Yakobo 3

Yakobo 3

Makosa ya ulimi.

1Ndugu zangu, haifai, wengi wakiwa wafunzi. Jueni: hukumu, tutakayoipata sisi, itakuwa kuliko ya wengine!

2Kwani sisi sote hukosa mengi. Mtu asipokosa kwa kusema, huyo ni mume mtimilifu anayeweza kuuongoza hata mwili wote.

3Tazameni, farasi twawatia hatamu vinywani, watutii sisi; nasi hivyo huwaongoza miili yao yote kwenda huko, tunakopenda.

4Tazameni, hata merikebu zilivyo kubwa sana, tena zinavyochukuliwa na pepo zenye nguvu! Nazo huongozwa na sukani iliyo ndogo sana, mwenye kuishika anakotaka.

5Vivyo hivyo nao ulimi ni kiungo kidogo, nao hujivunia makuu! Tazameni, moto ulio mdogo huchoma pori kubwa!

6Nao ulimi ni moto, ni ulimwengu wenye upotovu. Katika viungo vyetu ndio ulimi unaouchafua mwili wote, unavichoma vyote vilivyoumbwa, wenyewe ukiwashwa na moto ulioko kuzimuni.[#Fano. 16:26-27; Mat. 12:36-37; 15:11,18-19.]

7Kwani nyama wo wote, kama nyama wa porini na ndege na nyoka na nyama wa baharini, wote hufugika, nao wamekwisha fugwa na nguvu za watu.

8Lakini huo ulimi hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu yenye kuua.[#Sh. 140:4.]

9Ndio, unaotutukuzisha Bwana aliye Baba, tena ndio, unaotuapizisha watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu.[#1 Mose 1:27.]

10Matukuzo na maapizo hutoka katika kinywa kilekile kimoja. Ndugu zangu, mambo haya hayapasi kuwa hivyo.

11Je? Iko chemchemi inayotoa maji matamu na machungu katika kisima kilekile kimoja?

12Ndugu zangu, uko mkuyu unaoweza kuzaa chikichi, au mzabibu unaoweza kuzaa kuyu? Napo penye chumvi hapatoki maji matamu.

Ujuzi utokao juu.

13Kwenu yuko nani aliye mwerevu wa kweli wa kujua mambo? Ajionyeshe kuwa mwenye mwenendo mzuri, nazo kazi zake zijulike kuwa zenye upole utokao katika huo werevu wa kweli![#Yak. 2:18.]

14Lakini mkiwa wenye wivu ulio na uchungu na wenye uchokozi mioyoni mwenu msijivune, wala yaliyo ya kweli msiyageuze kuwa uwongo![#Ef. 4:31.]

15Kwani werevu huu haukutoka mbinguni juu, ila nchini, ni wa kimtu na wa Kisatani.

16Kwani wivu na uchokozi ulipo, ndipo palipo penye matata na mambo maovu yo yote.[#Yak. 1:5,17; Rom. 16:19.]

17Lakini werevu wa kweli utokao mbinguni juu kwanza ni wenye ung'avu, kisha ni wenye utengemano na upole na unyenyekevu, huwahurumia wote na kuwapatia mazao mema; haupendelei, maana hukataa ujanja.

18Nalo tunda la kuzaa wongofu hupandwa nao wenye utengemano panapotengemana.[#Yes. 32:17; Mat. 5:9.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania