The chat will start when you send the first message.
1Mimi Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo, niliye ndugu wa Yakobo, nawaandikia ninyi mwitwao, mkapendwa kwa kuwa wake Mungu Baba, mkalindwa, mmfikie Kristo.[#Mat. 13:55.]
2Upole na utengemano na upendo uwafurikie!
3Wapendwa, nimejikaza sana kuwaandikia ninyi mambo ya wokovu wetu sisi sote, nikashurutishwa moyoni kuwaandikia na kuwahimiza, mlipiganie tegemeo, watakatifu walilokwisha kupewa, liwe lilo hilo.[#1 Tim. 1:18.]
4Kwani wako watu waliojiingiza kwa kufichaficha, walivyo, lakini hukumu yao imekwisha kuandikwa kale kwamba: Hawamchi Mungu, maana hupenda uasherati, kisha husema: Mungu wetu hutuondolea hayo, naye yeye aliye mkuu peke yake, Bwana wetu Yesu Kristo humkana.
5Lakini nataka kuwakumbusha ninyi mliokwisha kuyajua hayo yote: Yeye Bwana aliyewaokoa wao wa ukoo wetu katika nchi ya Misri ndiye aliyewaangamiza waliokataa kumtegemea tena.[#4 Mose 14:35; 1 Kor. 10:5.]
6Hata malaika, wasioulinda ukuu wao wakijiendea na kuyaacha makao yao, amewafunga penye giza kwa mapingu yasiyovunjika, waingoje ile siku kubwa, wahukumiwe.[#1 Mose 6:2; Yoh. 8:44; 2 Petr. 2:4,9.]
7Hata wenyeji wa Sodomu na Gomora nao wa vijiji vilivyokuwako pembenipembeni walihimiza mambo ya ugoni vivyo hivyo na kufuata miili migeni; nalo lipizi lao, walilolipata la kuteketezwa na moto usiozimika, ni kielezo cha kutuonya.[#1 Mose 19:4-25.]
8Ndivyo, wale wanavyofanana navyo, wako kama wenye ndoto, huichafua miili yao, huutangua ukuu, huwatukana wenye utukufu.[#2 Petr. 2:10.]
9Lakini Mikaeli aliye malaika mkuu, aliposhindana na Msengenyaji na kubishana naye kwa ajili ya mwili wa Mose, hakujipa moyo wa kumwumbua na kumtukana, ila alisema tu: Bwana na akukemee![#Dan. 12:1; Zak. 3:2.]
10Lakini hao huvitukana, wasivyovijua; navyo vile, wanavyovijua, maana vya miili yao, huvijuaa kama nyama wasiojua kitu, kisha huozeshwa mumo humo.[#2 Petr. 2:12.]
11Yatawapata hao, kwani hushika njia ya Kaini, wakapotea na kutumbukia katika mshahara wa Bileamu, wakajiangamiza katika mapingano ya Kora.[#1 Mose 4:8; 4 Mose 16; 31:16; Ufu. 2:14.]
12Hao huwa kama madoa wakijiingiza hapo, mnapogawiana vyakula vya upendano; napo hapo hujilisha wenyewe tu pasipo woga! Tena huwa kama mawingu yasiyo na mvua, yanayochukuliwa na nguvu za upepo, huwa kama miti isiyo na majani, isiyozaa matunda, imekufa mara mbili, imeng'oka kabisa.[#2 Petr. 2:13,17.]
13Tena huwa kama mawimbi makali ya bahari yanayoyatoa mambo yao yaliyo yenye soni kuwa kama mapovu, huwa kama nyota zipoteazo ovyo, ambazo fungu lao, walilowekewa, ni lile giza jingi lililoko kale na kale.[#Yes. 57:20.]
14Mambo yao aliyafumbua Henoki aliyekuwa mtu wa saba tangu Adamu, aliposema: Tazameni, Bwana anakuja pamoja na malaika zake watakatifu maelfu na maelfu,[#1 Mose 5:21.]
15awahukumu na kuwapatiliza wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya matendo yote, waliyoyafanya kwa kuacha kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote, wakosaji hao wasiomcha Mungu walivyoyasema.[#Mat. 25:31.]
16Hao hunung'unika na kuchukizwa navyo, waliyoyapata yote, wakiendelea na kuzifuata tamaa zao; vivywa vyao husema maneno makuu, wenyewe hutazama nyuso za watu, waonee ya kupewa.[#2 Petr. 2:10,18.]
17Lakini ninyi, wapendwa, myakumbuke maneno yaliyosemwa kale na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo,
18maana waliwaambia ninyi: Siku za mwisho kutakuwa na wafyozaji watakaoendelea na kuzifuata tamaa zao wenyewe kwa kuacha kumcha Mungu.[#1 Tim. 4:1; 2 Petr. 3:3.]
19Hao ndio wanaoleta matengano, ni wa kimtu tu, lakini Roho hawanayo.[#1 Kor. 2:14.]
20Lakini ninyi, wapendwa, jijengeni wenyewe mkiyatumia mategemeo yenu matakatifu kuwa msingi! Mwombeni Mungu kwa nguvu ya Roho takatifu![#Ef. 6:18; Kol. 2:7; 1 Tes. 5:11.]
21Jilindeni wenyewe, mkae na kumpenda Mungu! Ingojeni huruma ya Bwana wetu Yesu Kristo, itokee na kuwapatia uzima wa kale na kale!
22Kama wako walio bado wenye mambo mawili, wahurumieni!
23Waokoeni mkiwapokonya motoni! Lakini wako na wengine, mwahurumie kwa kuogopa! Sharti mchukizwe nazo nguo zao zilizochafuliwa na miili yao![#Yak. 5:19,20; Ufu. 3:4.]
24Lakini yeye anaweza kuwalinda, msijikwae, na kuwaweka, mtekee penye utukufu wake na kushangilia kwa kuwa pasipo kilema,[#Fil. 1:10; 1 Tes. 5:23.]
25yeye ni Mungu peke yake na mwokozi wetu, maana alimtuma Yesu Kristo, Bwana wetu. Utukufu ni wake na ukuu na uwezo na nguvu kuanzia kale, siku zilipoanzia, na sasa na siku zitakazokuwa zote! Amin.[#Rom. 16:17; 1 Tim. 1:17.]