Yohana 21

Yohana 21

Yesu anatokea wanafunzi saba.

1Kisha Yesu akajijulisha tena kwa wanafunzi kwenye bahari ya Tiberia. Alivyojijulisha ni hivyo:

2walikuwako pamoja Simoni Petero na Toma anayeitwa Pacha na Natanaeli wa Kana wa Galilea na wana wa Zebedeo na wanafunzi wake wengine wawili.[#Yoh. 1:45.]

3Simoni Petero alipowaambia: Nakwenda kuvua, wakamwambia: Nasi tunakwenda pamoja na wewe. Basi, wakaondoka, wakaingia chomboni, lakini usiku ule hawakupata kitu.

4Kulipoanza kucha, Yesu alikuwa amesimama ufukoni, lakini wanafunzi hawakumjua, ya kuwa ndiye Yesu.[#Yoh. 20:14; Luk. 24:16.]

5Yesu alipowauliza: Wanangu, hamna kitoweo? wakamjibu: Hatuna.[#Luk. 24:41.]

6Ndipo, alipowaambia: Utupeni wavu kuumeni kwa chombo, ndiko, mtakakopata! Walipoutupa, tena hawakuweza kuuvuta kwa ajili ya samaki wengi.[#Luk. 5:4-7.]

7Ndipo, yule mwanafunzi, Yesu aliyempenda, alipomwambia Petero: Ni Bwana! Simoni Petero aliposikia, ya kuwa ni Bwana, akajifunga vazi, kwani alikuwa uchi, akajitupa baharini.[#Yoh. 13:23.]

8Wanafunzi wenziwe wakaenda kwa chombo wakiuvuta wavu uliojaa samaki, kwani pwani hapakuwapo mbali, palikuwa kama mikono 200 tu.

9Nao waliposhuka pwani wakaona: moto wa makaa ulikuwa umewashwa, navyo visamaki vilikuwa vimewekwa juu pamoja na mkate.

10Yesu akawaambia: Leteni kidogo katika visamaki hivyo, mlivyovivua sasa hivi!

11Simoni Petero akapanda chomboni, akauvuta wavu ufukoni; wakawamo samaki wakubwa tu 153. Nao wavu haukupasuka, wangawa wengi kama hao.

12Kisha Yesu akawaambia: Njoni, mle! Miongoni mwao hao wanafunzi hakuwamo hata mmoja aliyejipa moyo wa kumwuliza: Wewe u nani? Walimjua, ya kuwa ndiye Bwana.

13Kisha Yesu akaenda, akautwaa mkate, akawagawia, na kitoweo vilevile.[#Yoh. 6:11.]

14Hii ndiyo mara ya tatu, Yesu akijijulisha kwa wanafunzi alipokwisha fufuka katika wafu.

Yesu na Petero.

15*Walipokwisha kula, Yesu akamwuliza Simoni Petero: Simoni wa Yohana, wanipenda kuliko hawa? Akamwambia: Ndio, Bwana, wewe unajua, ya kuwa ninakupenda. Akamwambia: Walishe wana kondoo wangu![#Yoh. 1:42.]

16Alipomwuliza tena mara ya pili: Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia: Ndio, Bwana, wewe unajua, ya kuwa ninakupenda. Akamwambia: Vichunge vikondoo vyangu![#1 Petr. 5:2,4.]

17Alipomwuliza mara ya tatu: Simoni wa Yohana, Wanipenda? Petero akasikitika, kwa sababu alimwuliza mara ya tatu: Wanipenda? akamwambia: Bwana, wewe unayajua yote, wewe unatambua, ya kuwa ninakupenda. Yesu akamwambia: Vilishe vikondoo vyangu![#Yoh. 13:38; 16:30.]

18Kweli kweli nakuambia: Ulipokuwa kijana ulijifunga mwenyewe, ukaenda, ulikotaka. Lakini utakapokuwa mzee utainyosha mikono yako, mwingine akuvike, akupeleke, usikotaka.

19Neno hili alilisema, amwonyeshe kufa, alikotakiwa, amtukuze Mungu nako. Alipokwisha kuyasema haya akamwambia; Nifuate!*[#Yoh. 13:36.]

20Petero alipogeuka akaona, anafuata naye yule mwanafunzi, Yesu aliyempenda, ni yule aliyekuwa ameegamia kifuani pake, walipokuwa wakila jioni, aliyemwuliza: Bwana, ni nani, atakayekuchongea?[#Yoh. 13:23.]

21Basi, Petero alipomwona huyu akamwuliza Yesu: Bwana, na huyu je?

22Yesu akamwambia: Nikitaka, huyu akae, mpaka nitakapokuja, wewe unavikataliaje? Wewe nifuate tu!

23Basi, neno hili likaenea katika ndugu la kwamba: Mwanafunzi huyu hatakufa. Lakini Yesu hakumwambia: Hatakufa, ila: Nikitaka, huyu akae, mpaka nitakapokuja, wewe unavikataliaje?

24Huyu ndiye mwanafunzi aliyeyashuhudia haya na kuyaandika. Nasi twamjua, ya kuwa ushuhuda wake ni wa kweli.[#Yoh. 15:27.]

25Lakini yako hata mengine mengi, Yesu aliyoyafanya. Nayo kama yangaliandikwa moja moja, nadhani, ulimwengu wote usingevitoshea vitabu vitakavyoandikwa.[#Yoh. 20:30.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania