The chat will start when you send the first message.
1Siku ile Debora na Baraka, mwana wa Abinoamu, wakaimba kwamba:
2Kwa kuwa walikuwako waliowaongoza Waisiraeli, kwa kuwa nao watu wamejitoa wenyewe, kwa hiyo mtukuzeni aliye Bwana!
3Sikieni, ninyi wafalme! Sikilizeni, ninyi watawalaji! Mimi, mimi mwenyewe na nimwimbie Bwana, na nimshangilie Bwana Mungu wa Isiraeli!
4Bwana, ulipotoka Seiri, ulipopita mashambani kwa Edomu, nchi ikatetemeka, mbingu nazo zikanyesha, mawingu nayo yakanyesha mvua.[#5 Mose 33:2; Hab. 3:3-6.]
5Milima ikatukutika mbele ya Bwana, nao Sinai mbele yake Bwana, Mungu wa Isiraeli alipotokea.[#Sh. 68:9.]
6Siku za Samugari, mwana wa Anati, barabara zilikuwa zimekufa, hata siku za Yaeli; nao walioshika njia hupitia zile za kupotokapotoka.[#Amu. 3:31.]
7Kwao Waisiraeli hakukuwa na wakulima, walikuwa wamekoma, walikuwa wamekoma kweli, mpaka wewe, Debora, ulipotokea, nawe ukawatokea Waisiraeli kuwa mama yao.
8Walikuwa wamejichagulia miungu mipya; lakini vita vilipofika malangoni, haikuwako ngao wala mkuki kwao waume wa Waisiraeli, nao walikuwa maelfu arobaini.[#1 Sam. 13:19,22.]
9Moyo wangu huwaelekea waongozi wa Waisiraeli waliojitoa wenyewe miongoni mwa watu. Mtukuzeni aliye Bwana!
10Ninyi mpandao punda weupe, nanyi mkaliao mazulia, nanyi mtembeao njiani: yafikirini mioyoni![#Amu. 10:4; 12:14.]
11Wapiga mishale wanapocheza pamoja nao wachota maji, ndipo wayatangaze matendo ya Bwana yaongokayo, hayo matendo yaongokayo ndiyo, aliyowatendea wao waliokuwa wakulima kwao Waisiraeli. Ndipo, watu wa Bwana waliposhuka kufika malangoni.
12Amka! Amka, Debora! Amka! Amka, uimbe wimbo! Inuka, Baraka, upate kuwateka wanaotaka kukuteka, mwana wa Abinoamu!
13Ndipo, waliosalia waliposhuka kuwaendea wale watukufu, Bwana naye akashuka kuja kwangu nao hao mafundi wa vita:
14Efuraimu ndiko, walikotoka waliozaliwa Amaleki, Wabenyamini nao wakakufuata pamoja na watu wako wengi, kwao Wamakiri wakatoka wajuao kuongoza watu, kwao Wazebuluni wakatoka wao walioshika bakora, nazo zilikuwa zao waandaliaji wa vita.[#Amu. 12:15; Yos. 17:1.]
15Wakuu wa Isakari wakawa naye Debora, tena kama Isakari vilevile naye Baraka, ndiye aliyejihimiza kwa miguu yake kumkimbilia pale bondeni.
Lakini kule kwa vijito vya Rubeni kulikuwa na mambo, ndiyo mashauri ya mioyo yaliyo makuu.
16Mbona unataka kukaa tu mazizini kwa kondoo? Unataka kusikiliza mazomari yanayopigiwa makundi? Kweli vijitoni kwa Rubeni yako mashauri makuu ya mioyoni!
17Wagileadi wakasalia ng'ambo ya Yordani, mbona Wadani nao hukaa ugenini kwenye merikebu? Waaseri nao hukaa tu pwani kwenye bahari, kweli huwa kimya katika bandari zao.
18Lakini Wazebuluni ni watu wasiojiangalia kufani, Wanafutali nao ndivyo, walivyo kwao mashambani vilimani.
19Wafalme wakaja kufika huku, wapige vita; wafalme wa Kanaani ndio waliovipiga kule Taanaki kwenye maji ya Megido, lakini nyara, ijapo ziwe za fedha kidogo tu, hawakuzipata kabisa.
20Toka mbinguni wametupigania, nyota zilipokuja, zikaziacha njia zao kwa kupigana na Sisera.[#Amu. 4:15; 2 Mose 14:25; Yos. 10:14,42.]
21Kijito cha Kisoni kikawaporomosha, hicho kijito cha Kisoni kilicho kijito cha kale; roho yangu nawe, wakanyage kwa nguvu!
22Ndipo, zilipopiga shindo kwa kukimbia kwato za farasi, wanguvu waliowapanda walipowakimbiza.
23Ndivyo, asemavyo malaika wa Bwana: Uapizeni Merozi! Waapizeni! Waapizeni wao wenyeji wake! Kwani hawakufika kusaidiana na Bwana, hawakusaidiana na Bwana kwao walio mafundi wa vita.
24Yaeli ndiye atakayetukuzwa kuliko wenzake, mkewe Mkeni Heberi ndiye, watakayemsema mahemani, apate kutukuzwa zaidi kuliko wenzake.
25Alipomwomba maji, akampa maziwa, akampelekea mafuta ya maziwa katika chombo kitukufu.[#Amu. 4:19.]
26Akaukunjua mkono wake kuchukua uwambo, nao mkono wake wa kuume ukashika nyundo ya wahunzi, akakivunja kichwa chake Sisera na kukipiga nyundo, akakiponda na kulitoboa paji lake.
27Miguuni pake akaanguka magotini, kisha akalala, kweli akaanguka magotini miguuni pake; alipopiga magoti, ndipo, alipoanguka, akawa mfu.
28Anachungulia dirishani na kulia kwa sauti kuu, mamake Sisera anachungulia katika vyuma vya dirisha: Mbona gari lake limechelewa kuja? Mbona magurudumu ya magari yake yanakawia hivyo?
29Wenzake wakuu wa kike wakamjibu, nao ni werevu wa kweli, naye mwenyewe akajijibu maneno yaleyale ya kwamba:
30Labda wameona nyara za kujigawanyia: mwanamwali mmojammoja au wawiliwawili wa kila mtu mmoja, tena ziko nguo za rangi, ndizo nyara zake Sisera, hizo nyara ni nguo za rangi zilizofumwa vizuri, ni nguo za rangi za mbalimbali, ni zenye darizi pande mbili za kupatana na shingo zao walio wenye hizo nyara.
31Hivyo na waangamie wote walio adui zako, Bwana! Lakini wao wampendao na wawe kama jua lenyewe, likija kucha lenye utukufu wake![#Amu. 3:11.]
Kisha nchi ikapata kutulia miaka 40.