The chat will start when you send the first message.
1Magomvi yenu ya kupigana ninyi kwa ninyi yanatoka wapi? Sipo hapo, mzichezeapo tamaa zenu zinazoshindana katika viungo vyenu?[#1 Petr. 2:11.]
2Mwakifuata kijicho, lakini hampati; mwauana kwa wivu, lakini hamwezi kuyafikia, myatakayo; mwapigana na kugombana, lakini hamna kitu, kwa sababu hamwombi.
3Mngawa mwaomba, lakini hampewi, kwa sababu mwaomba vibaya, maana mwataka tu ya kutumia katika machezo yenu.
4Enyi wazinzi waume na wanawake, hamjui: kuupenda ulimwengu huu ni kuchukiwa naye Mungu? Anayetaka kuwa mpenzi wa ulimwengu huu, hugeuka kuwa mchukivu wa Mungu.[#Luk. 6:26; Rom. 8:7; 1 Yoh. 2:15.]
5Au mwawaza, ya kuwa Maandiko yanasema bure: Roho aliyekaa ndani yetu anataka sana kushindana na wivu?[#2 Mose 20:3,5; 34:14; Mat. 6:24; Rom. 8:14.]
6Nayo mema, atugawiayo, ni makubwa kuushinda. Kwa hiyo maandiko yasema:
Wenye kujikweza Mungu huwapingia,
lakini wanyenyekevu huwapatia huruma.
7Kwa hiyo mtiini Mungu! Satani mbisheni! Ndivyo, atakavyowakimbia.[#Ef. 6:12; 1 Petr. 5:8-9.]
8Mkaribieni Mungu! Ndivyo, atakavyowakaribia nanyi. Enyi wakosaji, ing'azeni mikono! Enyi wenye mioyo miwili, itakaseni mioyo![#Yes. 1:16; Zak. 1:3.]
9Jisumbueni na kusikitika na kuomboleza! Macheko yenu yageuke kuwa vilio, nazo furaha zenu zigeuke kuwa masikitiko![#Rom. 7:24.]
10Mjinyenyekeze mbele ya Bwana! Ndivyo, atakavyowakuza ninyi.[#1 Petr. 5:6.]
11Msitetane, ndugu! Anayemteta ndugu au anayemwumbua ndugu yake huyateta Maonyo na kuyaumbua Maonyo. Lakini ukiyaumbua hu mfanyaji wa Maonyo, ila muumbuzi.
12Mwenye kuyatoa Maonyo na mwenye kuhukumu ni mmoja, maana ni yeye anayeweza kuokoa na kuangamiza. Lakini wewe u nani ukimwumbua mwenzio?[#Mat. 7:1; Rom. 2:1; 14:4.]
13*Sasa tusemeane nanyi mnaosema: Leo au kesho tutakwenda mjini fulani, tukae huko mwaka mzima, tuchuuze na kuchuma![#Fano. 27:1.]
14Nanyi hamjui, itakayokuwa kesho. Kuishi kwenu ni kwa namna gani? Maana ninyi m kama mvuke unaoonekana kitambo kidogo, kisha hutoweka.[#Luk. 12:20.]
15Mngesema: Bwana akitaka, tutaishi, tufanye hivi na hivi.
16Lakini sasa mwajivunia kwa kujitutumua; majivuno yote yaliyo hivyo ni mabaya.[#Tume. 18:21.]
17Ajuaye kufanya mazuri, asiyafanye, amekwisha kukosa.*[#Luk. 12:47.]