tu? Ni vizuri; pepo nao huyaamini hayo, lakini hutetemeka![#Mat. 8:29.]

20Mtu mpuzi, unataka kutambua, ya kuwa kumtegemea Mungu kusikoendelea na matendo ni kwa bure?

21Baba yetu Aburahamu hakupata wongofu kwa matendo alipompeleka mwana wake Isaka, awe ng'ombe ya tambiko?[#1 Mose 22:9-10,12; Ebr. 11:17.]

22Unaona: Kumtegemea Mungu husaidiana na matendo yakupasayo; napo, alipofanya yampasayo, ndipo, kumtegemea Mungu kulipotimilika kwake,

23nayo yaliyoandikwa yakatimia kwamba:

Aburahamu alimtegemea Mungu,

kwa hiyo akawaziwa kuwa mwenye wongofu,

akaitwa mpenzi wake Mungu.

24Mnaona: Mtu hupata wongofu kwa matendo, siko kwa kumtegemea Mungu tu.

25Tena je? Yule mke mgoni Rahabu hakupata wongofu naye kwa matendo, alipowafikiza wale wajumbe na kuwatoa mjini kwa njia nyingine?[#Yos. 2:4,15; Ebr. 11:31.]

26Kwani kama mwili unavyokufa, usipopumua, vivyo hivyo nako kumtegemea Mungu kusikoendelea na matendo kunakufa.[#Yak. 2:17.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania