Iyobu 4

Iyobu 4

1Mtu akijaribu kukuambia neno, litakukasirisha?

2Lakini yuko nani awezaye kujizuia, asiseme?

3Tazama, uliowaonya ni wengi, ukashupaza mikono iliyokuwa imelegea.

4Maneno yako yakawainua waliojikwaa, nayo magoti yaliyokuwa yamechoka ukayatia nguvu.

5Lakini sasa mambo yakikufikia wewe, unazimia; yakikugusa wewe nawe, unastuka.

6Hivyo, unavyomcha Mungu, sivyo unavyoviegemea? tena hivyo, njia zako zinavyomwelekea Mungu, sivyo unavyovingojea?

7Kumbuka, kama yuko aliyeangamia akiwa hakukosa? tena wako wapi wanyokao waliotoweshwa?

8Nilivyoviona ni hivi: wenye kulima mapotovu nao wenye kupanda masumbuko, huyavuna yayo hayo.[#Fano. 22:8.]

9Mungu akiwapuzia, huangamia; akiwafokea kwa ukali wake humalizika.

10Sauti zake simba huwa zenye ukali, akinguruma; lakini meno yao wana wa simba yakivunjika,

11nao hukosa nyama za kula; ndivyo, naye simba anavyoangamia, nao watoto wa simba mke hutawanyika.

12Liko neno lililonijia kama mwizi, sikio langu likalipokea, liliponong'onezwa.

13Usiku uliponitia mawazo mengine kwa kuniotesha, ilikuwa hapo, watu wanapoangukiwa na usingizi mzito;

14ndipo, kistusho kiliponipata na kunitetemesha, mifupa yangu yote ikafa ganzi,[#1 Mose 15:12.]

15upepo ukapita usoni pangu, mara nywele za mwili wangu zikajisimamisha,

16kwani pakasimama mfano machoni pangu, nami sikuweza kuutambua vema, jinsi ulivyokuwa; lakini kwa kuwa kimya nikasikia sauti ya kwamba:

17Je? yuko mtu aongokaye kuliko Mungu? Je? yuko wa kiume atakataye kuliko yeye aliyemwumba?

18Tazama! Watumishi wake hawezi kuwategemea, nao malaika zake huwaona, wakikosa.[#Iy. 15:15.]

19Sembuse wao wakaao katika nyumba za udongo, ambazo waliziwekea misingi uvumbini? Wao ndio wanaopondwa, kama ni nondo tu.[#2 Kor. 5:1.]

20Toka asubuhi mpaka jioni husetwasetwa; nao wakiangamia kale na kale, hakuna aviwekaye moyoni.

21Kamba za mahema yao hakatwa, wakingali wamo; kwa kukosa werevu wa kweli hujifia tu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania