Waamuzi 18

Waamuzi 18

Wadani wanakiteka kinyago cha Mika.

1Siku zile hakuwako mfalme kwao Waisiraeli, tena siku zile wao wa shina la Dani walikuwa wanajitafutia fungu la nchi la kukaa, kwani mpaka siku hiyo fungu lao la nchi halijawaangukia katikati ya mashina ya Isiraeli.[#Amu. 1:34; 17:6.]

2Kwa hiyo wana wa Dani wakatoa katika ukoo wao wote mzima watu watano wenye nguvu waliokuwa wa Sora na wa Estaoli, wakawatuma kuipeleleza nchi na kuichunguza wakiwaambia: Nendeni mwichunguze nchi hii! Walipofika milimani kwa Efuraimu kwenye nyumba ya Mika wakalala huko.[#Amu. 13:25.]

3Walipokuwa nyumbani mwa Mika, wakamtambua yule kijana wa Kilawi kwa msemo wake; ndipo, walipomwendea, wakamwuliza: Ni nani aliyekuleta huku? Tena wewe unafanya nini hapa? Uko na kazi gani hapa?[#Amu. 17:7.]

4Akawaambia: Mika amenifanyizia hivi na hivi, akanipa kazi hii ya mshahara kuwa mtambikaji wake.

5Wakamwambia: Mwulize Mungu, tujue, kama njia yetu, tunayokwenda sisi, itafanikiwa.

6Mtambikaji akawaambia: Nendeni na kutengemana! Njia yenu, mnayoishika, Bwana anaiona.

7Hao watu watano walipokwenda zao wakafika Laisi, wakaona, ya kuwa watu waliokuwamo walikaa na kutulia tu kama desturi za Wasidoni, walikaa kimya na kutulia kweli, kwani hakuwako katika nchi hiyo aliyewafanyizia kibaya cho chote, nao wote walikuwa wenye mali. Tena kutoka kwa Wasidoni kufika kwao kulikuwa mbali, hawakupata matata yo yote na watu wo wote.

8Walipofika kwa ndugu zao huko Sora na Estaoli, nao walipowauliza: Mnaleta habari gani?

9wakawaambia: Ondokeni, twende kupanda kwao hao! Kwani tulipoitazama hiyo nchi, tumeiona kuwa njema sana. Nanyi mnanyamaza tu! Msikawilie kwenda na kuiingia hiyo nchi, iwe yenu!

10Mtakapofika mtafika kwenye watu wanaokaa na kutulia, nayo nchi hiyo inapanuka pande mbili. Kweli Mungu ameitia mikononi mwenu, tena ni mahali pasipokoseka lo lote lililoko huku nchini.

11Ndipo, walipoondoka huko Sora na Estaoli watu 600 wa ukoo wa Dani, kila mtu akiwa amejifunga mata ya kupigia vita.

12Walipopanda wakapiga makambi Kiriati-Yerarimu wa Yuda; kwa hiyo watu huita mahali pale Makambi ya Dani hata siku ya leo, pako nyuma ya Kiriati-Yearimu.

13Walipotoka huko na kushika njia ya kweda milimani kwa Efuraimu wakafika kwenye nyumba ya Mika.[#Amu. 17:1.]

14Nao wale watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laisi wakaanza kusema na ndugu zao, wakawaambia: Je? Mnajua, ya kuwa humu katika hizi nyumba kimo kisibau cha mtambikaji pamoja na kinyago cha nyumbani, nacho ni inyago cha kuchongwa kilichovikwa mabati ya fedha. Sasa lijueni la kufanya![#Amu. 17:4-5.]

15Walipoondoka kwenda huko wakaingia nyumbani mwa yule kijana wa Kilawi kwenye nyumba ya Mika, wakaamkiana naye.

16Nao wale watu 600 waliojifunga mata ya kupigia vita, wale wana wa Dani, walikuwa wamesimama pa kuingia langoni.

17Nao wale watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi hii wakaingia humo, wakakichukua kile kinyago cha kuchongwa pamoja na kisibau cha mtambikaji, ni kile kinyago cha nyumbani kilichovikwa mabati ya fedha, naye mtambikaji alikuwa amesimama pa kuingia langoni kwao wale watu 600 waliojifunga mata ya kupigia vita.

18Wale watano walipoingia nyumbani mwa Mika, wakichukue kile kinyago cha kuchongwa pamoja na kisibau cha mtambikaji, ni kile kinyago cha nyumbani kilichovikwa mabati ya fedha, ndipo, mtambikaji alipowauliza: Mnafanya nini?

19Lakini wao wakamwambia: Nyamaza tu ukiubandika mkono wako kinywani pako, upate kwenda nasi kuwa baba yetu na mtambikaji wetu. Ni vema, ukiwa mtambikaji wa mlango wa mtu mmoja, kuliko ukiwa mtambikaji wa shina na wa ukoo mzima kwao Waisiraeli?

20Moyo wa mtambikaji ukayaona haya kuwa mema; ndipo, alipokichukua kisibau cha mtambikaji pamoja na kile kinyago cha nyumbani, ni kile kinyago cha kuchongwa, akaingia kwa hao watu katikati.

21Kisha wakageuka kwenda zao; lakini wanawake pamoja na watoto na nyama wa kufuga na vyombo vilivyokuwa mali walitangulia mbele yao.

22Walipokwisha kuiacha nyumba ya Mika mbali, watu waliokaa katika zile nyumba kwenye nyumba ya Mika wakaitana, wakusanyike, wakaenda kuandamana na wana wa Dani.

23Walipowaita wana wa Dani, wakazigeuza nyuso zao, wakamwuliza Mika: Una nini, mkikusanyika kwa kuitana?

24Akasema: Mmeichukua miungu yangu, niliyoitengeneza, pamoja na mtambikaji, mkajiendea. Sasa mimi niko na nini tena? Nanyi mnaniulizaje: Una nini?

25Nao wana wa Dani wakamwambia: Usitupigie kelele tena, watu wenye uchungu mioyoni wasije kwenu na kuwapiga ninyi, roho yako nazo roho zao walio wa mlango wako zisiangamizwe pamoja.

26Kisha wana wa Dani wakaenda zao, naye Mika alipoona, ya kuwa wao ni wenye nguvu za kumshinda yeye, akarudi nyumbani kwake.

Wadani wanauteka mji wa Laisi.

27Nao wakavichukua vile, Mika alivyovitengeneza, pamoja na mtambikaji aliyekuwa kwake, wakaenda Laisi, kwenye wale watu waliokaa kimya na kutulia tu, wakawapiga kwa ukali wa panga, nao mji wakauteketeza kwa moto.

28Hakuwako aliyewaponya, kwani kwenda Sidoni toka kwao kulikuwa mbali, nao walikuwa hawana matata na watu wo wote; nao mji wao ulikuwa bondeni kuelekea Beti-Rehobu. Kisha wakaujenga huo mji tena, wakakaa humo.

29Lakini jina la mji wakaliita Dani kwa jina la baba yao Dani, Isiraeli aliyemzaa; lakini jina la kwanza la mji lilikuwa Laisi.[#Yos. 19:47.]

30Kisha wana wa Dani wakajisimamishia kile kinyago kilichochongwa, naye Yonatani, mwana wa Gersomu, mwana wa Mose, yeye pamoja na wanawe wakawa watambikaji wa shina la Dani mpaka siku hiyo, walipohamishwa kwenda katika nchi nyingine.[#1 Fal. 12:29.]

31Nao walikuwa wamejisimamishia hicho kinyago, Mika alichokitengeneza, siku hizo zote, Nyumba ya Mungu ilipokuwa huko Silo.[#Yos. 18:1.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania