The chat will start when you send the first message.
1Abimeleki, mwana wa Yerubaali, akaenda Sikemu kwa ndugu za mama yake, akawaambia wao nao wote walio wa ukoo wa mlango wa baba ya mama yake kwamba:[#Amu. 8:31.]
2Semeni masikioni mwao wote walio wenyeji wa Sikemu: Lililo jema lenu ni lipi? Watu 70 walio wote wana wa Yerubaali wawatawale, au awatawale mtu mmoja? Tena kumbukeni, ya kuwa huyu ni mwenzenu kwa mifupa na kwa nyama za mwili wake.
3Nao ndugu za mama yake walipoyasema maneno hayo yote kwa ajili yake masikioni mwao wenyeji wote wa Sikemu, mioyo yao ikageuka kumfuata Abimeleki, kwani walisema: Yeye ni ndugu yetu!
4Wakampa fedha 70, walizozitoa nyumbani mwa Baali la agano, naye Abimeleki akazitumia kujipatia watu wenye ukorofi wasiokuwa na kitu cho chote, wafuatane naye.[#Amu. 8:33.]
5Kisha akaenda Ofura nyumbani mwa baba yake, akawaua ndugu zake, wana wa Yerubaali, wote 70 juu ya jiwe moja, akasalia tu Yotamu, mwanawe mdogo Yerubaali, kwa kuwa alijificha.
6Kisha wenyeji wote wa Sikemu wakakusanyika nao wote waliokaa bomani, wakaenda, wakamfanya Abimeleki kuwa mfalme huko kwenye huo mvule wa ngomeni ulioko Sikemu.[#Yos. 24:26.]
7Watu walipompasha Yotamu habari hizi, akaenda, akasimama juu ya mlima wa Gerizimu, akapaza sauti yake, akawaitia kwamba: Nisikilizeni, ninyi wenyeji wa Sikemu, Mungu naye awasikie!
8Miti ilikwenda kupaka mmoja mafuta, awe mfalme wao, ikauambia mchekele: Ututawale wewe!
9Lakini mchekele ukaiambia: Niache kuzaa mafuta, nayo ndiyo, wanayoniheshimia Mungu na watu? Nitawezaje kwenda kuning'inia juu ya miti?
10Ndipo, miti ilipouambia mkuyu: Haya! Wewe ututawale sisi!
11Mkuyu nao ukaiambia: Niache kuzaa matunda yangu matamu yaliyo mazuri mno? Nitawezaje kwenda kuning'inia juu ya miti?
12Ndipo, miti ilipouambia mzabibu: Haya! Wewe ututawale sisi!
13Lakini mzabibu nao ukaiambia: Niache kuzaa mvinyo zangu mbichi zinazowafurahisha wote, Mungu na watu? Nitawezaje kwenda kuning'inia juu ya miti?
14Ndipo, miti yote ilipouambia mchongoma: Haya! Wewe ututawale sisi![#2 Fal. 14:9.]
15Mchongoma ukaiambia miti: Kama mnataka kweli kunipaka mafuta, niwe mfalme wenu, njoni, mkae pasipo woga kivulini pangu! Kama hamtaki, moto na utoke katika mchongoma, uile miangati ya Libanoni.
16Sasa ninyi je? Mmejitokeza kuwa wenye kweli na welekevu mlipomfanya Abimeleki kuwa mfalme? Au Yerubaali nao walio wa mlango wake mmewatendea mema na kuwafanyizia, kama mikono yake ilivyowafanyizia ninyi?
17Kwani baba yangu aliwapigia vita na kujitoa mwenyewe, apate kuwaponya mikononi mwa Wamidiani.
18Lakini ninyi mmeuinukia leo mlango wa baba yangu mkiwaua wanawe 70 juu ya jiwe moja, mkamfanya Abimeleki, mwana wa kijakazi wake, kuwa mfalme wa wenyeji wa Sikemu, kwa kuwa ni ndugu yenu.
19Bai, kama mmejitokeza kuwa wenye kweli na welekevu katika mambo haya, mliyomfanyizia leo Yerubaali nao walio wa mlango wake, na mmfurahie Abimeleki, naye na awafurahie ninyi!
20Lakini kama sivyo, moto na utoke kwake Abimeleki, uwale wenyeji wa Sikemu nao wakaao bomani! Tena moto na utoke kwao wenyeji wa Sikemu nako kwao wakaao bomani, umle Abimeleki![#Amu. 9:57.]
21Kisha Yotamu akapiga mbio kukimbia, akafika Beri, akakaa huko na kujificha, ndugu yake Abimeleki asimwone.
22Abimeleki alipowatawala Waisiraeli miaka mitatu,
23Mungu akatuma roho mbaya, Abimeleki na wenyeji wa Sikemu wakosane, nao wenyeji wa Sikemu wakamdanganya Abimeleki na kuyavunja maagano yao.
24Yakafanyika hayo kwamba makorofi, wale wana 70 wa Yerubaali waliyotendewa, yalipizwe, nazo damu zao zimjie ndugu yao Abimeleki aliyewaua, ziwajie nao wenyeji wa Sikemu walioishupaza mikono yake, apate nguvu za kuwaua ndugu zake.[#Amu. 9:5.]
25Kwa kumtakia mabaya wenyeji wa Sikemu wakaweka washambuliaji juu ya milima, wawanyang'anye mali zao wote waliopita njiani hapo, walipokuwa. Naye Abimeleki akapashwa habari hizi.
26Kisha Gali, mwana wa Ebedi, akaja na ndugu zake, akapita kuingia Sikemu, nao wenyeji wa Sikemu walikuwa wanamjetea.
27Walipotoka kwenda shambani kuvuna zabibu na kuzikamua, wakafanya sikukuu, wakaingia nyumbani mwa mungu wao, wakala, wakanywa, kisha wakamwapiza Abimelei.
28Ndipo, Gali, mwana wa Ebedi, aliposema: Abimeleki ni nani? nasi Wasikemu tu wa nani, tumtumikie? Siye mwana wa Yerubaali? Naye Zebuli siye msimamizi wake? Watumikieni watu wa Hamori aliye baba yao Wasikemu! Kwa nini sisi tumtumikie yeye?[#1 Mose 34:2.]
29Kama mtu angewatia watu hawa mkononi mwangu, ningemwondoa Abimeleki. Kisha akamwambia Abimeleki: Haya! Ongeza vikosi vyako, utoke!
30Zebuli, mkuu wa mji, alipoyasikia haya maneno ya Gali, mwana wa Ebedi, makali yake yakawaka moto.
31Kwa ujanja wake akatuma wajumbe kwenda kwa Abimeleki kwamba: Tazama, Gali, mwana wa Ebedi, na ndugu zake wamekuja Sikemu, nao hujulikana, ya kuwa wanawahimiza watu wa mji, wakukatae.
32Sasa ondoka usiku huu, wewe na watu wako walioko kwako, uvizie shambani!
33Tena asubuhi, jua litakapokucha, ujidamke, uushambulie mji huu! Hapo utakapomwona, akikutokea yeye pamoja nao wote walioko kwake, utamfanyizia, mkono wako utakayoyaona.
34Ndipo, Abimeleki alipoondoka usiku pamoja na watu wote waliokuwa kwake, wakauvizia Sikemu kwa vikosi vinne.
35Gali, mwana wa Ebedi, alipotoka na kusimama hapo pa kuliingilia lango la mji, Abimeleki akaondoka hapo, alipokuwa anavizia pamoja na wale watu waliokuwa kwake.
36Gali alipowaona hao watu akamwambia Zebuli: Tazama! Wako watu wanaotelemka toka milimani juu! Lakini Zebuli akamwambia: Vivuli vya milima unaviona kuwa kama watu.
37Naye Gali akasema tena kwamba: Tazama! Ni watu wanaotelemka kutoka katikati ya nchi hii, nacho kikosi kimoja kinatoka na kushika njia ya kwenda kenye mvule, wanakotambikia.
38Zebuli akamwambia: Sasa kiko wapi kinywa chako kilichosema: Abimeleki ni nani, tumtumikie? Kumbe hao watu sio, uliowabeua? Haya! Toka sasa, upigane nao!
39Ndipo, Gali alipotoka akiwatangulia wenyeji wa Sikemu, akapigana na Abimeleki.
40Lakini Abimeleki akamkimbiza, naye akamkimbia, wakaumizwa watu wengi, wakaanguka hapohapo mpaka pa kuingia langoni penye mji.
41Abimeleki akakaa Aruma, lakini Zebuli akamfukuza Gali na ndugu zake, wasikae Sikemu tena.
42Kesho yake watu walipokwenda shambani, naye Abimeleki alipopata habari,
43akawachukua watu wake, akawagawanya kuwa vikosi vitatu, akawavizia hapo shambani. Alipochungulia, mara akaona, watu wakitoka mjini, akawainukia, akawapiga.
44Mara Abimeleki na kikosi kilichokuwa naye wakavuka kwenda mbele, wakasimama pa kuingia langoni penye mji, navyo vikosi viwili vikawarukia wote waliokuwako mashambani, vikawaua.
45Abimeleki alipopigana nao wa mjini mchana kutwa, akauteka huo mji, nao watu waliokuwamo akawaua, nao mji akaubomoa kabisa, kisha akaumwagia chumvi.
46Wote waliokaa katika mnara wa Sikemu walipoyasikia wakajificha shimoni mle nyumbani mwa mungu wao wa agano.[#Amu. 8:33; 9:4.]
47Abimeleki alipopata habari, ya kuwa wote waliokaa katika mnara wa Sikemu wamekusanyika,
48Abimeleki akaupanda mlima wa Salmoni yeye pamoja na watu wote waliokuwa kwake, naye Abimeleki akachukua shoka mkononi mwake, akakata matawi ya miti, akayachukua na kujitwika mabegani, akawaambia wale watu waliokuwa naye: Mtakayoyaona, ya kuwa nimeyafanya, yafanyeni nanyi upesi kama mimi!
49Kwa hiyo nao watu wote wakakata matawi wakimfuata Abimeleki, wakayaweka juu ya lile shimo, wakayachoma moto juu yao waliomo shimoni; ndivyo, walivyokufa nao watu wote waliokaa katika mnara wa Sikemu, ni kama watu 1000 wanawaume na wanawake.
50Kisha Abimeleki akaenda Tebesi, akapiga makambi kule Tebesi, kisha akauteka.
51Katikati ya mji palikuwa na mnara wenye nguvu; ndimo, walimokimbilia wanawaume na wanawake wote na wenyeji wote wa huo mji, wakafunga nyuma yao, wakapaa kipaani pa mnara.
52Abimeleki alipofika penye mnara huo kupiga vita huko, akaukaribia mlango wa mnara, auchome moto.
53Ndipo, mwanamke mmoja alipomtupia Abimeleki kichwani pake jiwe la sago, likakivunja kichwa chake.
54Naye akamwita upesi kijana aliyemchukulia mata yake, akamwagiza: Uchomoe upanga wako, uniue, watu wasiseme, ya kama mwanamke ameniua![#1 Sam. 31:4.]
55Ndipo, kijana wake alipomchoma upanga, kisha akafa.
56Waisiraeli walipoona, ya kuwa Abimeleki amekufa, wakaenda zao kila mtu mahali pake.[#Amu. 9:5.]
57Ndivyo, Mungu alivyoyalipiza yale mabaya ya Abimeleki, aliyomfanyizia baba yake na kuwaua ndugu zake 70.[#Amu. 9:20.]
58Nayo mabaya ya watu wa Sikemu Mungu aliwarudishia vichwani pao; ndivyo, kiapizo cha Yotamu, mwana wa Yerubaali, kilivyowajia.