Yohana 14

Yohana 14

Kwenda kwa Baba.

1Mioyo yenu isizizimke! Mtegemeeni Mungu, nami mnitegemee!

2Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi. Kama visingekuwa hivyo, ningewaambia: Nakwenda kuwatengenezea mahali.

3Nami ijapokuwa ninakwenda kuwatengenezea mahali, nitakuja tena, niwachukue kuwapeleka mwangu, kwamba nanyi mwepo hapo, nilipo mimi.[#Yoh. 12:26; 17:24.]

4Nayo njia ya kwenda pale, nitakapokwenda mimi, mmeijua.

5Ndipo, Toma alipomwambia: Bwana, tusipopajua, unapokwenda, njia tutaijuaje?

6Yesu akamwambia: Mimi ndiyo njia na kweli na uzima; hakuna atakayefika kwa Baba asiponishika mimi.*[#Yoh. 11:25; Mat. 11:27; Rom. 5:1-2; Ebr. 10:20.]

7Kama mngenitambua mimi, mngemjua hata Baba yangu. Tangu sasa mwamtambua, tena mmemwona.

8Filipo akamwambia: Bwana, tuonyeshe Baba! hivi vitatutosha.

9Yesu akamwambia: Miaka hii yote nipo pamoja nanyi, nawe hujanitambua, Filipo? Aliyeniona mimi amekwisha kumwona Baba. Unasemaje: Tuonyeshe Baba?[#Yoh. 12:45; Ebr. 1:3.]

10Huyategemei, ya kuwa mimi nimo mwa Baba, naye Baba yumo mwangu mimi? Maneno, ninayowaambia, siyasemi kwa mawazo yangu mwenyewe, ila Baba anayekaa mwangu ndiye anayezitenda kazi zake.[#Yoh. 12:49.]

11Nitegemeeni, ya kuwa mimi nimo mwake Baba, naye Baba yumo mwangu mimi! Lakini mkishindwa, nitegemeeni kwa ajili ya kazi zizo hizo![#Yoh. 10:25,38; 14:20.]

12Kweli kweli nawaambiani: Mwenye kunitegemea naye yeye atazifanya kazi, ninazozifanya mimi, naye atafanya zilizo kubwa kuliko hizi, maana mimi nakwenda kwa Baba.[#Mar. 16:19-20.]

13Tena lo lote, mtakaloliomba katika Jina langu, nitalifanya, Baba apate kutukuzwa, kwa kuwa yumo mwake Mwana.[#Yoh. 15:7; Mar. 11:24.]

14Mtakaloniomba katika Jina langu, nitalifanya.[#Yoh. 16:23-24; 1 Yoh. 5:14-15.]

Kiagio cha Roho Mtakatifu.

15*Mkinipenda yashikeni maagizo yangu!

16Nami nitamwomba Baba, naye atawapa mtuliza mioyo mwingine, akae pamoja nanyi kale na kale.[#Yoh. 15:10; 1 Yoh. 5:3.]

17Ndiye Roho wa kweli, ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni, wala haumtambui. Ninyi mnamtambua, kwani anakaa kwenu, naye atakuwamo mwenu.[#Yoh. 14:26; 15:26; 16:7; Yes. 51:12.]

18Sitawaacha peke yenu, nitakuja kwenu.[#Yoh. 16:13; 7:39.]

19Bado kidogo ulimwengu hautaniona tena, lakini ninyi mtaniona, kwani mimi nipo ninaishi, nanyi mtakuwa mnaishi.[#Yoh. 16:16; 20:20.]

20Siku ile mtatambua ninyi, ya kuwa mimi nimo mwake Baba yangu, nanyi mmo mwangu, nami nimo mwenu.[#Yoh. 17:21-23.]

21Aliye na maagizo yangu, akiyashika, huyo ndiye mwenye kunipenda. Lakini mwenye kunipenda atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda nimwonyeshe, nilivyo.*[#2 Kor. 3:18.]

22Yuda, lakini siye Iskariota, akamwambia: Bwana, imekuwaje, ukitaka kutuonyesha sisi, ulivyo, usipovionyesha wao wa ulimwengu?[#Tume. 10:40-41.]

23*Yesu akajibu, akamwambia: Mtu akinipenda atalishika Neno langu, naye Baba yangu atampenda, nasi tutamfikia, tufanye makao kwake.[#Yoh. 13:34; 14:21; Fano. 8:17; Ef. 3:17.]

24Asiyenipenda hayashiki maneno yangu; nalo Neno, mnalolisikia, silo langu, ila la Baba aliyenituma.[#Yoh. 7:16.]

25Haya nimewaambia nikingali kwenu.

26Lakini yule mtuliza mioyo, yule Roho Mtakatifu, Baba atakayemtuma katika Jina langu, ndiye atakayewafundisha yote na kuwakumbusha yote, mimi niliyowaambia ninyi.[#Yoh. 14:16.]

27Nawaachia utengemano, utengemano wangu nawapani. Mimi siwapi, kama ulimwengu unavyowapa. Mioyo yenu isizizimke, wala isiogope![#Yoh. 16:33; Fil. 4:7.]

28Mmesikia, nilivyowaambia: Nakwenda zangu, tena nitawajia. Kama mngenipenda, mngefurahi, ya kuwa nakwenda kwa Baba, kwani Baba ni mkubwa kuliko mimi.[#Yoh. 14:3,6,18.]

29Sasa nimewaambia, yanapokuwa hayajafanyika bado, mpate kunitegemea, yatakapofanyika.

30Sitasema nanyi mengi tena, kwani mtawala ulimwengu huu anakuja; lakini hakuna tena, anachokiweza kwangu mimi,[#Yoh. 12:31; Ef. 2:2.]

31ni kwamba tu, ulimwengu upate kutambua, ya kuwa nampenda Baba, nikafanya hivyo, Baba alivyoniagiza., Inukeni, tutoke humu!*[#Yoh. 10:18.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania