Waamuzi 6

Waamuzi 6

Gideoni anakwitwa kuwa mwamuzi.

1Wana wa Isiraeli walipoyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, Bwana akawatia mikononi mwao Wamidiani miaka saba.

2Mikono ya Wamidiani ilipowalemea Waisiraeli, wana wa Isiraeli wakajitengenezea kwa ajili ya Wamidiani mashimo yaliyokuwa milimani na mapango na magenge.

3Ikawa, Waisiraeli walipopanda mbegu, Wamidiani na Waamaleki na wengine waliokaa upande wa maawioni kwa jua wakapanda kwao,[#5 Mose 28:33.]

4wakapiga makambi kwao, wakayaharibu yote yaliyozaliwa mashambani, mpaka kufika Gaza, hawakusaza kwao Waisiraeli hata nyama mmoja, wala kondoo, wala ng'ombe, wala punda.

5Kwani walipopanda wakaleta makundi na mahema yao, wakaja wengi mno kama nzige, hawakuhesabika wala wenyewe, wala ngamia wao, nao wakajia tu kuiharibu nchi.

6Waisiraeli walipopondeka sana kwa ajili ya Wamidiani, wakamlilia Bwana.

7Ikawa, wana wa Isiraeli walipomlilia Bwana kwa ajili ya Wamidiani,

8ndipo, Bwana alipotuma mfumbuaji kwa wana wa Isiraeli: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Isiraeli, akawaambia: Mimi nimewaleta huku na kuwatoa Misri nyumbani, mlimokuwa watumwa.

9Nikawaponya mikononi mwa Wamisri namo mikononi mwao wote waliowatesa, nikiwafukuza mbele yenu, kisha nikawapa nchi yao,

10nikawaambia: Mimi Bwana ni Mungu wenu, msiiche miungu yao Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao! Lakini hamkuisikia sauti yangu.

11Kisha malaika wa Bwana akaja, akakaa chini ya mkwaju kule Ofura uliokuwa wa Yoasi wa Abiezeri, mwanawe Gideoni alipokuwa akipura ngano penye kukamulia mvinyo, azifiche machoni pa Wamidiani.

12Malaika wa Bwana alipomtokea akamwambia: Bwana yuko pamoja na wewe uliye fundi wa vita mwenye nguvu!

13Gideoni akamwambia: E bwana wangu, kama Bwana yuko nasi, haya yote yamewezaje kutupata? Yako wapi matendo yake yote ya kustaajabu, baba zetu waliyotusimulia kwamba: Kumbe Bwana hakutuleta huku na kututoa Misri? Lakini sasa Bwana ametutupa, akatutia mikononi mwa Wamidiani.

14Ndipo, Bwana alipomgeukia na kusema: Nenda kwa hizi nguvu zako kuwaokoa Waisiraeli mikononi mwa Wamidiani! Je? Si mimi ninayekutuma?[#1 Sam. 12:11; Ebr. 11:32.]

15Akamwambia: E bwana wangu, niwaokoe Waisiraeli kwa nini? Tazama, udugu wetu ni mnyonge kuliko zote za Manase, nami ni mdogo nyumbani mwa baba yangu.

16Bwana akamwambia: Mimi nikiwa na wewe, ndipo, utakapowapiga Wamidiani, kama ni mtu mmoja tu.[#2 Mose 3:12.]

17Naye akamwambia: Kama nimeona upendeleo machoni pako, nipatie kielekezo, nijue, ya kuwa ndiwe wewe unayesema na mimi.

18Usiondoke hapa, mpaka niingie nyumbani, nikuletee kipaji changu, nikiweke mbele yako. Akasema: Basi, mimi nitakaa, mpaka urudi.[#Amu. 13:15.]

19Ndipo, Gideoni alipoingia nyumbani, akatengeneza kidume cha mbuzi na vikate, mara moto ukatoka mwambani, ukazila hizo nyama na hivyo vikate visivyochachwa vya pishi ya unga; kisha nyama akazitia katika kikapu nao mchuzi katika nyungu, akampelekea huko chini ya mkwaju, akamkaribisha.

20Naye malaika wa Mungu akamwambia: Chukua hizi nyama na hivi vikate, uviweke mwambani pale, kisha vimwagie huu mchuzi. Akafanya hivyo.

21Naye malaika wa Bwana akaipeleka ncha ya mkongojo, aliokuwa nao mkononi, akazigusa hizo nyama na hivyo vikate. Kisha malaika wa Bwana akatoweka machoni pake.[#3 Mose 9:24.]

22Ndipo, Gideoni alipoona, ya kuwa yeye alikuwa malaika wa Bwana; kwa hiyo Gideoni akasema: Limenipata, Bwana Mungu! Kwa kuwa nimemwona malaika wa Bwana uso kwa uso!

23Ndipo, Bwana alipomwambia: Tengemana tu! Usiogope! Hutakufa.[#Amu. 13:22.]

24Kwa hiyo Gideon akamjengea Bwana huko pa kumtambikia, akapaita Utengemano wa Bwana, napo pangalipo hata siku hii ya leo huko Ofura kwao wa Abiezeri.

25Ikawa usiku ule, ndipo, Bwana alipomwambia: Chukua dume la ng'ombe la baba yako na dume jingine la ng'ombe la miaka saba! Kisha pabomoe mahali pa baba yako pa kumtambikia Baali, nacho kinyago cha Ashera kilichopo hapohapo kando yake kikatekate![#2 Fal. 11:18; 23:12-15.]

26Kisha umjengee Bwana Mungu wako pa kumtambikia hapa juu ngomeni na kupatengeneza vema! Kisha lichukue lile dume la ng'ombe la pili, ulitoe kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ukivitumia vile vipande vya kinyago cha Ashera, ulichokikatakata, kuwa kuni!

27Ndipo, Gideoni alipochukua watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya, kama Bwana alivyomwagiza; lakini kwa kuwaogopa wao wa mlango wa baba yake na watu wa mjini hakuvifanya machana, ila usiku.

28Watu wa mjini walipoamka asubuhi na mapema, wakaona: Pa kumtambikia Baali pamebomolewa, nacho kinyago cha Ashera kilichokuwa kando yake kimekatwakatwa, nalo dume la pili limekwisha kuteketezwa lote zima hapo pengine pa kutambikia palipojengwa.

29Wakaulizana kila mtu na mwenzake: Ni nani aliyelifanya jambo hili? Walipotafuta hivyo na kuchunguza mwisho wakasema: Gideoni, mwana wa Yoasi, amelifanya jambo hili.

30Ndipo, watu wa mjini walipomwambia Yoasi: Mtoe mwanao, auawe! Kwani pa kumtambikia Baali amepabomoa, nacho kinyago cha Ashera kilichokuwa kando yake amekikatakata.

31Lakini Yoasi akawaambia hao wote waliosimama mbele yake: Je? Ninyi mwataka kumgombea Baali, mmwokoe? Ndiye atakayemgombea atauawa na mapema haya. Kama yeye ni mungu, na ajigombee mwenyewe, kwa kuwa wako waliopabomoa pake pa kumtambikia.[#1 Fal. 18:21.]

32Kwa hiyo watu wakamwita Gideoni siku hiyo Yerubaali, ni kwamba: Baali na ajigombee, kwa kuwa wako waliopabomoa pake pa kumtambikia.

33Wamidiani na Waamaleki na wengine waliokaa upande wa maawioni kwa jua walipokusanyika wote pamoja, wakavuka, wakaja kupiga makambi bondeni kwa Izireeli.

34Ndipo, roho ya Bwana ilipomjaa Gideoni; alipopiga baragumu, wa Abiezeri wakaitikia na kumfuata.[#Amu. 3:10; 11:29; 13:25.]

35Kisha akatuma wajumbe katika nchi yote ya Manase, nao wakaitikia na kumfuata. Hata katika nchi za Aseri na za Zebuluni na za Nafutali akatuma wajumbe, nao wakapanda kuja kuwakuta.

36Naye Gideoni akamwambia Mungu: Ikiwa, unataka kuwaokoa Waisiraeli kwa kuitumia mikono yangu, kama ulivyosema,

37basi, niweke ngozi ya kondoo yenye manyoya hapa penye kupuria ngano; kama umande utakuwa ngozini tu, nchi yote ikiwa kavu, ndipo, nitakapojua, ya kuwa utawaokoa Waisiraeli kwa kuitumia mikono yangu, kama ulivyosema.

38Ikawa hivyo; kesho yake alipoamka na mapema, akaikamua ile ngozi, auondoe umande humo ngozini, nayo maji yake yakajaza bakuli.

39Gideoni akamwambia Mungu: Makali yako yasiniwakie, nikisema tena mara hii tu kwa kuijaribu ngozi hii tena mara moja tu: ngozi pekee yake iwe kavu, lakini nchi yote ipate umande![#1 Mose 18:30.]

40Mungu akafanya hivyo usiku huo, ngozi ikawa kavu peke yake, lakini nchi yote ikawa yenye umande.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania