Yoeli 3

Yoeli 3

Mapatilizo ya wamizimu.

1Siku zile za huo wakati zitakapotimia,

mtaniona nikiyafungua mafungo ya Yuda na ya Yerusalemu.

2Ndipo, nitakapowakusanya wamizimu wote,

niwapeleke katika bonde la Yosafati;

ndiko, nitakakowakatia shauri

kwa ajili ya ukoo wangu wa Isiraeli ulio fungu langu,

kwa kuwa wamewatawanya kwenye wamizimu,

wakajigawanyia nchi yangu.

3Wao walio ukoo wangu wamewapigia kura,

wakitoa mtoto wa kiume, wajipatie mwanamke mgoni,

tena wamenunua mvinyo kwa mtoto wa kike, wakazinywa.

4Ninyi wa Tiro na wa Sidoni mwanitakiaje?

Nanyi nyote mkaao upande wa Wafilisti?

Je? Ninyi mwataka kunilipisha niliyofanyiziwa?

Au mnacho, mtakacho kunifanyizia?

Sasa hivi kwa upesi nitawarudishia matendo yenu,

yaje kuwaangukia vichwani penu.

5Kwani mmezichukua fedha zangu na dhahabu zangu,

nayo mapambo mazuri yaliyonipendeza

mmeyapeleka katika majumba ya miungu yenu.

6Nao wana wa Yuda na wa Yerusalemu mmewauzia wana wa Wagriki,

mpate kuwapeleka mbali, wasirudi mipakani kwao.

7Lakini mtaniona, nikiwainua mahali hapo, mlipowauzia,

nitakapowarudishia matendo yenu, yaje kuwaangukia vichwani penu.

8Kisha nitawauza wana wenu wa kiume na wa kike

na kuwatia mikononi mwao wana wa Yuda,

nao watawauzia Wasaba, kwa kuwa ni taifa likaalo mbali;

kwani Bwana ndiye aliyevisema.

Wokovu na utukufu wao walio ukoo wa Bwana.

9Yatangazeni haya kwa mataifa! Kisha eueni vita!

Wainueni wenye nguvu!

Wote walio mafundi wa vita na waje na kujipanga!

10Yafueni majembe yenu, yawe panga,

navyo visu vyenu, viwe mikuki!

Naye aliye mnyonge sharti aseme: Mimi ni mwenye nguvu!

11Pigeni mbio, mje mkusanyike,

ninyi mataifa yote mkaao na kuwazunguka!

Nawe Bwana, wapeleke wanguvu wako, wawatelemkie kuko

huko!

12Mataifa na waimbe, waje huko bondeni kwa Yosafati!

Kwani ndiko, nitakakokaa, niwahukumu

wao wa mataifa yote wakaao na kuwazunguka.

13Haya! Leteni miundu! Kwani mavuno yameiva.

Njoni, mkanyage! Kwani kamulio limejaa,

mapipa nayo yanamwagikia, kwani mabaya yao ni mengi.

14Yako makundi ya watu mengi na mengi

huko bondeni kunakokatwa mashauri,

kwani siku ya Bwana iko karibu huko bondeni kunakokatwa mashauri.

15Jua na mwezi umeguiwa na giza, nazo nyota zimekoma

kuangaza.

16Ndipo, Bwana atakaponguruma mle Sioni,

ataivumisha sauti yake mle Yerusalemu,

mbingu na nchi zitetemeke.

Lakini Bwana atakuwa kimbilio lao walio ukoo wake

na ngome yao walio wana wa Isiraeli.

17Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi Bwana ni Mungu wenu

akaaye Sioni penye mlima wangu mtakatifu.

Nao Yerusalemu utakuwa mji mtakatifu, msimopita wageni

tena.

18Siku ile itakuwa, milima idondoe mvinyo mbichi,

navyo vilima vitachuruzika maziwa,

navyo vijito vyote vya Yuda vitaleta maji mengi.

Kisha Nyumbani mwa Bwana mtatokea chemchemi,

italinywesha Bonde la Migunda.

19Misri itakuwa mapori tu,

nayo Edomu itakuwa nyika yenye mapori matupu,

kwa kuwa wamewakorofisha wana wa Yuda,

wakamwaga katika nchi yao damu zao wasiokosa.

20Lakini Yuda itakaa watu kale na kale,

namo Yerusalemu watakaa vizazi kwa vizazi.

21Ndivyo, nitakavyozilipiza damu zao, ambazo sikuzilipiza

bado.

Naye Bwana atakuwa anakaa Sioni!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania