The chat will start when you send the first message.
1Kisha Yerubaali, ndiye Gideoni, na watu wote waliokuwa naye, wakaondoka asubuhi, wakapiga makambi kwenye chemchemi ya Harodi, nayo makambi ya Wamidiani yalikuwa upande wa kaskazini humo bondeni nyuma ya kilima cha More.[#Amu. 6:32.]
2Ndipo, Bwana alipomwambia Gideoni: Watu walio kwako ni wengi, sitawatia Wamidiani mikononi mwao, Waisiraeli wasijitukuze kuliko mimi kwamba: Mikono yetu ndiyo iliyotuokoa.
3Sasa tangaza masikioni mwa watu kwamba: Aogopaye kwa kuwa mwenye moyo mdogo na arudi na kuondoka kilimani kwa Gileadi! Ndipo, waliporudi watu 22000, wakasalia 10000.[#5 Mose 20:8.]
4Lakini Bwana akamwambia Gideoni: Watu wangaliko wengi bado; watelemshe kufika penye maji, ndipo, nitakapokuchagulia watu. Kila nitakayekuambia: Huyu na aende na wewe, basi, ndiye atakayekwenda na wewe; lakini kila nitakayekuambia: Huyu asiende na wewe, basi, yeye hatakwenda.
5Ndipo, alipowatelemsha watu kufika penye maji, naye Bwana akamwambia Gideoni: Kila atakayelamba maji kwa ulimi wake, kama mbwa anavyolamba, umweke mahali pake! Vilevile kila atakayepiga magoti yake, apate kunywa, umweke pake!
6Basi, hesabu yao waliolamba maji wakiyapleeka vinywani kwa viganja ikawa watu 300; wengine wote walipiga magoti yao, wapate kunywa maji.
7Ndipo, Bwana alipomwambia Gideoni: Nitawatumia hawa watu 300 waliolamba maji, niwaokoe ninyi nikiwatia Wamidiani mikononi mwako; lakini wale watu wote wajiendee kila mtu mahali pake![#1 Sam. 14:6.]
8Ndipo, walipozichukua pamba za njiani za hao watu na mabaragumu yao mikononi mwao, kisha akawapa ruhusa wale Waisiraeli wote kila mtu kwenda hemani kwake, akiwashika wale 300 tu. Lakini makambi ya Wamidiani yalikuwa mle bondeni upande wa chini yake.
9Usiku huo Bwana akamwambia: Inuka, ushuke kufika kwenye makambi! Kwani nimewatia mikononi mwako.
10Lakini kama unaogopa kushuka, shuka wewe tu na kijana wako Pura, mfike kwenye makambi.
11Napo, utakapoyasikia wanayosemeana, ndipo, mikono yako itakapopata nguvu, ushuke kuingia makambini. Kwa hiyo akashuka yeye na kijana wake Pura, wafike pembeni kwao wenye mata waliokuwamo mle makambini.
12Nao Wamidiani na Waamaleki nao wote wengine waliokaa upande wa maawioni kwa jua walikuwa wamelala humo bondeni wengi mno kama nzige, nao ngamia wao hawakuhesabika, kwani walikuwa wengi kama mchanga ulioko ufukoni kwenye bahari.
13Gideoni alipofika, mara akasikia, mtu alivyomsimulia mwenzake ndoto na kusema: Angalia! Nimeota ndoto, nikaona, mkate wa mofa wa mawele ulivyofingirika katika makambi ya Wamidiani, ukafika kwenye hema moja, ukalipiga, lianguke, ukalifudikiza, ya chini yaje juu; basi, hilo hema likalala hivyo pale chini.[#1 Mose 40:9,16.]
14Mwenzake akamjibu akisema: Hili silo jingine lisipokuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoasi, yule mtu wa Isiraeli. Mungu amewatia Wamidiani na makambi haya yote mikononi mwake.
15Ikawa, Gideoni aliposikia, hiyo ndoto ilivyosimuliwa, tena ilivyofumbuliwa maana, akamwangukia Mungu, kisha akarudi makambini kwa Waisiraeli, akawaambia; Inukeni! Kwani Bwana ameyatia makambi ya Wamidiani mikononi mwenu.[#Yes. 9:4.]
16Kisha akawagawanya wale watu 300 kuwa vikosi vitatu, akawapa kila mtu mkononi mwake baragumu na chungu kitupu kilichomo na mienge ya moto.
17Akawaambia: Mtakayoyaona kwangu mtayafanya nanyi. Mtakaponiona, ya kuwa nimefika pembeni kwenye makambi, ndipo mfanye sawasawa, kama mimi nitakavyofanya!
18Nitakapopiga baragumu mimi pamoja nao wote walioko kwangu, ndipo, nanyi mtakapoyapiga mabaragumu pande zote pia za makambi yote na kusema: Tunaye Bwana na Gideoni!
19Gideoni na watu mia waliokuwa naye wakafika pembeni kwenye makambi, zamu ya usiku wa manane ilipoanza, kwani papo hapo walikuwa wameweka walinzi; mara wakapiga mabaragumu pamoja na kuvivunja vyungu, walivyovishika mikononi mwao.
20Ndipo, vikosi vyote vitatu vilipoyapiga mabaragumu na kuvivunja vile vyungu, wakashika mikononi mwao mwa kushoto mienge, namo mikononi mwao mwa kulia yale mabaragumu ya kupiga, wakapiga makelele kwamba: Tunao upanga wa Bwana na wa Gideoni!
21Lakini wakasimama tu kila mtu mahali pake pande zote za makambi. Ndipo, majeshi yote yalipopiga mbio na kulia sana, yakakimbia kabisa.
22Yale mabaragumu 300 yalipolia, Bwana akazielekeza panga zao wenyewe, kila mtu ampige mwenzake katika makambi yote; ndipo, hayo majeshi yalipokimbia mpaka Beti-Sita kunakoelekea Serera, wengine mpaka mto wa Abeli-Mehola karibu ya Tabati.
23Kisha Waisiraeli wakaitwa katika nchi za Nafutali na za Aseri na za Manase pia, wakawakimbiza Wamidiani.
24Gideoni akatuma wajumbe kwenda milimani po pote kwa Efuraimu kwamba: Shukeni kuwajia Wamidiani, mfike mbele yao kwenye maji ya Beti-Bara, hata kwenye Yordani. Watu wote wa Efuraimu wakaitikia, wakapapata pote palipo penye maji mpaka Beti-Bara, nao Yordani.
25Wakakamata wakuu wawili wa Midiani, Orebu (Kunguru) na Zebu (Chui), wakamwua Orebu penye Mwamba wa Kunguru, naye Zebu wakamwua penye Kamulio la Chui. Walipokwisha kuwafukuza Wamidiani, wakavichukua vichwa vyao Orebu na Zebu ng'ambo ya huko ya Yordani, wakampelekea Gideoni.