Waamuzi 12

Waamuzi 12

Yefuta anawashinda Waefuraimu.

1Waefuraimu wakaitwa kukusanyika, wakaenda upande wa kaskazini, wakamwambia Yefuta: Kwa sababu gani ulikwenda kupigana nao wana wa Amoni, usituite kwenda pamoja na wewe? Sasa tutaichoma moto nyumba yako juu yako.[#Amu. 8:1.]

2Lakini Yefuta akawaambia: Vita, tulivyovipiga mimi na watu wangu na wana wa Amoni, vilikuwa vikali mno, nami nilipowaita ninyi, hamkuniokoa mikononi mwao.

3Nilipoona, ya kuwa ninyi hamniokoi, nikajitoa mwenyewe, nikawaendea wana wa Amoni, naye Bwana akawatia mikononi mwangu Ni kwa sababu gani, mkinipandia leo hivi kupigana na mimi?[#Amu. 5:18; 9:1.]

4Kisha Yefuta akawakusanya watu wote wa Gileadi, apigane na Waefuraimu; nao watu wa Gileadi wakawapiga Waefuraimu, kwani walikuwa wamesema: Ninyi m watoro wa Efuraimu, maana Gileadi uko katikati ya nchi ya Efuraimu na ya Manase.

5Lakini Wagileadi walivitwaa vivuko vya Yordani vya kwenda Efuraimu. Vikawa hivyo: kila mara watoro wa Efuraimu waliposema: Na nivuke, watu wa Gileadi wakamwuliza: Wewe u Mwefuraimu? Naye aliposema: Hapana,

6wakamwambia: Tamka Shiboleti! Tena aliposema: Siboleti kwa kuwa hakuweza kutamka Shiboleti, wakamkamata, wakamwua hapo penye vivuko vya Yordani; ndivyo, walivyouawa wakati huo Waefuraimu 42000.

7Yefuta akawa mwamuzi wa Waisiraeli miaka 6, kisha Yefuta wa Gileadi akafa, akazikwa katika mmoja wao miji ya nchi ya Gileadi.

Waamuzi Ibusani na Eloni na Abudoni.

8Baada yake Ibusani wa Beti-Lehemu akawa mwamuzi wa Waisiraeli.

9Alikuwa mwenye wana wa kiume 30 na wa kike 30, ndio aliowaoza kwenda pengine, tena aliingiza wanawake wengine 30 toka pengine, wawe wake za wanawe. Akawa mwamuzi wa Waisiraeli miaka 7.

10Ibusani alipokufa akazikwa Beti-Lehemu.

11Baada yake Eloni wa Zebuluni akawa mwamuzi wa Waisiraeli miaka 10.

12Eloni wa Zebuluni alipokufa akazikwa huko Ayaloni katika nchi ya Zebuluni.

13Baada yake Abudoni, mwana wa Hileli wa Piratoni, akawa mwamuzi wa Waisiraeli.

14Naye alikuwa mwenye wana 40 na wajukuu 30 waliopanda wana wa punda 70. Akawa mwamuzi wa Waisiraeli miaka 8.

15Abudoni, mwana wa Hileli wa Piratoni, alipokufa akazikwa huko Piratoni katika nchi ya Efuraimu mlimani kwa Waamaleki.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania