The chat will start when you send the first message.
1Kulikuwa na fundi wa vita mwenye nguvu, ndiye Yefuta wa Gileadi; naye alikuwa mwana wa mwanamke mgoni, naye Gileadi ndiye aliyemzaa Yefuta.
2Naye mkewe Gileadi alikuwa amemzalia wana; hao wana wa huyu mwanamke walipokua wakamfukuza Yefuta wakimwambia: Haifai, ukipata urithi nyumbani mwa baba yetu, kwani wewe u mwana wa mwanamke mwingine.[#1 Mose 21:10.]
3Ndipo, Yefuta alipowakimbia ndugu zake, akakaa katika nchi ya Tobu, wakakusanyika kwake watu wasiokuwa na kitu cho chote, nao hutoka naye kwenda huko na huko.[#Amu. 9:4; 1 Sam. 22:2.]
4Siku zilipopita, wana wa Amoni wakaja kupigana na Waisiraeli.
5Ikawa, wana wa Amoni walipokuja kupigana na Waisiraeli, ndipo, wazee wa Gileadi walipokwenda kumchukua Yefuta katika nchi ya Tobu,
6wakamwambia Yefuta: Njoo, uwe kiongozi wetu, tupate kupigana na wana wa Amoni!
7Lakini Yefuta akawaambia wazee wa Gileadi: Je? Ninyi ham wachukivu wangu? Hamkunifukuza nyumbani mwa baba yangu? Mbona sasa mnaposongwa mwanijia mimi?
8Ndipo, wazee wa Gileadi walipomwambia Yefuta: Kweli ni kwa sababu hii, tukirudi kwako; sasa nenda pamoja na sisi, tupate kupigana na wana wa Amoni, nawe uwe kichwa chetu sisi sote tukaao Gileadi![#Amu. 10:18.]
9Naye Yefuta akawauliza wazee wa Gileadi: Mkinirudisha kwenu, nipigane nao wana wa Amoni, naye Bwana akiwatoa, waangamie mbele yangu, mimi nitakuwa kweli kichwa chenu?
10Wazee wa Gileadi wakamwambia Yefuta: Bwana ndiye anayeyasikia, tunayoyasemeana; na atuhukumu, tusipoyafanya uliyoyasema.
11Ndipo, Yefuta alipokwenda pamoja na wazee wa Gileadi, nao watu wakamweka kuwa kichwa chao na kiongozi wao. Naye Yefuta akasema maneno yake yote kule Misipa masikioni pa Bwana.[#Amu. 20:1.]
12Kisha Yefuta akatuma wajumbe kwa mfalme wa wana wa Amoni kwamba: Tuko na mapitano gani mimi na wewe, ukinijia kupiga vita katika nchi yangu?
13Mfalme wa wana wa Amoni akawajibu wajumbe wa Yefuta: Kwa kuwa Waisiraeli wameichukua nchi yangu kutoka Arnoni mpaka Yaboko na Yordani, walipotoka Misri kuja huku; sasa hizi nchi zirudishe pasipo kupiga vita!
14Ndipo, Yefuta alipotuma mara ya pili wajumbe kwa mfalme wa wana wa Amoni,
15akamwambia: Hivi ndivyo, Yefuta anavyosema: Waisiraeli hawakuchukua nchi ya Wamidiani wala nchi ya wana wa Amoni.[#5 Mose 2:9,19.]
16Kwani walipotoka Misri kuja huku, Waisiraeli walishika njia ya nyikani mpaka kufika kwenye Bahari Nyekundu, wakaingia Kadesi.
17Ndipo, Waisiraeli walipotuma wajumbe kwa mfalme wa Edomu kwamba: Na tupite katika nchi yako! Lakini mfalme wa Edomu hakuwasikia; naye mfalme wa Moabu akakataa, walipotuma kwake. Kwa hiyo Waisiraeli wakakaa kwanza Kadesi,[#4 Mose 20:14-21.]
18kisha wakapita nyikani na kuizunguka nchi ya Edomu na nchi ya Moabu. Walipoifikia nchi ya Moabu upande wa maawioni kwa jua wakapiga makambi ng'ambo ya Arnoni pasipo kuingia mipakani kwa Moabu, kwani Arnoni ndio mpaka wa Moabu.[#4 Mose 21:13.]
19Ndipo, Waisiraeli walipotuma wajumbe kwa Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyetawala Hesiboni, nao Waisiraeli wakamwambia: Na tupite katika nchi yako, tufike mahali petu![#4 Mose 21:21-31; 5 Mose 2:26-37.]
20Lakini Sihoni hakuwategemea Waisiraeli, hakuacha, wapite mipakani kwake, ila Sihoni akawakusanya watu wake wote, wakapiga makambi kule Yasa. Lakini alipopigana na Waisiraeli,
21Bwana Mungu wa Isiraeli akamtia Sihoni pamoja na watu wake wote mikononi mwa Waisiraeli, wakawapiga. Ndipo, Waisiraeli walipoichukua nchi yote nzima ya Waamori waliokaa katika nchi hii, iwe yao.
22Wakaichukua nchi yote iliyokuwa mipakani kwa Waamori, iwe yao toka Arnoni mpaka Yaboko, tena toka nyikani mpaka Yordani.
23Bwana Mungu wa Isiraeli alipokwisha kuwafukuza Waamori mbele yao walio ukoo wake wa Waisiraeli, sasa wewe unataka kuwafukuza?
24Kumbe Mungu wako Kamosi anayokupa kuwa mali zako huyachukui, yawe yako? Nayo yote, Bwana Mungu wetu anayotupa machoni petu kuwa yetu, basi, sisi huyachukua.[#4 Mose 21:29.]
25Sasa je? Wewe u mwema kuliko Balaka, mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu? Aligombana nao Waisiraeli, apige vita nao?[#4 Mose 22:2.]
26Nao Waisiraeli hawakukaa Hesiboni na katika mitaa yake, hata Aroeri na katika mitaa yake na katika miji yote iliyoko pande zote mbili za Arnoni miaka 300? Mbona wakati huo hamkutaka kuipokonya?
27Mimi sikukukosea wewe, lakini wewe unanifanyizia vibaya ukija kupigana na mimi. Bwana aliye mwamuzi wa kweli na atuamue leo sisi wana wa Isiraeli nanyi wana wa Amoni.
28Lakini mfalme wa wana wa Amoni hakuyasikia maneno ya Yefuta, aliyotuma kumwambia.
29Ndipo, roho ya Bwana ilipomjia Yefuta, akaenda kupita katika nchi ya Gileadi na ya Manase, kisha akaenda Misipe wa Gileadi, toka Misipe wa Gileadi akawaendea wana wa Amoni.[#Amu. 6:34.]
30Ndipo, Yefuta alipomwapia Bwana kiapo kwamba: Kama utawatia wana wa Amoni mikononi mwangu,
31nami nikirudi salama katika vita vya wana wa Amoni, ndipo, yule atakayetoka wa kwanza milangoni mwa nyumbani mwangu, anijie njiani, atakuwa wake Bwana, nami nitamtoa kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima.
32Kisha Yefuta akawaendea wana wa Amoni kupigana nao, naye Bwana akawatia mikononi mwake.
33Akawapiga kutoka Aroeri, mpaka mtu akifika Miniti kwenye miji ishirini hata Abeli-keramimu (Mbuga ya Mizabibu), pigo hilo likawa kubwa sana. Ndivyo, wana wa Amoni walivyonyenyekezwa mbele yao wana wa Isiraeli.
34Yefuta alipofika Misipa kwenye nyumba yake, mara mwanawe wa kike akatoka kumwendea njiani akipiga patu na kuchezacheza, naye alikuwa mwanawe wa pekee, kuliko yeye hakuwa na mwana mwingine, wala wa kiume, wala wa kike.
35Ikawa, alipomwona akazirarua nguo zake akilia: E mwanangu! Unaninyenyekeza sana! Kumbe wewe nawe u mmoja wao wanaonisikitisha! Mimi nimekifumbua kinywa changu kusema na Bwana, siwezi kuyarudisha niliyoyasema.[#4 Mose 30:3.]
36Naye akamwambia: Baba yangu, kama umekifumbua kinywa chako kusema na Bwana, nifanyizie, kama kinywa chako kilivyosema! Kwa kuwa Bwana amekupa kuwalipiza adui zako, hao wana wa Amoni.
37Kisha akamwambia baba yake: Hili moja tu nilipate: Niache miezi miwili, niende kutembea milimani, niuombolezee uwanawali wangu, mimi pamoja na wenzangu.
38Akamwambia: Basi, nenda kwanza! akampa ruhusa kujiendea miezi miwili. Naye akaenda na wenzake, akauombolezea uwanawali wake huko milimani.
39Hiyo miezi miwili ilipokwisha, akarudi kwa baba yake, naye akamtimilizia kiapo chake, alichokiapa; naye alikuwa hajatambua mtu mume. Tangu hapo ikawa desturi kwao Waisiraeli,
40vijana wa kike wa Waisiraeli waende mwaka kwa mwaka kumwimbia matukuzo binti Yefuta wa Gileadi siku nne.