The chat will start when you send the first message.
1Ndipo, malaika wa Bwana alipotoka Gilgali, akaja kupanda Bokimu, akasema: Naliwatoa Misri, nikawaleta katika nchi hii, niliyoapa kuwapa baba zenu, nikasema: Agano, nlilolifanya nanyi, sitalivunja kale na kale.
2Ninyi msifanye maagano na wenyeji wa nchi hii! Ila pabomoeni pao pa kutambikia! Lakini hamkuisikia sauti yangu; maana yao haya, mliyoyafanya, ndio nini?[#5 Mose 7:2-5.]
3Kwa hiyo nasema nami: Sitawafukuza mbele yenu, wapate kuwasonga mbavuni, nayo miungu yao iwanase kama tanzi.[#Yos. 23:13.]
4Malaika wa Bwana alipowaambia wana wote wa Isiraeli maneno haya, watu wakazipaza sauti zao, wakalia.
5Kwa hiyo wakaliita jina la mahali hapo Bokimu (Vilio), kisha wakamtambikia Bwana.
6Hapo Yosua alipowapa watu wa ukoo huu ruhusa kwenda kwao, wana wa Isiraeli walikwenda kila mtu kwenye fungu lake la nchi, alichukue.
7Watu wakamtumikia Bwana siku zote, Yosua alizokuwapo, nazo siku zote, walizokuwapo wale wazee waliokaa siku nyingi kuliko Yosua, ndio wale walioyaona matendo makuu yote, Bwana aliyowatendea Waisiraeli.[#Yos. 24:31.]
8Naye Yosua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa mwenye miaka 110.
9Wakamzika katika mipaka ya fungu lake huko Timunati-Heresi milimani kwa Efuraimu upande wa kaskazini wa mlima wa Gasi.[#Yos. 24:29-30.]
10Watu wote wa kizazi hicho walipokwisha kukusanywa kwenda kwa baba zao, wakaondokea watu wengine wa kizazi kingine wasiomjua Bwana wala matendo, aliyowatendea Waisiraeli.
11Ndipo, wana wa Isiraeli walipoyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana kwa kuyatumikia Mabaali.
12Wakamwacha Bwana Mungu wa baba zo aliyewatoa katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine miongoni mwao miungu ya makabila yaliyowazunguka, wakaiangukia. Ndivyo, walivyomkasirisha Bwana.
13Walipomwacha Bwana wakamtumikia Baali, nayo Maastaroti.
14Kwa hiyo makali ya Bwana yakawawakia waisiraeli, akawatia mikononi mwa wanyang'anyi, wawanyang'anye mali zao, namo mikononi mwa adui zao waliowazunguka, akawauza, wasiweze tena kusimama usoni pao adui zao.
15Po pote walipotokea, mkono wa Bwana ukawapatia mabaya, kama Bwana alivyowaambia, kama Bwana alivyowaapia; kwa hiyo wakasongeka sana.[#3 Mose 26:17; 5 Mose 28:20.]
16Ndipo, Bwana alipowainulia waamuzi, wawaokoe mikononi mwao waliowanyang'anya mali zao.
17Lakini nao waamuzi hawakuwasikia, kwani walivunja maagano kama wagoni waliofuata miungu mingine na kuiangukia; ndivyo, walivyoondoka upesi katika njia, baba zao waliyoishika, ni ile ya kuyasikia maagizo ya Bwana. Hawakuyafanya hayo.
18Bwana alipowainulia waamuzi, Bwana alikuwa na yule mwamuzi, awaokoe mikononi mwa adui zao siku zote za huyu mwamuzi, kwani Bwana aliwaonea uchugu, walipompigia kite kwa ajili yao waliowatesa na kuwasukumasukuma.
19Lakini huyo mwamuzi alipokufa, wakafanya tena mabaya kuliko baba zao wakifuata miungu mingine, waitumikie na kuiangukia; hawakuacha kabisa kuyafanya hayo matendo yao na kuishika hiyo njia yao iliyokuwa ngumu sana.
20Ndipo, makali ya Bwana yalipowawakia Waisiraeli, akasema: Kwa kuwa watu hawa wamelikosea Agano langu, nililowaagiza baba zao, wakikataa kuisikia sauti yangu,
21mimi nami sitaendelea kufukuza mbele yao watu wa hayo mataifa, Yosua aliowaacha alipokufa.
22Ila nitawatumia kuwajaribu Waisiraeli, kama wataiangalia njia ya Bwana, waishike, kama baba zao walivyoishika, au kama wataiacha.[#Amu. 3:1-4; 5 Mose 8:2.]
23Kwa hiyo Bwana akayaacha hayo mataifa, wakae, asiwafukuze upesi. Kwa hiyo hakuyatia mikononi mwa Yosua.