The chat will start when you send the first message.
1Kisha Yosua akayakusanya mashina yote ya Waisiraeli huko Sikemu, akawaita wazee wa Waisiraeli na wakuu wao na waamuzi wao na wenye amri wa kwao, wakajipanga mbele ya Mungu.
2Ndipo, Yosua alipowaambia watu wote: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wenu anavyosema: Tangu kale baba zenu, walipokaa ng'ambo ya huko ya lile jito kubwa, naye Tera, babake Aburahamu na babake Nahori, walitumikia miungu mingine.[#1 Mose 11:26; 31:19; 35:2.]
3Ndipo, nilipomchukua baba yenu Aburahamu na kumtoa ng'ambo ya huko ya lile jito kubwa, nikamtembeza katika nchi yote ya Kanaani, nao walio wa uzao wake nikawazidisha kuwa wengi nilipokuwa nimekwisha kumpa Isaka.
4Naye Isaka nikampa Yakobo na Esau, naye Esau nikampa milima ya Seiri, aichukue, iwe yake, lakini Yakobo na wanawe wakashuka kwenda Misri.[#1 Mose 32:3; 46:6.]
5Kisha nikamtuma Mose na Haroni, nikaipiga nchi ya Misri kwa hayo matendo, niliyoyafanya huko kwao, kisha nikawatoa ninyi.[#2 Mose 3:10.]
6Nilipowatoa baba zenu huko Misri, nanyi mlipofika baharini, Wamisri wakapiga mbio kuwafuata baba zenu kwa magari na kwa farasi mpaka kwenye Bahari Nyekundu.[#2 Mose 12:33.]
7Walipomlilia Bwana, akaangusha giza jeusi, liwe katikati yenu na Wamisri; halafu akaleta bahari, iwatose na kuwafunika. Macho yenu yaliyaona hayo, niliyowafanyizia Wamisri, kisha mkakaa nyikani siku nyingi.[#2 Mose 14:10.]
8Kisha nikawapeleka katika nchi ya Waamori wanaokaa ng'ambo ya huko ya Yordani; walipopiga vita nanyi, nikawatia mikononi mwenu, mkaichukua nchi yao, nilipowaangamiza machoni penu.[#4 Mose 21:25,31.]
9Balaka, mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, alipoondoka kupigana na Waisiraeli, tena alipotuma kumwita Bileamu, mwana wa Beori, awaapize ninyi,[#4 Mose 22.]
10sikutaka kumsikia Bileamu, naye hakuwa na budi kuwabariki ninyi, nikawaponya mkononi mwake.[#4 Mose 23:11,20.]
11Kisha mkauvuka Yordani, mkafika Yeriko; tena hapo, wenyeji wa Yeriko, Waamori na Waperizi na Wakanaani na Wahiti na Wagirgasi, Wahiwi na Wayebusi, walipopigana nanyi, nikawatia mikononi mwenu,[#Yos. 3:14; 6:1.]
12Nikatanguliza mbele yenu mavu, nao wakawafukuza mbele yenu wale wafalme wawili wa Waamori, msichomoe upanga, wala msitumie upindi.[#2 Mose 23:28.]
13Nikawapa ninyi nchi, msiyoisumbukia, nayo miji, msiyoijenga, mkakaa humo, mkapata kula mazao ya mizabibu na ya michekele, msiyoipanda.[#5 Mose 6:10-11.]
14Sasa mwogopeni Bwana na kumtumikia kwa mioyo yote na kwa welekevu, mkiiacha miungu, baba zenu waliyoitumikia ng'ambo ya huko ya lile jito kubwa nako kule Misri, mpate kumtumikia Bwana.[#2 Mose 32; Yos. 24:2.]
15lakini kama ni vibaya machoni penu kumtumikia Bwana, basi, jichagulieni siku hii ya leo, mtakayemtumikia, kama ni miungu, baba zenu waliyoitumikia ng'ambo ya huko ya lile jito kubwa, au kama ni miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi nao waliomo nyumbani mwangu tutamtumikia Bwana.[#Mat. 6:24.]
16Ndipo, watu walipojibu wakisema: Shauri hili na litukalie mbali la kumwacha Bwana na kutumikia miungu mingine.
17Kwani Bwana ni Mungu wetu. Yeye ndiye aliyetuleta huku na kututoa sisi na baba zetu katika nchi ya Misri nyumbani, tulimokuwa watumwa, naye ndiye aliyevifanya vile vielekezo vikubwa machoni petu, naye alituangalia katika njia zote, tulizokwenda, na katika makabila yote, ambao tulipita katika nchi zao.
18Yeye Bwana ndiye aliyeyafukuza makabila yote machoni petu, nao Waamori waliokuwa wenyeji wa nchi hii; kwa hiyo nasi tutamtumikia Bwana, kwani yeye ni Mungu wetu.
19Naye Yosua akawaambia watu: Hamwezi kumtumikia Bwana, kwani yeye ni Mungu mtakatifu, tena Mungu mwenye wivu, kwa hiyo hatayavumilia mapotovu yenu na makosa yenu.[#2 Mose 20:5; 5 Mose 5:29.]
20Kwani mtakapomwacha Bwana na kutumikia miungu migeni, atawafanyizia mabaya tena, awamalize ninyi akiacha kuwafanyizia mema.
21Lakini watu wakamwambia Yosua: Hivi havitakuwa, kwani tutamtumikia Bwana.
22Ndipo, Yosua alipowaambia watu: Ninyi mnajishuhudia wenyewe, ya kuwa mmejichagulia kumtumikia Bwana; nao wakaitikia kwamba: Tunajishuhudia hivyo.
23Naye akasema: Sasa iondoeni miungu hiyo migeni iliyoko kwenu! Kisha ielekezeni mioyo yenu kumtazamia Bwana Mungu wa Isiraeli![#1 Mose 35:2.]
24Ndipo, watu walipomwambia Yosua: Bwana Mungu wetu ndiye, tutakayemtumikia na kuisikia sauti yake.
25Ndivyo, Yosua alivyoagana na watu siku hiyo akiwatolea maongozi na maamuzi huko Sikemu.[#2 Fal. 23:3.]
26Kisha Yosua akayaandika haya mambo yote katika kitabu cha Maonyo ya Mungu, akachukua jiwe kubwa, akalisimika chini ya mkwaju uliokuwako huko kwenye Patakatifu pa Bwana.[#1 Mose 35:4; Amu. 9:6.]
27Kisha Yosua akawaambia watu wote: Tazameni! Jiwe hili na lituwie shahidi! Kwani limeyasikia maaneno yote, Bwana aliyoyasema na sisi. Kwa hiyo litakuwa shahidi lenu, msimwongopee Mungu wenu![#1 Mose 31:48; Yos. 22:27.]
28Kisha Yosua akawapa watu ruhusa kwenda kwao kila mtu kwenye fungu lake.
29Ikawa, hayo yalipomalizika, akafa Yosua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, mwenye miaka 110.
30Wakamzika katika mipaka ya fungu lake huko Timunati-Sera ulioko mlimani kwa Efuraimu upande wa kaskazini wa mlima wa Gasi.[#Yos. 19:50.]
31Nao Waisiraeli wakamtumikia Bwana siku zote, Yosua alizokuwapo, nazo siku zote, walizokuwapo wale wazee waliokaa siku nyingi kuliko Yosua, ndio wale walioyajua yale matendo yote, Bwana aliyowatendea Waisiraeli.[#Amu. 2:7.]
32Nayo mifupa ya Yosefu, wana wa Isiraeli waliyokuja nayo walipotoka Misri, wakaizika Sikemu katika fungu lile la shamba, Yakobo alilolinunua kwa vipande mia vya fedha kwa wana wa Hamori, babake Sikemu; kwa hiyo hilo fungu likawa lao wana wa Yosefu.[#1 Mose 33:19; 50:25.]
33Elazari, mwana wa Haroni, alipokufa, wakamzika huko Gibea uliokuwa mji wa mwanawe Pinehasi, maana ndio, aliogawiwa milimani kwa Efuraimu.