The chat will start when you send the first message.
1Siku zilipopita, siku za mavuno ya ngano zilipokuwa karibu, Samusoni alikwenda kumwamkia mkewe na kumpa mwana mbuzi, akisema moyoni: Nitaingia chumbani kwa mke wangu. Lakini baba yake hakumpa ruhusa kuingia.
2Baba yake akamwambia: Nilidhani, umechukizwa naye, nikampa mwenzako; je? Ndugu yake mdogo si mwema kuliko yeye? Na awe wako mahali pake![#Amu. 14:20.]
3Samusoni akawaambia: Mara hii sitakora manza kwao Wafilisti nikiwafanyizia mabaya.
4Kisha Samusoni akaenda, akakamata mbweha 300, kisha akachukua mienge yenye moto, akawafunga wawiliwawili mkia kwa mkia, akatia mwenge mmoja katikati ya mikia miwili.
5Tena alipokwisha kuiwasha moto ile mienge, akawaacha, waende mashambani kwa Wafilisti kwenye ngano; ndivyo, alivyozichoma hizo ngano zilizokwisha kufungwa miganda, nazo zilizokuwa mabuani bado, hata mizabibu na michekele.
6Wafilisti walipoulizana: Ni nani aliyeyafanya haya? watu wakasema: Ni Samusoni, mkwewe yule mtu wa Timuna, kwa kuwa amemchukua mkewe, akampa mwenzake. Ndipo, Wafilisti walipopanda huko, wakamteketeza kwa moto yule mwanamke pamoja na nyumba ya baba yake.
7Lakini Samusoni akawaambia: Mkifanya mambo kama hayo, kweli nitajipatia malipizi kwenu, kisha nitaacha.
8Akawapiga akitumia mguu wa mmoja wa kupigia kiuno cha mwingine, likawa pigo kubwa sana. Kisha akaenda kukaa katika pango la mwamba wa Etamu.
9Kisha Wafilisti wakapanda, wakapiga makambi katika nchi ya Yuda, wakajieneza huko Lehi.
10Wayuda walipowauliza: Mmetupandia kwa sababu gani? wakasema: Tumepanda, tumfunge Samusoni, tumfanyizie, kama alivyotufanyizia sisi.
11Ndipo, waliposhuka watu 3000 toka Yuda kwenda kwenye pango la mwamba wa Etamu, wakamwambia Samusoni: Kumbe hujui, ya kuwa Wafilisti wanatutawala? Mbona unatufanyizia mambo kama hayo? Akawaambia: Kama walivyonifanyizia, ndivyo, nilivyowafanyizia nao.
12Wakamwambia: Tumekuja, tukufunge, tukutie mikononi mwa Wafilisti. Samusoni akawaambia: Niapieni, ya kuwa hamtanipiga ninyi, mniue!
13Nao wakamwambia kwamba: Hivyo sivyo, sisi tunataka tu, tukufunge, tukutie mikononi mwao, lakini hatutakuua kabisa. Kisha wakamfunga kwa kamba mbili mpya, wakampandisha kutoka pale mwambani.
14Yeye alipofika Lehi, Wafilisti wakamawendea njiani na kumzomea. Ndipo, roho ya Bwana ilipomjia kwa nguvu, nazo kamba, ambazo mikono ilifungwa nazo, zikawa kama nyuzi zilizounguzwa na moto, pingu zake nazo zikayeyuka na kuanguka mikononi pake.[#Amu. 14:6.]
15Alipoona hapo mfupa mbichi wa taya la punda, akapeleka mkono wake, akauchukua, akaua nao watu 1000.
16Kisha Samusoni akasema:
Kwa taya la punda wanalala machungu,
huku chungu moja, huko machungu mawili;
kwa taya la punda nimewaua watu elfu zima.
17Alipokwisha kuyasema haya, akautupa huo mfupa wa taya, alioushika mkononi mwake; kwa hiyo watu wakapaita mahali pale Ramati-Lehi (Kilima cha Taya).
18Kisha akaona kiu kali, ndipo, alipomlilia Bwana akisema: Wokovu huu mkubwa umewapatia hawa kwa mkono wa mtumishi wako; sasa nife kwa kiu, nianguke mikononi mwao hao wasiotahiriwa!
19Ndipo, Mungu alipopasua shimo lililoko Lehi, mara yakatoka maji humo, naye akanywa, mpaka roho yake ikamrudia, akapata kuwa mzima tena. Kwa hiyo hapo huitwa Chemchemi ya Mliaji, nayo iko huko Lehi hata siku hii ya leo.[#1 Sam. 30:12.]
20Akawa mwamwuzi wa Waisiraeli miaka 20 siku zile za Wafilisti.[#Amu. 16:31.]